Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie katika hoja hii ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nitoe pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri unazofanya. Mheshimiwa Waziri vilevile nikupe pongezi kubwa kwa kupokea ushauri mzuri wa Mheshimiwa Juma Nkamia na sote kwa kusema kwamba Bunge lianzishe studio yake, hongera sana.
Napenda kutoa pongezi pia kwa Wizara hii kwamba katika vyombo vya habari Tanzania imeonekana kuwa ni nchi ambayo imeruhusu kuwa na vyombo vingi vya habari, hongereni sana kwa hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaongea yote kwa mustakabali mzima wa Taifa kuhusu Wizara hii, nianze Mheshimiwa Waziri katika mkoa wangu wa Simiyu tuna Chuo cha Michezo cha Malya, tunaomba Chuo cha Michezo cha Malya kitengewe pesa kwa maana ya kukiendeleza. Tunatambua eneo la Kanda ya Ziwa pamoja na mkoa wangu wa Simiyu kuna vipaji vingi sana vya utamaduni pamoja na michezo ya mpira. Hivyo tunaomba chuo hicho kiongezewe zana pamoja na walimu kuweza kutoa elimu ya michezo katika mkoa wetu na kwa manufaa ya Taifa zima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkoa wetu wa Simiyu ni mkoa mpya ambao tulikuwa tumeji-attach na mkoa wa Shinyanga kabla, tulikuwa tuna kiwanja chetu kama mkoa maana ya kiwanja cha Kambarage kilikuwa kinawakilisha mkoa japo ni kiwanja cha Chama chetu cha Mapinduzi, lakini sasa mkoa wetu hauna kiwanja! Katika pesa ya maendeleo niliyoona hapa sijaona eneo ambalo imetengwa pesa maalum kwa kuendeleza viwanja au kujenga viwanja! Kwa hiyo, tunaomba katika mkoa wa Simiyu Wizara itutizame kama mkoa mpya, mtuwekee kiwanja cha mpira na hasa mpira wa miguu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kutoa maoni au ushauri pia kwa Wizara hii. Upande wa mpira wa miguu au timu ya Taifa kwa maana ya Taifa Stars, Tanzania tunategemea sana tutengeneze timu ya Taifa kupitia timu za ligu kuu. Kutengeneza timu ya Taifa kupitia timu ya ligi kuu ni kitu kimoja kigumu sana, tujikite katika kuanzisha football academy, hii ndiyo njia pekee ambayo inaweza ikatusaidia kutengeneza timu ya Taifa na kuipeleka katika Kombe la Dunia, lakini tukisema tutegemee premier league, wachezaji kutoka Simba na Yanga itakuwa ni tatizo kubwa sana kutengeneza timu ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu Nigeria na Ivory Coast wameweza kutengeneza timu zao za Taifa vizuri, kwa kuwa na football academies za kutosha zinazofaa, zinawajenga vijana, zinajenga wachezaji wazuri ambao wanawakilisha timu hizo kwenda kwenye makombe mbalimbali Afrika pamoja na Kombe la Dunia. Tunaomba Wizara hii katika mkakati tuliouona hapa, haijatengwa pesa nzuri ya kuanzisha football academies. Ukienda pale TFF wana mkakati na mpango mkubwa sana wa kuanzisha au wa kuboresha hizi timu, lakini kwa kutumia premier league peke yake hatuwezi kutengeneza timu ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika premier league, unapokuwa na timu za premier league tubadilike sasa! Tunapokuwa na ligi yetu ambayo mara nyingi inafadhiliwa na Vodacom tunataka iwe ni ligi ambayo ni commercial, ligi ya kibiashara. Tunapoweka wachezaji katika hizi timu zinazocheza premier league, tunataka tucheze kibiashara kama wanavyofanya Uingereza na nchi nyingine. Tunataka ule mkakati wa kusema timu isajili wachezaji wasizidi watano kutoka nje, hii naomba niseme Mheshimiwa Waziri haifanani na bidhaa. Tuna-discourage bidhaa kuingizwa au ku-import bidhaa kutoka nje, lakini kwenye football ni kitu kingine. Kwenye football tunahitaji ku-import wachezaji ili waweze ku-inspire wachezaji wetu local wacheze kiushindani na wachezaji wetu ambao ni wachezaji wa ndani waweze kuwa inspired kucheza kwa kiwango cha Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ukitizama timu kama Azam, leo tunamwekea Azam limit asisajili zaidi ya wachezaji watano kutoka nje, wakati akitoka hapo anakwenda kucheza champions league ya Afrika, champions league ya Afrika ni biashara. Akishinda kwenye champions league ya Afrika tunaingiza pesa na sifa katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia TP Mazembe ya Congo imesajili wachezaji kutoka nje karibu kumi na kitu! Na wanaposhinda champions league ya Afrika sifa inakwenda Congo. Lakini sisi tunazuia na wachezaji wetu hawawezi kufikia kile kiwango tunapowapeleka kule kushindana na wale wachezaji wengine timu zetu zinakuwa ni kichwa cha mwendawazimu, zinafungwa zinarudi. Yanga sasa hivi wameenda juzi wamefungwa huko wamerudi, wameenda kuungana na yale mashindano ya timu ambazo hazijui na yenyewe tuwaombee Mungu, lakini hatuna mikakati ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kuchangia kwenye suala hili hili la michezo, kuhusu rushwa kwenye michezo. Rushwa imetawala kwa marefa, tunaomba Wizara kwa kushirikiana na TFF muangalie hili suala, kwa kweli rushwa ni hatari, PCCB ikiwezekana ihusishwe katika kupambana na rushwa kwenye michezo. Waamuzi wanasababisha timu zifungwe ambazo hazistahili kufungwa! Waamuzi wanaharibu mpira na kusababisha fujo wakati mwingine kwa sababu tayari wameshachukua mlungula mfukoni! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta referee anaamua ndivyo sivyo, matokeo yake timu nyingine zimezoea kununua mechi kwa sababu wamezoea kuhonga ma-referee, wanahonga hadi wachezaji, mechi zinapangwa matokeo, mnashinda humu Tanzania mnakuwa mabingwa mkitoka nje mnafungwa. Mnajisifu mnajua mpira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili litizamwe kwa upana wa kutosha. Mheshimiwa Waziri tunaomba mshirikiane na TFF mkomeshe rushwa kwenye michezo. Leo hapa Mheshimiwa Zitto katoa ushauri mzuri kwamba betting na hizi bahati nasibu ndizo zinazoendesha hizi ligi kubwa duniani, huwezi kuendesha ligi kubwa duniani wakati tayari michezo ina rushwa. Huwezi kufanya betting ya kwamba leo Simba atafungwa na Yanga wakati kuna watu wameshaamua Yanga ifungwe mezani au wengine wameamua Simba ifungwe mezani. Uamuzi umeshatoka mezani. Hiyo betting itaingiza pesa kiasi gani? Siwezi ku-bet mimi kwenye kitu ambacho kiko corrupt. Ndiyo maana betting za Uingereza zinakuwa na maana kwa sababu wamepunguza kiwango cha rushwa, watu kweli wanakaa wanaanza ku-bet. Wana-bet, wana-predict kutokana na kwa sababu michezo inayochezwa kule Uingereza na sehemu zingine ile hali ya rushwa haipo. Kwa hiyo, ndugu zangu mlitizame kwa kina suala la rushwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia pia ufadhili wa timu. Sasa hivi kwa mfano, kuna timu zimeshinda ubingwa wa mikoa, zimegawanywa Kanda mbalimbali, kwa mfano sisi kwetu kuna timu inatakiwa iende Kagera kufanya kambi kwa maana ya kuingia kwenye mashindano ya Kitaifa, hakuna ufadhili. Wabunge ndiyo tunaoombwa tuchangie pesa ya kupeleka zile timu kwenye Kanda. Hakuna mkakati wa Serikali na TFF wa kuzifadhili hizi timu ziende zikacheze. Matokeo yake Wabunge ndiyo mnaokamuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, kuna ndugu yangu mmoja tulishirikiana naye alikuwa anafadhili timu, timu ikawa inafanya vizuri, vijana wanacheza, tunatoa pesa. Yule mfadhili mkubwa anatoa pesa timu inakwenda kucheza, ikafika kiwango pesa hamna, timu ina uwezo. Yule bwana ikabidi ahonge timu ifungwe ili irudi nyumbani kwa sababu watu hawachangii pesa kwenye michezo na hawaoni umuhimu wa kuchangia pesa kwenye michezo. Kwa hiyo, tunaomba elimu itolewe, tunaomba Serikali iwe na mkakati kabisa thabiti wa kuweza kuhakikisha tunaendeleza michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la viwanja nimeliongea hapo mwanzo, hata hatujui tuwaombe TAMISEMI Tuombe kwenye Wizara! Nani anahusuka na viwanja? Tunaomba Wizara ishikilie hili suala, ishikilie michezo kuanzia kwenye shule ya msingi tusiachie TAMISEMI, tusiachie Wizara ya Elimu, mshikilie michezo kuanzia chini mpaka juu, kwa maana ya kuanzisha football academies na kusimamia michezo kwa ujumla, ili tuweze kutengeneza timu bora za michezo ya aina mbalimbali. Sasa hivi uwezo huo uko Jeshini tu.
Mheshimiwa Mwenyekiit, kumbuka zamani tulipata watu waliotuwakilisha Tanzania kwenye michezo ya Kimataifa wakaleta sifa akina Filbert Bayi, akina Juma Ikangaa, Samson Ramadhan, Iswege Christopher, Ndassa Mafuru, Samwel Mwang‟a, Hatii Shamba, Restituta Joseph, Hawa wote walitokana na Jeshi, lakini sisi kama Wizara tumeshindwa kutengeneza hawa watu. Ina maana Jeshi peke yake ndiyo lina uwezo wa kutengeneza hawa watu. Kwa hiyo, tunaomba tushirikiane, ili tuweze kutengeneza timu zetu pamoja na timu ya olyimpic.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. Nakushukuru mno kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja, lakini marekebisho hayo naomba yasikilizwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.