Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Juma Selemani Nkamia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii, pia nimshukuru sana Mwenyezi Mungu Subhuhana Wataalah kwa kuniamsha salama na mimi nitoe mchango wangu katika bajeti hii ya Wizara ya Habari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ambaye kwangu mimi binafsi ni mwalimu wangu wa darasani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana mama yangu Makamu wa Rais, nimpongeze Waziri Mkuu na hali kadhalika nimpongeze rafiki yangu Mheshimiwa Nape Moses Nnauye na Naibu Waziri wake, Dada yangu Wambura kwa kazi nzuri mliyoanza nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utakuwa kwenye ushauri zaidi. Kwanza ni TBC, mimi nimekulia pale. Ametoa mchango mzuri sana Mheshimiwa Zitto Kabwe, lazima tufike wakati tufanye maamuzi! BBC inaendeshwa kwa tv license, kila mwenye televisheni analipa paundi 100 kama sikosei ilikuwa wakati naishi kule, kwa ajili ya kuendesha BBC. Zaidi ya wafanyakazi 4,000 wa BBC katika channel zote – wana lugha karibu 143, wanaendesha kwa kutumia tv license! Fanyeni maamuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, msiogope kwamba leo tuki introduce tv license wananchi watakasirika – wanataka kuona matangazo! They have to pay! Tutaondoa hii lawama, tv haionekani, haifanyi nini! Hilo lilikuwa wazo langu la kwanza. Mheshimiwa Zitto amezungumza pale, eh kabisa, anzisheni tu. Ninaamini Wabunge mkijenga hoja vizuri, TBC watapata fedha, wana hali mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni mwaka wa sita kwangu hapa Bungeni, TBC hawana hela, mwaka nenda mwaka rudi, decide sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni michezo. Nasikia magari ya TFF yamekamatwa leo wanadaiwa TRA hawajalipa, wanadaiwa karibu shilingi bilioni 1.16. Kodi iliyotokana na mchezo kati ya Taifa Stars na Brazil. Ninavyofahamu Serikali ilikopa fedha shilingi bilioni tatu kutoka NMB kusimamia mchezo ule. TFF wameshalipa ama hela yao iliyochukuliwa na TRA karibu shilingi milioni 407. Waziri Nape nikuombe kaka yangu, kaa na TFF, kaa na TRA kodi hii wala haiwahusu TFF. Fedha yao inachukuliwa bila sababu hapa, TFF hawana hela wale, kaa nao, kila kitu kinajulikana. Kulikuwa na Kamati Maalum ambayo ilikuwa inasimamia mchezo ule kati ya Tanzania na Brazil uliofanyika uwanja wa Taifa wakati wa maandalizi ya Fainali za Kombe ya Dunia nchini Afrika ya Kusini, TFF ilikuwa ni umbrella tu lakini hawakuhusika na kitu chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunazungumza kuinua michezo, Utainuaje michezo wakati ngazi za chini msimamizi mwingine, ngazi za juu msimamizi mwingine! Ndiyo mimi nasema mfumo wetu D by D we have to sit down tuutafakari kwa kina umetusaidia?
Leo Waziri wa TAMISEMI ndiye anasimamia UMISETA, anasimamia UMITASHUMTA, hana wataalam wa michezo, wewe ndiyo una wataalam, utakwendaje? Kaeni chini, sisi kazi yetu ni kushauri tu. Kaeni chini muangalie, hivi TAMISEMI wakisimamia UMISETA are they capable? Wana wataalam? UMITASHUMTA huko ambako mnazalisha wachezaji, nani anasimamia na wataalam wapo? Pamoja na kazi nzuri sana inayofanywa na Baraza la Michezo chini ya Mzee wangu Dionis Malinzi, nampongeza sana, lakini hatuwezi kufikia malengo bila kufanya mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo nilitaka nilisemee kidogo, angalieni leo kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Ndugu Charles Boniface Mkwasa “Master” anadai mshahara! Mwaka jana hapa tulipitisha bajeti ya mshahara wa makocha wa timu za Taifa, kwa nini msimlipe? Kwani mkimlipa hizo fedha dola 12,000 alizokuwa analipwa mzungu kuna dhambi gani na anafundisha national team? Ameonesha kwamba anaweza kufanya kazi yake vizuri na mimi naamini kwa dola 12,000 zile mkampa Mkwasa mkampa na wasaidizi wake, wanaweza kufanya wonders kwa ajili ya Taifa letu. Kwa nini mmezuia? Mlipeni tu eeh. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni vyama vya michezo. Vyama vingi vya michezo havina ofisi. Uwanja wa Taifa nilikuona Mheshimiwa Nape siku moja wale Wachina pale wanatengeneza kiwanda cha mbao, kwa nini msiwape vyama vya michezo ofisi mle? Uwanja ule ni mkubwa na watawasaidia zaidi hata kwenye ulinzi na kuboresha uwanja ule, wapeni. Leo Chama cha Darts kinatembelea kwenye begi la mtu ambaye ni Mwenyekiti, ndiyo ofisi yake. Wawekeni mle tatizo liko wapi? Mnawakata hela kidogo, kwani shida iko wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni kuhusu vyombo vya habari. Nitakuwa sijatenda haki sana bila kuwazungumzia waandishi wa habari wenzangu. Waandishi wengi wa habari wa Tanzania hawana mikataba ya kudumu ya kazi. Wengi wanalipwa per piece, hawana bima na hawajui mustakabali wa maisha yao ya baadaye. Leteni sheria hapa ndani ya Bunge tuunde sheria, ama Bunge litengeneze sheria, vyombo vya habari viwe na wajibu wa kuhakikisha waandishi wao wa habari wana mikataba ya kazi, wana bima na wanakuwa na mustakabali wa maisha yao ya baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, waandishi wa habari wengi wanalalamika sana hakuna mikataba, hakuna nini. Wanatembea kwenye vumbi. Wanalipwa kutokana na piece yake aliyokwenda kutafuta. Tukileta sheria hapa, Bunge likatunga sheria, nina imani kabisa kutaundwa bodi maalum ya waandishi wenyewe, kwa hiyo Serikali itakuwa ni ku-monitor tu. Lakini mkiunda bodi maalum ya kusimamia kama zilivyo NBAA kwa ajili ya wahasibu, madaktari wana bodi zao, kwani waandishi wa habari wana dhambi gani? Leteni sheria hapa tufanye kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa lakini siyo kwa umuhimu, niwapongeze sana wasanii wa Tanzania, wanafanya kazi nzuri sana. Wanastahili kweli jasho linalowatoka? Leo kwenye simu humu ukipiga mlio unasikia Diamond, ukipiga hivi unasikia fulani, ukipiga hivi unasikia nani. Je, nani anawajibika kulipa, wanapata kweli haki yao au makampuni ya simu haya yanawatumia tu kama kigezo cha kupata umaarufu? Tufike mahala tuone jambo hili. Wengi wameshauri hapa, ni kweli.
Mimi bahati nzuri nimefanya kazi kwenye nchi nyingine, siyo rahisi ukute Marekani wanapiga wimbo wa Sugu. Kwanza hawamjui na hawana interest naye. Siyo rahisi wimbo wa Koffi Charles Olomide uusikie BBC unless amehojiwa, kwetu tumeiga mambo ya ajabu sana. Stick on that, mimi naamini kabisa tutafika mahali tutarudisha heshima ya Taifa letu na wasanii wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema haya naunga mkono hoja. Ahsanteni sana.