Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa ya kuwa mchangiaji wa kwanza katika Mpango wa Maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa uwasilishaji mzuri pamoja na heka heka ambazo tumezipata mwanzoni mwa wiki, lakini Wahenga wanasema kawia ufike. Naomba nijielekeze moja kwa moja katika Hotuba na mapendekezo ya Serikali kuhusiana na Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja, pamoja na vipaumbele vyote ambavyo tumeviweka, ningependa kuona Serikali inaweka kipaumbele katika ujenzi wa reli ya kati. Naungana na Wabunge wote wa mikoa yote ambao wamekuwa wanaliongelea suala la reli ya kati. Tukitaka kupaisha uchumi wetu, tukitaka kuimarisha uchumi wetu bila ya kuwa na reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge naamini kabisa tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, Serikali itakapokuja kufanya hitimisho tunataka kauli iliyokuwa thabiti na wala isiyopinda kuhusiana na nini mikakati yetu ya kujenga reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge, tumeliongea sana, tuliliongelea katika Bunge la Kumi, sasa umefika muda wa utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tungependa kusikia na kuona Mpango wa Serikali katika kuimarisha Bandari ya Dar es Saalam, tuipanue, kuna kazi kubwa ambayo mmeweza kuifanya na nimpongeze sama Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya ya maboresho katika bandari. Bado tunahitaji kupunguza muda wa utoaji mizigo pale na kuongeza ufanisi na ikiwezekana bandari yetu iwe inafanya kazi saa 24. Hii iendane sambamba na upanuzi wa Bandari ya Mtwara, ni bandari ambayo inakuja kwa kasi, tukiweza kuwekeza katika Bandari ya Mtwara, hakika kabisa tutakuwa tumepiga hatua kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nichangie, ni ushirikishwaji wa sekta binafsi. Nchi yetu ina sera nzuri sana ya ushirikishaji wa sekta Binafsi (Private Public Partnership) na tuna sheria ambayo inaendana na hiyo sera ambayo tunayo. Katika upande wa utekelezaji tumekuwa na changamoto kubwa sana, sasa nadhani umefika muda muafaka, miradi yote hii, mipango yetu yote hii, hatuwezi tukaifanya kwa hela ya Serikali, tuishirikishe sekta binafsi katika baadhi ya hii miradi ili sasa Serikali ijikite katika ile mipango mingine mahususi, haya mambo mengine tuweke mazingira mazuri ya uwezeshaji ili sekta binafsi iweze nayo kufanya kazi na tuwape support.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto moja ambayo imekuwa ipo ni kwamba Serikali imekuwa na bureaucracy kubwa sana na tumekuwa tunawa-frustrate sana wawekezaji ambao wanataka kuja kushirikiana na sisi Serikali. Kwa hiyo, naomba sana Serikali itengeneze mazingira mazuri ili kwa wawekezaji binafsi tuweze kuwashirikisha kwa kupitia mpango wa PPP.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kuligusia ni eneo la barabara hususani katika Mkoa wa Dar es Salaam. Tumekuwa tunaliongelea sana jambo hili, Dar es Salaam sasa hivi kwa mtu kutoka maeneo anayoishi kuweza kufika mjini si chini ya masaa mawili na masaa mawili tena wanayatumia kutoka katika maofisi kwenda majumbani. Tumekuwa tunaongelea masuala ya barabara ya mzunguko (ring roads). Niiombe sana Serikali ifike sasa wakati tuwekeze na tuwe na dhamira ya dhati kuwekeza katika barabara za mzunguko katika Mkoa wa Dar es Salaam, tuondokane na hii adha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kufanya investment kubwa kwa wakati mmoja, tunaweza tukawa tumeondokana na hili. Tuna miradi mingi ambayo tumeweza kuifanya, tuna Mradi DMDP, lakini tuje na mradi mahususi ambao utaondoa kero ya usafiri katika Mkoa wa Dar es Salaam. Tunashukuru kwa kuona kwamba zile flyovers zimeanza kujengwa, lakini niongelee kwa upande wa mimi kama Mbunge wa Kigamboni, tumejenga daraja, linakamilika mwezi Machi, lakini tuna changamoto ya approach roads kwa upande wa Kigamboni lakini vilevile kwa upande wa Kurasini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili daraja halitakuwa na manufaa iwapo zile approach roads kuanzia Bendera Tatu mpaka Kamata hazitajengwa. Niiombe sana Serikali, tumefanya investment kubwa sana ya over two hundred billion pale katika Daraja la Kigamboni lakini tuhahitaji zile approach roads ili sasa lile daraja liweze kutumika kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka kuligusia ni upande wa maji. Inasikitisha kuona kwamba nchi yetu ni asilimia ndogo sana ya wananchi ambao wana huduma ya maji. Ni jambo ambalo nalo tumekuwa tunaliongelea kwa muda mrefu sana, tumeweka mikakati na nakumbuka katika Bunge la mwaka jana au mwaka juzi tuliweka mikakati mahususi na tukatenga bajeti, kwamba, Serikali itumie fedha hii katika kuhakikisha kwamba huduma ya maji tunaisambaza. Naungana mkono na Wabunge wengine ambao wana mtazamo tuwe na Agency kama REA kwa ajili ya maji vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, hii itasaidia sana na tu-specify vyanzo vya mapato ambavyo vitakwenda pale kuhakikisha kwamba kama tulivyokuwa na Mfuko wa Barabara na Mfuko wa Umeme Vijijini, basi tuwe na chanzo cha fedha kwa ajili ya maji vijijini, itatusaidia sana kuweza kupiga hatua katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tena katika eneo hilo la maji, tuna mradi wa maji ya chini kule Kimbiji, Kigamboni, mradi ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia, unachimba visima 20,000. Niwaombe sana, mradi ule unasuasua mno na ni mradi muhimu sana kwa sisi wakazi wa Kigamboni ambao hatuko katika mfumo wa maji salama kwa DAWASA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba mradi ule uharakishwe na usambazaji uweze kufanyika na wanufaika wa kwanza wawe wananchi wa Kigamboni. Hatutakubali maji yale yakaondoka Kigamboni bila wananchi wa Kigamboni kuwa walengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nataka kugusia katika sekta ya afya, tuna changamoto kubwa sana. Burden of disease inazidi kuongezeka, tuna magonjwa ya kuambukizwa na sasa hivi tunaanza kuona magonjwa yasiyoambukizwa, none communicable diseases. Idadi ya wananchi wa Tanzania inaongezeka kwa kasi kubwa sana, sijui kama wachumi wetu na sisi mnakaa mnaliona hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka tunaongeza Watanzania takribani milioni moja, Watanzania hawa wanahitaji huduma za jamii, bajeti ya afya inashuka kila mwaka, sasa hivi tuko kwenye eight to nine percent. Kuna umuhimu sasa wa kuhakikisha kwamba tunakuwa na vyanzo mbadala vya kuendesha sekta ya afya na mimi ni muumini mkubwa sana wa universal coverage, wananchi wote tuwaingize katika mfumo wa bima ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika suala la UKIMWI linatufedhesha sana. Asilimia 90 ya fedha za kuendesha mradi wa UKIMWI nchini zinatoka kwa wafadhili na sasa hivi tuko katika hali ngumu kidogo, wafadhili wametuambia tuweke Matching Funds ambayo sisi hatujaweka. Mwaka jana tumepitisha Sheria ya Aids Trust Fund, ni hatua nzuri, lakini niombe sana twende mbali zaidi ku-specify, kwa sababu mwaka jana tuliweka kwamba tuwe na three hundred billion Serikali haiku-commit hiyo fedha. Kwa hiyo, niiombe sasa twende mbali, tu-identify vyanzo na tuweze kuwa na fedha za kuendesha Mfuko wa UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, nashukuru sana na naipongeza Serikali kwa uwasilishaji mzuri. (Makofi)