Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka 53 iliyopita (1962) ambapo ilikuwa ni mwaka mmoja tu baada ya Uhuru, Mwalimu Nyerere aliwaambia Watanganyika kuwa we must run while they walk, kwamba kama Taifa ni lazima tukimbie wakati wao wanatembea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaelekea katika mfumo wa viwanda ili kuwezesha Watanzania kuweza kuwa na uchumi wa kati, ni vyema kama Taifa tukajitathmini upya. Hatuwezi kufikia uchumi wa viwanda kama tutaacha nyuma sekta shirikishi, mfano sekta za miundombinu na kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kuwa viwanda vinategemea uwepo wa miundombinu kama barabara na reli ili kuweza kusafirisha malighafi kutoka shambani kwenda viwandani, vilevile kusafirisha bidhaa toka viwandani hadi sokoni, hivyo ni vyema kama Serikali ikazitupia jicho pia sekta wezeshi hizi ili kuwezesha viwanda vyetu kuwa na malighafi za kutosha kwa ajili ya uzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema pia kama Taifa tuondoe kauli mbaya kuwa tunazalisha tusichokitumia na tunatumia tusichokizalisha. Tuungane kwa pamoja kumpa nguvu Mheshimiwa Rais katika kujenga uchumi unaozingatia mahitaji ya nchi na soko kwa ujumla, nchi ya viwanda vitakavyoongeza thamani ya mavuno kwa mkulima. Kujenga Taifa ambalo mkulima wa kahawa atanufaika kuliko mnunuzi wa kahawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kuwa Mkoa wa Songwe ni mkoa mpya hivyo kukabiliwa sana na changamoto ya kiuchumi, naishauri Serikali tunapoelekea uchumi wa viwanda ni vyema Serikali isiiache nyuma mikoa mipya kama ya Songwe, Njombe na Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali ya kusikitisha, Mkoa wa Songwe hauna kiwanda chochote kikubwa ilhali Mkoa wa Songwe ni maarufu kwa kuzalisha mahindi na kahawa. Hivyo naiomba Serikali itujengee kiwanda kikubwa cha kukoboa mahindi ili kuweza kuzalisha unga ambao utauzwa ndani na nje ya nchi, sambamba na kiwanda cha kahawa ili kuwezesha wananchi wa Mkoa wa Songwe kunufaika pia na mpango huu madhubuti wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati.