Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ili nichangie katika Wizara ya Ujenzi. Kwa ukweli kabisa kwa dhati ya moyo wangu japokuwa nina mgogoro kidogo na barabara yangu kubwa kule iliyopelekea mpaka nikaa kwenye matope, lakini nimshukuru Mheshimiwa Waziri Injinia Chamuriho, mwezi Januari mapema kabisa alitenga muda wake, akaenda jimboni kwangu kwa dhati ya moyo, namshukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru pia Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Kaka Emmanuel Tutuba kwa kweli kuna vitu ambavyo vilikwama kuhusu barabara yetu ya Ifakara - Kidatu na juzi nilikuwa kule site amezungumza na yule mkandarasi, kwa hiyo naona dalili njema. Kwa kweli kwa dhati nimpongeze sana Katibu Mkuu huyu, nina imani atatusaidia kutatua changamoto za barabara yetu ya msingi sana kutoka Ifakara kwenda Kidatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua mgogoro huu Waziri wangu wa Ujenzi anafahamu fika kwamba barabara hii ni miongoni mwa barabara ambazo zimesainiwa na Wizara ya Fedha. Najua watu wangu wa ujenzi inawezekana kwenye mioyo yao hawajaridhika sana kwamba barabara hii imekuwajekuwaje Wizara ya Fedha wakasaini mikataba na wakati utaalam uko kwenye Wizara ya Ujenzi. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na wataalam wake na watu wa TANROAD wa Mkoa wanafanya kazi nzuri, wanafanya vizuri, watusaidie kuendelea kuifuatilia barabara ya Ifakara - Kidatu kwa sababu ndio barabara ya ajenda yetu kubwa ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikaa chini kwenye matope kwa sababu nilikaa na wananchi kuanzia saa tano usiku barabara ilikuwa haipitiki mpaka saa tano asubuhi. Ukiniuruhusu hata hapa Bungeni nitakaa endapo Waziri kwenye majumuisho yake ataniambia kwamba barabara hii
itakamilika kwa kiwango cha lami kama Naibu Waziri alivyowahi kujibu Bungeni hapa kwamba Oktoba safari hii itakamilika, ijapokuwa ni muda mfupi sana. Kwa hiyo ukiniruhusu nitakaa hata hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kusisitiza nikae?

NAIBU SPIKA: Hapana hapana Mheshimiwa.

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, huo ni msisitizo kwamba barabara hii tangu 2017 mpaka sasa hivi ni mvutano…

NAIBU SPIKA: Tutaweka utaratibu mzuri, usiwe na wasiwasi wale wanaotaka kumwonyesha Mheshimiwa Waziri kwa vitendo; kuna mzee wa sarakasi, kuna wewe unataka kukaa, kuna Mheshimiwa anataka kugalagala, tutafanya hilo jambo nje pale, tutaweka utaratibu. (Makofi/Kicheko)

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba dakika zangu zilindwe, kwa sababu dakika tano ni chache, ili nisishike shilingi na naomba uniweke kwenye orodha ya watu watakaoshika shilingi. Mgogoro huu tumeujadili wilayani, tumeujadili mkoani kwenye kikao mpaka cha RCC na Wabunge wa Mkoa wa Morogoro na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, ikaonekana kwamba mjenzi contractor na consultant wana mvutano mkubwa kuhusu barabara hii na unachangia kuchelewesha barabara hii. Sababu gani? Kuna nje ya nchi huko, walipata tenda pamoja wakagombana na wamekuja site wanagombana. Sasa tukashauriana, mmoja yule hasa consultant anatakiwa aondoke apishe ili kutafuta mtu mwingine wa kusimamia barabara ile ili iweze kwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefuatilia, inaonekana consultant kuna mkubwa huyo anamtetea na sitaki kumtaja jina lake hapa, lakini Mheshimiwa Waziri tumezungumza naye jambo hili na ameniahidi kwamba bado muda mfupi huyo consultant amalize mkataba ili twende vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakupa mfano, kwa mfano barua ambayo mkandarasi ameandika kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ambaye ameifanyika kazi kwa kiwango cha asilimia 90. Anasema kuchelewa kwa GN na Exemption ndani ya miezi 40 wamepata GN mara tisa, barabara hii haiwezi kukamilika na barabara hii ina mgogoro mkubwa sana na imeahidiwa na viongozi wa chama akiwepo Spika alipokuja jimboni kwetu kuomba kura. Sasa hili tusishikiane shilingi nataka majibu ya huyu consultant anaondoka lini? (Makofi)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, amefanya kazi miezi mitano. Nilindie dakika zangu.

NAIBU SPIKA: Kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Godwin Kunambi.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika nampa taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na mambo mengine, kilichofanya mradi huu uchelewe kwa muda mrefu ni kitendo cha Wizara ya Fedha kusaini mkataba na ikashindwa kujiombea exemption kitu ambacho kwa mujibu wa sheria hakiwezekani. Ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Abubakari Asenga, unaipokea taarifa hiyo

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa murua, taarifa bora kabisa. Kama nilivyosema nimewaomba watu wa Wizara ya Ujenzi waridhike kwenye mioyo yao japokuwa barabara hii ilisainiwa na Wizara nyingine na nina imani chini ya Katibu Mkuu mambo mengi yataenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine, ndani ya miezi mitano consultant amemwongezea contractor makalavati karibu kumi na tano, anazidi kutengeneza ucheleweshaji. Kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Injinia Chamuriho, anisaidie, alibebe hili, awashauri watu wa Wizara ya Fedha, awashauri kwa sababu Waziri ni mtaalam, ameingia kwenye mikataba na ujenzi wa reli ya kisasa, viwanja vya ndege, kununua ndege, hii kilometa 66.9 itamshindaje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwenye barabara hii, namwomba Mheshimiwa Waziri, angalau kule kijijini kwetu kila tarafa ina vituo vile vikubwa ambavyo vinafanywa kama masoko, watakavyoendelea na dizaini na marekebisho, watusaidie kuweka vile vituo na taa angalau za barabarani ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu wanakuja barabarani kuja kuuza ndizi, kuuza karanga kwa hiyo barabara hiyo ikidizainiwa ikawa na maeneo makubwa ya vituo itatusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii katikati ina kituo kinaitwa Mang’ula Kona. Hii Mang’ula Kona ni kona hatari sana pale ajali zinatokea mara kwa mara. Kwa sababu gani kuna kona? Ni kwa sababu kuna mita 50 kwa 100 za eneo la TANAPA zimeingia barabarani. Nimemwomba Waziri wa Maliasili na Utalii ameniambia anaweza kutusaidia, tunaomba atusaidie Injinia achonge apanyoshe pale ili kuondoka ile kona ambayo imeitwa kona, kona na inasababisha ajali za mara kwa mara. Kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Waziri anisaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kugusia kuhusu Kiwanja cha Ndege cha Ifakara. Kuna Kiwanja cha Ndege, ndege zinatua kwenye kiwanja kile cha vumbi, Mji wa Ifakara una mzunguko mkubwa wa pesa, wafanyabiashara wale wanaambiwa zikija ndege mara kwa mara, kwa mfano laki moja, laki mbili, waende Dar es Salaam watapanda, wataenda na mji wetu utaendelea kuboreka sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)