Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi. Naomba nianze kwa kumshukuru Mungu. Hatimaye nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa uwasilishaji wake mzuri ambao umegusa sehemu nyingi katika eneo lake la Wizara yake, vile vile nawapongeza wataalam kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijikite katika mambo machache sana, kwanza kuhusiana na suala zima la barabara. Kama mnavyofahamu na mnavyojua barabara ya kuelekea kusini inaanzia Kilwa inaishia Mtwara lakini katikati hapa kuna sehemu inaitwa Mingoyo. Hii barabara ni barabara ya Taifa na hii barabara iko chini ya TANROAD, lakini barabara hii sidhani kama kuna barabara inayofanana nayo katika nchi hii kwa upungufu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa mvua barabara hii imeharibika sana tena sana. Ninachoomba na ninachoshauri pamoja na kwamba Mheshimiwa Dkt. Pombe Joseph Magufuli, Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema, alipokuja kwenye mbio za kuzima mwenge kitaifa ilifanyika kule, alisimama pale njiani na akatoa order na ile order ilitekelezwa kwa kile kipande. Tunashukuru imemalizika, lakini sehemu kubwa barabara hii sio nzuri na wala sio salama na inapitiwa na magari mengi na mazito.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, katika bajeti haipo, sikuiona sehemu yoyote barabara hii. Lindi - Dar es Salaam ni sawa na sehemu nyingine yoyote katika Taifa hili la Tanzania. Naomba waiwekee bajeti ili barabara hii nayo itengenezwe, maeneo mengi ya barabara hii ni mabovu. Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ninalotaka niliombe kwa ujumla wake naongelea Jimbo la Mchinga ambalo ndio Jimbo langu. Katika jimbo hili kuna sehemu inaitwa Mchinga A na Mchinga B au Mchinga I na Mchinga II. Pale kuna wanafunzi wanaotoka Mchinga I kuelekea Mchinga II, wanafunzi wale wanapata adha kubwa ya kuvuka kwa miguu na yale maji ni mengi, pale kuna mkondo wa bahari maji yale ni mengi sana. Watoto wengi na watu wazima wamepoteza maisha yao kwenye eneo lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona kwenye ujenzi wa madaraja pamoja na ujenzi wa maboti na kuwapatia watu maboti, kwenye eneo hilo naamini tutapata usafiri kwa ajili ya kuwanusuru wanafunzi wale ili wasiweze kufa wakati wanavuka pale kwenda Mchinga II kutafuta elimu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini elimu ni haki ya msingi kwa kila mtu, nilisema Jimbo la Mchinga ni Jimbo pekee ambalo halina barabara ya lami hata kidogo, wengine wanasema tuna nusu kilomita, wengine kilometa moja, wengine sijui kilometa 10, lakini Mchinga hakuna, labda lami utaiona pale sehemu inayoitwa Rutamba kuelekea Rondo na ile nafikiri ni private haikuwekwa na Serikali

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba hili Jimbo la Mchinga nalo wale watu wanataka waione hiyo lami sasa lini watatuwekea hiyo lami. Naomba tufanye hima hata kidogo tupate, Jimbo la Mchinga ni Jimbo gumu, Jimbo la Mchinga linataka lifunguliwe, Jimbo la Mchinga linazalisha mazao mengi ya chakula na biashara, korosho zinatoka Mchinga, ufuta unatoka Mchinga, tuna kila sababu ya kuiangalia Mchinga kwa jicho la aina yake.

Mheshimiwa Naibuu Spika, nilisema nitasema machache tu, baada ya kusema hayo, nimalizie kwa kusema, naomba Waziri atakapokuja kufanya majumuisho, basi mtupatie angalau majibu ya matumaini kwa Jimbo letu la Mchinga na Wanamchinga.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana na nawatakia Wizara kila la heri. (Makofi)