Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwanza kukushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hii bajeti ya Wizara ya Miundombinu. Kusema ukweli bajeti tumeiona, kwangu mimi leo ninachoweza kusema ni masikitiko yangu. Ni masikitiko yangu kwa maana kwamba, yako mambo ambayo yanazungumzwa ambayo tunataraji kwamba ndani ya muda mfupi yanapaswa yapate utekelezaji. Kwa bahati mbaya sana kuna baadhi ya mambo ambayo naamini kwamba watendaji wetu aidha wanayapuuza au basi tu wanayawekwa kwa muda ambao hata haukustahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Musoma Mjini tuna tatizo la uwanja wa ndege na tatizo hili ni la muda mrefu kwa sababu ule uwanja wetu ni wa vumbi na sasa hivi hakuna ndege ya abiria ambayo inatua pale. Sasa kinachonisikisha ni kwamba katika awamu iliyopita kwa maana ya marehemu John Pombe Magufuli aliahidi kwamba tutajenga uwanja wa ndege. Kwa hiyo nikashukuru kwamba ndani ya muda mfupi, mpaka fedha za fidia zikaja shilingi bilioni 4.2.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kusikitisha ni kwamba, fedha hizo zimekuja toka mwaka jana, lakini mpaka leo yaani zililipwa tu fedha kidogo kama bilioni mbili hivi na kitu, watu wengine walitathminiwa gharama za fidia, lakini mpaka leo ni zaidi ya mwaka hawajapata fidia, fedha zile 4.2 bilioni ziko kwenye akaunti pale Musoma. Sasa unajiuliza kwanza Sheria yenyewe ya Fidia inasema baada ya miezi sita inatakiwa ifanyike evaluation mpya. Sasa wale watu wameendelea kukaa pale hawajalipwa, wamelipwa watu kiasi na fedha zipo, sasa tafsiri yake ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachonipa mashaka kabisa ni kwamba, leo Waziri huyu ndiye aliyekuwa Katibu Mkuu wakati huo. Kwa maneno mengine nasema yeye ndiye ametoa zile fedha, leo tena amekuja, bahati nzuri amekuwa Waziri, kwa nini hawa watu wasilipwe ili wakaendelee na maisha yao kuliko kuwaacha wakaendelea kupata adha ambayo watu hawa wanaendelea kuipata hadi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo yake ni kwamba, siku watakuwa tayari kulipa fidia, maana yake kwamba miezi sita imeisha na kwa kuwa miezi sita imeisha evaluation mpya inapaswa ikafanyike na zile nyumba kwa sababu watu walishahama wanasubiri walipwe fidia zitakuwa zimeanguka, kwa hiyo labda huyo mtu badala ya kulipwa milioni 100 au milioni 200, sasa atalazimika kulipa milioni 50 au chini ya hapo. Kwa hiyo na hilo ningependa Mheshimiwa Waziri aweze kulitolea ufafanuzi, ni lini hao watu watalipwa fedha yao mara moja ili maisha yao yaendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo vilevile linanifanya nishindwe kufahamu, kama tulisikia ripoti ya CAG japokuwa labda muda wake bado wa kuizungumza, kati ya jambo alilolisema ni kwamba Shirika la Ndege ni shirika ambalo limefanya vibaya katika kipindi sasa cha miaka mitano. Sasa nimejiuliza, nimejaribu kusikiliza katika hotuba ya Waziri yote na kuipitia, hakuna mahali ambapo pameonesha kwamba ni hatua gani ambazo Wizara imechukua kwa ajili ya kulinusuru shirika lile la ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa haraka haraka nilichokifahamu ni kwamba, aidha basi yawezekana habari hiyo labda haikuwa sahihi na kama ilikuwa sahihi, mbona basi suala hilo Wizara haijazungumza chochote katika kulinusuru hilo Shirika la Ndege. Naenda mbali zaidi naanza kujenga mashaka yawezekana kuna habari zingine za upotoshwaji ambazo labda wakitueleza vizuri tunaweza kuelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, naunga mkono hoja lakini nasubiri majibu sahihi kuhusu fidia ya watu wa Musoma. (Makofi)