Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nijitahidi kuwa very honest. Nawashukuru sana wenzetu wa Wizara ya Ujenzi kwa maana ya Wizara ya Uchukuzi na TANROADS kupitia Engineer Mfugale na Meneja wetu pale wa Mkoa wa Arusha, Eng. Kalupale, wanafanya kazi kubwa na kazi nzuri sana hasa kwenye Jimbo letu la Arusha mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utakumbuka kwamba, Jimbo la Arusha Mjini tulipata bahati ya kuwa na barabara ya mzunguko ile ya Arusha bypass, tunaiita ya kilometa 42.4, lakini pia tulipata barabara ya Sakina - Tengeru ya Kilometa 14.1. Barabara hizi ni nzuri sana kwa sababu kupitia barabara hizi kwa mara ya kwanza ndiyo tumeweza kuwa na barabara za njia nne katika Mji wa Kimataifa wa Arusha.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto iliyokuwepo, tunajua phase ya kwanza mmejenga barabara lakini mmetoa baadhi ya matoleo ambayo yanachukua maji kutoka Wilaya ya Arumeru yanawapeleka kwa wananchi, kiasi ambacho barabara kila mwaka zinaharibika. Ombi langu ni kwamba, kwa sababu tunayo mito kwenye maeneo hayo; tuna Mto Nduruma, Mto Ngarenaro, Mto Balaa na Mto Naura, tulikuwa tunaomba sasa phase inayofuata, waisaidie TANROADS kuyazuia yale maji na kuyaelekeza kwenye mito ili yasiweze kuharibu barabara za kawaida na kuwapa changamoto kubwa zaidi wenzao wa TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ambazo zinaathirika sana na changamoto hii, tuna Kata 12; Kata ya Sakina, Kata ya Sekei, Kata ya Balaa, Kata ya Levolesi, Kata Kaloleni, Kata ya Ngarenaro, Kata ya Kimandolu, Mushono, Ololien, Sombetini, Osunyai na Unga Limited; karibu nusu ya kata zote za Jiji la Arusha. Ni imani yangu kwamba TANROADS kupitia ujenzi wa barabara mpya ile ya kutoka Arusha Airport na ile barabara ya Arusha Kisongo ambayo na yenyewe ni ya njia nne, watakwenda kujenga mitaro ambayo itaweza kuya- tap yale maji na kuyapeleka kwenye mito ili wananchi wa Kata ya Sombetini Osunyai na Unga Limited wasipate hivyo changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kwenye uwanja wetu wa ndege wa Arusha Airport, pale TANROADS na kushirikiana na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, wamefanya kazi kubwa na nzuri sana. Kuna barabara pale za kisasa zimejengwa na mazingira yamekuwa ni mazuri sana. Changamoto kubwa tuliyokuwa nayo sasa hivi ni changamoto ambayo inahusiana na majengo yaliyoko pale; majengo kama ya abiria wale wanaoingia na wanaotoka, restaurant za kisasa, maeneo ya kununua zawadi mbalimbali ili yafanane na mandhari ya Mji wa Arusha na masuala yaweze kuwa vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni Imani yangu kuwa Mheshimiwa Waziri na timu yake watakwenda kwenye phase II kutuwekea utaratibu mzuri zaidi ili maeneo yale yaweze kuwa mazuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la tatu, pale tunao madereva taxi, madereva taxi wale kwao hii ni fursa, wamekuwa pale kwa muda mrefu, wengine wako toka mwaka 1998, lakini ukiangalia lakini ukiangalia sasa hivi wenzetu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wamekuja na utaratibu wa kusema wanataka kuongeza mapato eti wanataka watangaze tenda ili wawapate watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani badala ya kutangaza tenda wangekaa na wale ambao walikuwa pale kwa muda mrefu kwa sababu ile kwao ni fursa na ni ajira pia ili mwisho wa siku waweze kuangalia utaratibu mzuri zaidi wa kuweka mazingira mazuri zaidi ili walewale waliokuwepo waweze kuendelea. Vinginevyo watakuja watu wengine ambao wana uwezo zaidi, watatenda kwa juu zaidi halafu wale watu ambao wako kwa muda mrefu na ni watu ambao ni wanyonge watakosa hiyo fursa. Ni imani yangu kuwa Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake watakwenda kulipa jambo hili kipaumbele ili Watanzania wanaopata riziki zao pale waweze kuwepo na waweze kunufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la nne ni kwamba tuna barabara yetu ya Tipekazi - Losinyai ambayo yenyewe imewekwa kwenye mzunguko ule wa kawaida wa barabara ya Arusha – Kibaya - Kongwa ambayo ni ya kilometa 430. Ile barabara ni kubwa sana inawezekana ujenzi wake ukawa ni wa muda mrefu.

Mheshimiwa NaibU Spika, tuna ombi maalum, tunaomba pale kwenye Kata ya Mwishono kuna kipande kidogo sana kilometa ambazo hazizidi saba kutoka kona ya Kiseriani mpaka kwenda kwenye eneo la By pass ambapo barabara hiyo ikijengwa itatusaidia kuondoa msongamano katika Jiji la Arusha lakini pia na watalii wakiingia mjini watakuwa na route nyingi zaidi za kutuletea dola katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu pia tunayo changamoto ya corona katika nchi yetu. Ni imani yangu wale wafanyakazi sasa wa Mamlaka za Viwanja vya Ndege mara baada ya ripoti ya jana, ya timu ambayo imeundwa na Mheshimiwa Rais wataanza kuvaa sasa zile barakoa na vifaa vingine vyote ambavyo vitairejesha dunia kwamba Tanzania tuko makini na jambo hilo, ili watalii waje wengi zaidi tuendelee kupata dola na miradi hii ambayo tunaililia leo hapa iweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)