Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Eng. Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunisimamia na kuniongoza mpaka kufikia hapa nilipo. Naomba kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayofanya katika ujenzi wa miundombinu ya nchi yetu na kipekee kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri wa Makadirio ya Bajeti ya Mwaka wa Fedha unaokuja wa 2021/ 2022. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia suala nzima la ndege. Serikali imefanya kazi nzuri ambayo siyo ya kubezwa kwa kununua ndege nane nzuri kabisa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Katika mwaka wa fedha unaokuja, tumetenga shilingi bilioni 450 kwa ajili ya kununua ndege nyingine tatu, lakini vile vile, kwa ajili ya kuboresha karakana zetu za viwanja vya ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali iweke msisitizo katika karakana zetu ndege ni karakana hii bilioni 450 iliyotengwa kwa hakika naona haitoshi kwenda kununua ndege tatu, kumalizia deni la Airbus na vilevile, kufanya karakana zetu za ndege. Naona kama ni kizungumkuti. Nafikiri ni muhimu tukaziboresha karakana zetu kwa uhakika zaidi wa kuhakikisha ndege zetu zitadumu kuliko kuongeza ndege nyingine tatu hali ya kuwa karakana zetu zinahitaji maboresho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuishauri Serikali iliangalie jambo hili kwa kina. Ndege ni karakana, tusipofanya hivi shirika letu la ndege litakuja kurudi nyuma kama huko nyuma tulipotoka; na mzimu wa Marehemu utatuandama kama hatutatengeneza karakana za ndege Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia pia na kuhusiana na kiwanda cha ndege cha Tanga. Kule tunafahamu kuna mgogoro na umewekwa katika bajeti. Naomba Serikali ikamalize mgogoro ule ili kuweza kujenga kiwanja cha ndege cha Tanga. Ni tangu Mheshimiwa Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli wakati anazindua mradi wa bomba la mafuta, aliahidi kiwanja cha ndege kule kujengwa lakini mpaka leo tunakwenda kusaini mkataba wa bomba la mafuta, kiwanja cha ndege cha Tanga bado hakijajengwa. Serikali iweke commitment kuhusiana na jambo hili. Ni fedheha kama wataalamu watakaokuja kejenga bomba la mafuta watatokea Kenya wakati Tanga tuna kiwanja cha ndege. Tunahitaji kiwanja cha ndege hicho kiingizwe katika commitment ya Serikali na kijengwe haraka iwezekanavyo. Ni miaka minne sasa imepita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia kuhusiana na bandari. Niliwahi kusema jamani, tunafanya miradi mikubwa sana ya upanuzi wa bandari zetu, lakini tunahitaji tafiti na wataalam wa kujua kwa nini kina cha bandari zetu zinapungua? Bila tafiti tutaendelea kutumia mabilioni ya pesa kuongeza kina cha bandari zetu, lakini mwisho wa siku tunapiga mark time; leo tutafanya capital dragging, baadaye tutafanya maintenance dragging lakini hatujui sababu kwa nini kina cha bahari kina pungua? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Western California Beach ya Marekani iliwahi ku-sediment, yaani kina kupungua; na sababu kuu ilikuwa ni ujenzi wa mabwawa ya maji ya umeme. Sasa tuangalie mahusiano ya mito yetu na bahari zetu ambapo tunajenga au tunapanua hizi bandari zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inasemwa kwa mujibu wa port and coastal engineering, mto hata ukiwa na kilomita 150 unaweza kuleta madhara katika bandari iliyoko huku. Kwa hiyo, bila tafiti pia hatuwezi kusema kwamba huu utaratibu wa kuongeza kina kwa maana hii ya dragging ni wa faida kiasi gani kwa Taifa letu? Kwa sababu siyo njia pekee ya ku-control sedimentation, zipo njia nyingine. Je, tunafanyaje cost comparison analysis kama hatuna tafiti za kujua vyanzo vingine vinavyosababisha sedimentation na njia ya ku-control? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala nzima la Bandari ya Tanga kuhusu ufanisi wake…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)


MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, samahani naomba nimalizie…

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagongwa Mheshimiwa. (Makofi)

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kidogo aah.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa, muda wangu umebana sana. Kwa hiyo,…

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja, nashukuru. (Makofi)