Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Assa Nelson Makanika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kufunga dimba la leo. kKabla ya yote nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wameweza kutupa salamu za pongezi kwa ushindi tulioupata wa kishindo kwa majimbo mawili ya Mkoani Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunajadili Wizara hii ya Ujenzi ambayo ni Wizara muhimu sana katika nchi yetu ya Tanzania na Wizara hii inamgusa kila Mtanzania na inagusa maisha ya kila masikini wa nchi hii. Miundombinu ndio uti wa mgongo wa nchi hii na ni moyo hasa, kulingana na rejea ya hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Rais wa nchi hii tarehe 22 Aprili, 2021. Lakini ukiangalia bado kuna changamoto nyingi sana, na changamoto hizi zinazopatikana kutokana na Wizara hii, kwa kweli zinaonyesha kabisa kwenye hali ya uchumi wa nchi hii bado kuna shida kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi wa kwanza tarehe 8 Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje bwana Wang’ alitembelea nchi yetu ya Tanzania. Alizungumza kauli moja sana na kauli ile Wachina wengi sana wanaipenda na waliitumia kipindi wako kwenye taratibu za kukomboa nchi yao kiuchumi. Alisema ukitaka kumkomboa mtu mnyonge wa nchi yoyote ile mpelekee muundombinu kwa sababu, mkulima yeyote akilima anataka aweze ku-exchange mazao yake na pesa. Anaweza kufanyaje hivyo ni lazima awe na muundombinu wa kupeleka zao lile alilolima sokoni, atawezaje kama muundombinu hauridhishi au haumfikishi sokoni? Matokeo yake muundombinu ukiwa uko hohehahe hawezi kutoka kwenye hali aliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, niiombe Wizara hii iweze kuweka mpango wake madhubuti. Ukiangalia mfumo wa kibajeti tulionao, ni tofauti kidogo na mifumo ya nchi zingine kama nchi za Marekani. Nchi za Marekani wanatumia federal reserve lakini sisi tunatumia basket fund, ambapo


masikini wa Kigoma analima shamba lake anatoa kodi ambayo kodi hiyo isiporudi kumpelekea muundombinu, inakwenda kujenga muundombinu wa mkoa mwingine. Na hii inatokea endapo tunakuwa hatujaweka mgawanyo sawa wa rasilimali hii ambayo ndio keki ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa Wizara kwa kupitia mfumo huu wa kibajeti tulionao, iweze kuangalia namna ambavyo inagawanya haka ka keki kadogo. Kwa sababu inaweza ikachukua pesa kutoka sehemu nyingine ikaenda kuwahudumia watu wengine. Huenda hata hayo ma-fly over tunayoyasema huenda na kodi pia ya mtu wa Kigoma amejenga yeye kila siku anapitia kwenye matope haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu wa kijijini ameenda kujenga miji yeye bado yuko kwenye hali ya chini, na hii inatokana kulingana na mgawanyo mdogo ambao hauna usawa hata kidogo haumrudii mtu wa kijijini katika kujiletea maendeleo. Nitoe mfano mdogo tu, huku Kigoma kwetu mpaka dakika ya sasa mkoa wetu mnafahamu bado haujaunganishwa na mikoa mingine kwa lami. Sehemu kubwa sana ukiangalia njia ya Kaliua hii mpaka kuja Tabora bado kuna zaidi ya kilometa 90 na kitu hazijaunganishwa kwa lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija njia hii ya Kasulu bado haijaunganishwa kwa lami. Pamoja na kwamba tunashukuru ndio mkandarasi yupo, tuombe sana Serikali iendelee kuongeza nguvu sana, ili na mkoa wetu na mikoa jirani hii iweze kuunganishwa kwa lami. Lakini, imekuwa ni jambo la kusikitisha sana juzi nimesikitika sana, Mbunge wa Kakonko anaomba kilometa 3 za lami ndani ya mji tena ndio mjini. Lakini wapo Wabunge ambao wanaomba zaidi ya kilometa 15 tena pembezoni mwa mji, hii sio sawa na Wizara isikie. Hiki tunachokifanya ni kitu ambacho tunafanya tuamshe hisia za watanzania wengine, huku tunakwenda kuwanufaisha watanzania wengine na huku wengine, wataamsha hisia za hasira na tunaweza tukafika mahala ambapo sio pazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niiombe Wizara iweze kugawa sungura huyu kwa kuangalia uwiano sahihi kabisa, ili watanzania wote waweze kuona ya kwamba na waji-feel proud ya kwamba ni sehemu ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, itakupa mifano michache tu pale kwetu Kigoma, kuna baadhi ya wananchi mpaka sasa toka tunaupata uhuru hawajawahi kuona gari! Toka uhuru ukienda Kata ya Kagunga, ukienda Kata ya Mwamgongo, ukija na Kata ya Ziwani zaidi ya wananchi 70,000 gari haifiki. Barabara yetu ya kuanzia Mwandiga kupita mpaka Chankere kwenda mpaka Mwamgongo na kufika mpaka bandari ya Kagunga haijawahi toboka mpaka dakika ya sasa! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kwenda kuwatembelea wananchi wetu hawa lazima upite nchi jirani ya Burundi. Mheshimiwa Waziri alikuja Kigoma, ameshindwa kufika kuwatembelea wananchi wetu na hiyo yote ni kwa kuwa hakuna barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara iweze kuangalia iwezekanavyo iwapelekee wananchi na hawa wajione ni sehemu ya nchi hii. Waweze kuona ya kwamba na wao wanachangia kuijenga nchi ambayo na wao wanapata haki sawa. Ukiangalia bajeti nilikuwa napitia na nimepitia nikiwa safarini natokea Kigoma, wametengewa ile barabara milioni 200 barabara ambayo inahitaji zaidi ya bilioni 23. Unakwenda kutenga milioni 200 itatoboka lini? Itamalizika lini hii barabara? Na hii barabara iko kwenye Ilani ukurasa wa 74 wa Ilani ya Chama chetu Cha Mapinduzi, umeisema hii barabara kilometa 60 lakini ukiangalia pesa zinazotengwa zinasikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, niiombe Wizara nitakuwa na machache sana na msingi wangu ni kwenye hii barabara. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, shida umeiona, utakapokuja ku-wind up hapa uje utuambie ya kwamba ni lini wananchi hawa watakuja kupata uhuru kama wananchi wa sehemu zingine? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema machache hayo naomba kuunga hoja mkono, lakini Waziri utuambie ya kwamba barabara hii ya kutokea Mwandiga mpaka kwenda bandari ya Kagunga ambapo Serikali imewekeza mabilioni ya pesa kwenye bandari ile ya Kagunga. Lakini hayana manufaa yoyote, ili yaweze kuwa na manufaa na bandari ile ifanye vizuri lazima tupate muunganiko wa barabara hii ya Kagunga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho kabisa kuna barabara ya Mwandiga – Manyovu imeanza ujenzi mwaka 2008. Barabara ile imejengwa lakini kuna wahanga wa barabara ile ambao walibomolewa majumba yao walipoteza na baadhi ya maeneo yao. Hawajalipwa fidia mpaka sasa, nikuombe Waziri ikiwezekana uweze kufika uzungumze nao, imekuwa ni muda mrefu hawajalipwa fidia za nyumba zao zilizobomolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya machache hayo niweze kuunga hoja mkono, nakushukuru sana. (Makofi)