Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami nitumie nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niongelee tu kwa ujumla sekta hii ya usafirishaji, kwanza sifa zake mahususi kiulimwengu ili sekta hii ionekane iwe bora. Sifa ya kwanza, ni lazima kuwe na mifumo mizuri iliyotengenezwa ya usafirishaji kwenye miji au tunasema well designed inter-city systems. Sifa nyingine ni ku-avoid unnecessary traffic flows au tunasema ni kuepuka ile misongamano isiyokuwa ya muhimu.


Mheshimiwa Naibu Spika, sifa nyingine ni kuhakikisha kwamba mifumo ya usafirishaji inapunguza gharama. Sifa nyingine ni kuhakikisha mifumo ya usafirishaji wetu inakuwa salama na ya uhakika. Nyingine ni kuhakikisha kwamba tunaweka mifumo mizuri ya usimamizi ya miundombinu yetu ya usafirishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichangie pale kwenye kuweka mifumo mizuri ya usafirishaji kwenye miji yetu. Ndugu zetu hawa wa Wizara ya Ujenzi wao ni wataalam na bahati nzuri sana Waziri tuliyenaye alikuwa Katibu wa Wizara hii. Napenda kushauri jambo moja kwenye Wizara hii. Kwanza, kuangalia mifumo ya usafirishaji kwenye miji yetu. Ipo miji imekuwa sasa kama ni vigogo vya usafirishaji kwenye mazao yanayotoka kwenye mikoa mbalimbali na yanayotoka kwenye vijiji vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, umeongea kuhusu Mji wa Mbeya asubuhi, lakini mimi nitaongea kuhusu Mji wa Iringa pia. Miji ile inapita au ipo katikati ambapo barabara kubwa zinapita katikati ya ile miji. Tunafahamu katikati ya miji mikubwa kama ile, kuna shughuli nyingi za kibinadamu zinafanyika. Sasa wenzetu hawa ni wataalam, walipokuwa wanajenga miundombinu ya barabara hizi, wakifungua mikoa mingine walijua kabisa geti kubwa litakuja kuwa ni Iringa; walijua barabara kubwa itakayosafirisha magari makubwa yote kutoka kwenye mikoa sita inayotegemewa kulisha nchi hii kwenda kaskazini na Kanda ya Ziwa mikoa sita itapita katikati ya Mji wa Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walijua kabisa kwamba nchi zile ambazo ni landlocked countries, kwa mfano Zimbwabwe, zinapita katikati ya Jiji la Mbeya. Kwa hiyo, ilitakiwa wenzetu hawa watusaidie kutengeneza miundombinu ya kufungua yale majiji yasiwe barrier. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii viazi vinatoka Songwe vinaozea Mbeya, au vinaanza kuungua Mbeya; vikifika Iringa vinataka kupita vije Dodoma viende Mwanza, vinafia Iringa. Kwa sababu miji haipitiki. Ni sawa na umetengeneza barabara ya njia sita halafu unakwenda kuipitisha kwenye daraja la mita moja, lazima uvunje lile daraja; na ndicho kinachofanyika kwenye miji yetu. Mle kwenye miji ndiyo maana sasa kumekuwa na matatizo. Sisi Wabunge tumeongezewa kazi nyingine nje ya ilani kwenda kuanza kuzuia migomo inayotokea katikati ya vyombo vinavyopita kwenye miji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, umeongelea mgomo uliotokea Mbeya; wiki iliyopita sisi Iringa tulikuwa tuna mgomo wa watu wa barabara, bajaji na bodaboda. Sasa hivi ninavyoongea, kuna vijana wengine pia wamegoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunafahamu, nami nawaomba Waheshimiwa Wabunge, mchawi bwana mkabidhi mtoto akulelee. Mimi nafikiri sasa TARURA tuwakabidhi hawa hawa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, iwe chini yao na wawe na full mandate ya kui-control TARURA ili sasa kule kulaumiana kwamba hapa alitakiwa atengeneze TARURA, kusiwepo. Wasimamie wenyewe kuanzia juu mpaka chini ili wanapofika kwenye mji ule waweze kuwasiliana na wenzao wa TARURA waangalie ni namna gani sasa mji huu tunaufungua? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Iringa tuna bypass. Tunapoongelea miji hii mikubwa, kwa mfano pia Songea kuna bypass, Mbeya kuna bypass. Sasa hizi bypass waliziweka kabisa kitaalam, wamelipa fidia, wamefanya kila kitu, yaani kinachotakiwa ni kuzijenga. Kwa mfano, Iringa tuna kilometa 7.3, ili tuchepushe yale magari makubwa yapite pembezoni activities nyingine katikati ya mji ziendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo tunakuja kwenye ile sifa nyingine ya kupunguza unnecessary traffic flows kwenye miji. Hizo ni unnecessary, tungekuwa tumejenga zile bypass tusingekuwa na sababu ya magari kuja pale. Njegere za akina mama zinaozea kwenye barabara, viazi vya vijana wetu…

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Twaha Mpembenwe.

T A A R I F A

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimpe taarifa mzungumzaji kwamba tatizo hilo la kutoweza kuzijenga barabara kwa wakati kama mifano tunayopewa ya barabara ya kutoka Mbeya kwenda Tunduma na barabara nyingine za Iringa, barabara ya Kibiti mpaka Mloka, hii yote ni kutokana na sababu ya mambo ya utelezi. (Kicheko/Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Msambatavangu, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili. Niseme kwamba huu utelezi ndiyo tunataka utolewe. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bypass zijengwe kwenye miji yetu. Kwa nini tunasema bypass zijengwe? Kwa sababu mijini ndipo huduma za jamii zinakopatikana, watu wetu wanakwenda kupata huduma kule. Watu wanafia barabarani. Pia mijini ndiko kwenye masoko. Wewe umefikisha bidhaa mpaka stendi inashindwa kufika sokoni kwa sababu tu ya traffic jam. Sasa uangalie, huo ndiyo utelezi tunasema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, angalia Mji kama Iringa, kwanza barabara yenyewe ya Tanzam inapita iko kwenye mlima, malori makubwa yote yanakwama pale. Lori likianguka katikati pale, Iringa haipitiki kwenda chini, kwenda juu; na malori ya dagaa zilizotoka Mwanza zinaozea pale. Tunawaomba wenzetu waangalie haya, tunaomba sana watusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ninachotaka kuongea hapa, sisi tumepitisha hapa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Sasa inaonekana kama Mpango tunaoupitisha hauendani na mipango ya Wizara nyingine. Nilimsikiliza Katibu Mkuu Kiongozi wakati anaapa, alisema kazi yake ni ku-coordinate hizi Wizara. Tunaomba kupitia Bunge hili aka-coordinate mambo ili Mpango wetu wa Miaka Mitano uende sambamba na mipango ya hizi Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunataka sekta ya utalii ichangie watalii wafike milioni tano ifikapo 2025, na share kubwa tunategemea kupata kwenye utalii wa Southern Zone. Leo tumeiwekea barabara inayokwenda National Park kujenga kwa usawa wa kilometa 1.5, barabara ya kilometa 104, hivi tunapomaliza huu Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2020 - 2025 ni kweli tutakuwa tumefikisha sisi kuchangia pato hilo la Taifa, kufika dola bilioni 6.0? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine tunajiuliza hii mipango tumeweka Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano halafu bado tunaongelea kuunganisha madaraja tu hatuongelei barabara zile zinazokwenda kwenye strategic areas. Tunaongelea kilometa mbili, kilometa tano kwenda kwenye miradi ile ya kimikakati ya kutuongezea pato la Taifa. Je, tupo serious? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana ndugu zangu tuwaangalie Watanzania kwa jicho la huruma, tuwaangalie hawa vijana wetu wa bajaji, wa bodaboda waliopo mijini kwa jicho la huruma. Askari wanafanya kazi kubwa yaani mpaka wanashindwa sasa. Leo TARURA inapewa fedha ya maintenance tu, asilimia 80 mpaka 90, lakini kwa maana ya miradi ya maendeleo wanapewa asilimia 10 mpaka 20. Miji yetu inakua, Waheshimiwa Wabunge tunaposema maintenance maana yake unapewa fedha za kutunza barabara tu zilizokuwepo, hawapewi pesa ya kuongeza mtandao wa barabara. Miji yetu sisi inakua, Iringa TARURA haijapewa fedha ya miradi ya maendeleo na mji unakua wale watu kule wanafuatwa vipi. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, hizi bajaji sijui bodaboda zinafikaje kule kwenye makazi ya watu? Kama watu wanapewa fedha ya kutunza barabara ambazo hazipo, mtoto huyu akabidhiwe wenyewe, wakabidhiwe hawa Ujenzi na Uchukuzi wamchukue TARURA wakae nae ili yanapotokea matatizo tusilaumu kwamba huyu yupo TAMISEMI, tujue ni wenyewe Uchukuzi asilimia mia wamefeli hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba TARURA wapewe, nashukuru wamenipatia milioni 120 kwenye barabara yangu inayopita Kleruu, nayo inatakiwa itengenezwe kwa kiwango cha kokoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kiwango cha kokoto si kiwango. Sasa nashukuru kwa ajili ya hilo lakini niwaombe sana tujaribu ku-coordinate mpango wetu na mambo yetu tuliyoyapanga lakini tujaribu kuangalia hizi by pass kwenye majiji zifunguliwe ili huduma zingine za kiuchumi ziendelee. (Makofi)