Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii ili niweze kuchangia Wizara hii muhimu ya Ujenzi na nitajikita zaidi katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Kilolo jimbo ambalo ni pendwa sana kwa upande wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuchangia kiundani nataka nitoe tu mlinganisho wa bei za vitu unaotokana na ubovu wa miundombinu katika eneo la Kilolo. Mfano, ubao wa mbili kwa nne unaouzwa Sh.6,000 Mafinga, Kilolo utauzwa kwa Sh.3,500 na hii ni kutokana na changamoto za miundombinu ya usafirishaji. Sasa Barabara hii ya kutoka Iringa Mjini kwenda Kilolo hadi Idete ni barabara ambayo ni ahadi za Maraisi kadhaa kama zilivyo barabara nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii kwa kiasi fulani nianze kuipongeza Wizara kwa kazi ambayo tayari inafanyika. Najua kuna kilometa 10 ambazo mkandarasi yupo kazini, amekuwa taratibu kidogo, huyu mkandarasi amefanya kazi pale kwa karibu miaka mitatu, nimepita hivi karibuni nimeona sasa angalau kazi inaendelea, inatia moyo. Nafahamu pia kwamba kuna kilometa tatu nyingine za kutoka kwenye daraja pale Ndiwili kuelekea mjini ambazo zimeshapata makandarasi, nalo pia ninalipongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tutakuwa tumebakiza kama kilometa 13 hivi kufika Iringa Mjini, naomba, nimeona imetengwa shilingi 140, sijajua milioni 140 ni ya kilometa ngapi, lakini imeandikwa kwamba ni kuweka lami kwa hizo kilometa zilizobaki, basi naomba kama ambavyo barabara nyingine zina umuhimu, hii milioni 140 iongezewe ili ile barabara iweze kufika Iringa Mjini. Hiyo ndiyo wilaya peke yake kwenye Mkoa wa Iringa ambayo haijaunganishwa na barabara ya lami hadi kwenye Makao Makuu ya Mkoa. Kwa hiyo kama tutakamilisha hiyo, nitakuwa na sababu ya kupongeza na nitakuwa naunga mkono hoja zenu kwa moyo mkunjufu kwenye miaka ijayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa pia nizungumzie kuhusu hii barabara ambayo inatoka Ilula inapita Mlafu inaenda Ukwega - Kising’a - Mtitu na inakuja kutokea Kilolo ambayo uchumi wake ni mkubwa na tayari kutokana na athari za mvua barabara hii inapitika kwa shida sana. Kwanza inatakiwa ifanyiwe maintenance ya kawaida kabla haijawekwa lami, lakini mapendekezo yangu, kwa sababu barabara hii inasumbua mara nyingi kwenye maeneo kadhaa na kwa sababu tayari Meneja wa TANROADS ameshafanya ubunifu wa kukata baadhi ya milima ili barabara ile iweze kupitika kwa urahisi jambo ambalo tunapongeza. Ningependa yale maeneo ambayo yana hali ngumu zaidi yanapitika kwa shida na yale maeneo mbayo udongo wake ni shida hata ukiweka kokoto inazama yale yafikiriwe kuwekwa lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuwe na mpango wa kuweka lami katika maeneo korofi, sisi hatusemi muweke yote, sisi tunasema waweke maeneo korofi, wakitupa kilometa mbili tutachagua sehemu ya kuweka, wakitupa kilometa tatu tutachagua sehemu ya kuweka, ili mradi magari yaweze kupita kwa muda wote. Kule sasa hivi kuna watu wengi ambao ni wazawa wanaoitwa wawekezaji, wanafanya kilimo cha maparachichi na tayari wameshaanza kuuza. Njombe bei ni kubwa kule sasa hivi wanauza kilo moja ni Sh.1,000, tatizo ni miundombinu ya barabara hiyo ambayo ni barabara inayokatisha kwenye eneo kubwa sana la Jimbo la Kilolo na ni barabara ya muhimu. Naomba barabara hii itiliwe mkazo hasa kwenye maintenance na kwenye kuweka lami kwenye maeneo korofi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kujielekeza, ni kuhusu utaratibu wa kupaki magari hasa Ilula na Ruaha Mbuyuni. Sasa hivi pale Ilula kimewekwa kituo nafikiri ni cha watu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, sasa wameweka banda pembeni ya barabara na magari sasa yanapaki pale yanaziba ile barabara kabisa. Nafikiria hizi sehemu kama Ilula ambapo kunahitajika ile barabara iwe wazi, basi kama kunawekwa kituo chochote cha kiserikali kitafute namna nzuri kama ilivyofanywa mizani. badala ya kuweka stop ambazo zinazuia barabara hasa kwenye haya maeneo. Tatizo hilo linaweza likawepo hata kwenye maeneo mengine, lakini kwa uchache nitayataja hayo maeneo mawili Ilula na Ruaha Mbuyuni ambayo nimepita na kuona na kuona kwamba ile ni changamoto kubwa na ningefikiria kwamba ingeweza kufanyiwa marekebisho ili magari yaweze kupita kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa pia kutaja eneo lingine ambalo kama lingekarabatiwa vizuri lingetusaidia. Barabara hii kutoka pale Kidabaga kuna milima michache, kuna Mlima Msonza uko pale, wenyewe huko nyuma ulikuwa haupitiki kabisa, lakini baada ya ukarabati
ule mkubwa unapitika, lakini ile mifereji ile miundombinu yake kwa sababu milima ya kule inamomonyoka, Serikali inatumia fedha nyingi sana kuchimba ile milima, lakini kwa sababu hakuna namna yoyote inayowekwa ili kuzuia ile milima isimomonyoke ile milima inaendelea kumomonyoka na kuharibu tena barabara. Kwa hiyo kuna namna ya kutengeneza ile miundombinu ya mifereji ili barabara zile ziendelee kudumu kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zile sehemu zote pia hapo kwenye Mlima Msonza ukienda kama unaenda Idete kuna milima mingine kama miwili, ile nayo kwasababu ni milima ambayo ni sumbufu kwa muda mrefu na yenyewe ingeweza kufikiriwa kuwekwa lami. Tunapozungumzia lami hatuzungumzii, sisi hata ingewekwa kama hii ambayo ni ya kwenda Iringa iliyochanikachanika hata ikimwagiwa kokoto kokoto tu sisi hatuna tatizo ili mradi iweze kupitika mwaka wote. Kwa sababu sisi hatutajali sana ubora ili mradi ipitike tu mwaka mzima, nafikiri hapo hata bei itakuwa nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hizi milioni 60 walizotuwekea, milioni 140 wakiongeza tu kama milioni 300 hivi angalau tutapata kilometa saba au nane zitasaida katika yale maeneo ili wananchi waweze kupita kwa urahisi na waendelee vizuri na shughuli zao za kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili niweze kuweka mkazo kwenye hizi barabara ambazo nimezitaja labda niendelee kuweka msisisitizo zaidi kwenye kipengele cha barabara nyingine ambazo zipo katika Mkoa wa Iringa na niza kiuchumi na kwa kweli tulikubaliana katika Mkoa wa Iringa kuendelea kuzitaja hasa zinazoingia kwenye mbuga za Wanyama. Na hapa nataka nikumbushe kwamba mbuga ya wanyama ya Udzungwa ambayo kwa kiwango kikubwa iko katika Wilaya ya Kilolo asilimia 80 lango lake la kuingilia liko Morogoro ambako ni asilimia 20 tu ya mbuga ndiko iliko na hii inatokana na tatizo la miundo mbinu la barabara inayotokea pale Mahenge na kuingia Udekwa ambapo kuna geti ambalo ndiko asilimia 80 ilipo. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, na hii barabara ilishachimbwa kilomita 14 lakini haikutoboka kwa hiyo walianzia Udekwa wakachimba kilomita 14 wakaitengeneza tu vizuri kabisa lakini imebaki kilomita 7 kuingia kwenye lami. Sasa kule kunaota majani huku walikochimba kilomita 14 ni useless kwa sababu hakuna mtu anayepita kwenda asikofika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningependekeza pia kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili ambako ndiko geti liliko lile geti la Udekwa waweze kwenda kuangalia kama ilikuwa ni halali kuchimba barabara na kuacha kilomita 7 kutoboa kwenye barabara ya lami halafu unaishia hapo halafu ile barabara inakuwa yakwenda porini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa hivi wanapita tu Ngedere Tumbili na wanyama wengine waliopo kule, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)