Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi ambayo imewasilisha hotuba yake leo asubuhi. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali na Wizara kwa ujumla kwa kujenga Barabara ya Chaya - Nyahua ambayo ilikuwa ni kero kwa wakazi wa Mkoa wa Tabora, lakini nishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kuikamilisha kwa asilimia 100 ambayo ilikuwa katika Jimbo langu la Igalula, wananchi wa Igalula wanashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii imetoa fursa kwa watumia barabara hasa wa Mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mwanza badala ya kupita Igunga sasa wanapitia Jimbo la Igalula. Nitoe wito wanapopita katika Jimbo la Igalula tuna migahawa mizuri sana wakifika Tula pale kuna mama mmoja anaitwa mama Tausi, wakifika wapite pale kuna kuku wa kienyeji, anajua kuwapika vizuri. Vile vile wakipita Kizengi pale kuna mgahawa mmoja unaitwa Tula Mgahawa, basi mambo yanakuwa mazuri. Naibu Spika nawe karibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani zangu hizo nirudi, mkandarasi amemaliza ujenzi wa barabara, Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi nilikwishamwandikia barua ya kumwomba majengo yale ya Kizengi. Naomba wakimaliza na wakakabidhi mradi, basi naomba yale majengo waikabidhi halmashauri yangu ili tuweze kufanyia utaratibu mwingine hasa tuweze kupata kituo cha afya kwa sababu Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi imetuelekeza tutajenga vituo vya afya kwa kila kata. Kwa hiyo, wakinikabidhi yale majengo nitayatumia kwa ujenzi wa kituo cha afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nichangie baadhi ya mambo kidogo, pamoja na mazuri wanayoyafanya Serikali lakini bado tunachangamoto ya upatikanaji wa barabara. Kuna Kamati iliundwa ya Mapitio ya Barabara, sasa hii kamati ilivyoundwa ilikuwa inaenda kuzitambua barabara ambazo zinatekelezwa na TARURA, lakini mpaka leo kamati hii imekwishamaliza kazi, lakini hatujui hizi barabara ni lini zitaingizwa kwenye mfuko wa upatikanaji wa fedha wa barabara.


Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kwangu kuna barabara ambazo ni uchumi, ni muhimu sana katika maeneo yangu, zinaunganisha wilaya na wilaya, lakini zingine zinaunganisha mkoa na wilaya nyingine ndani ya mkoa mwingine. Kwa mfano, kuna Barabara ya Makibo – Msololo – Goweko - Kamama mpaka Nyahua. Hii barabara ina zaidi ya kilometa 80, tunapoisema barabara hii ni muhimu sana kwa sababu inatoka katika Wilaya ya Sikonge inakuja katika Wilaya ya Uyui. Tukisema itekelezwe na TARURA haiwezekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanzoni tulikuwa tumeweka utaratibu mzuri wa kuainisha hizi barabara, tunazipandisha hadhi TANROAD wanafanya utaratibu mzuri wa kuweza kuzitengeneza, lakini utaratibu ule Wizara waliukataa, wakasema hizi barabara zitekelezwe na TARURA. Leo wilaya yangu inapata bajeti ya TARURA 1.2 bilioni, ukisema utekeleze hii barabara yenye kilometa 80, tutakuwa tunawaonea TARURA. Niombe Serikali ni ile ile, TARURA ni ile ile, niombe Waziri atakapoongeza fedha kwenye Mfuko wa TARURA hata kwa emergency, basi atakuwa ameokoa wananchi wa Kata ya Jimbo la Igalula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Barabara ya Sikonge inakuja Igalula inatokea Goweko, nayo barabara ni nzuri sana kwa uchumi wa wananchi wa Sikonge na wananchi wa Jimbo la Igalula, Wilaya ya Uyui. Leo Mheshimiwa Kakunda akiwa anataka kwenda kufanya ziara kwenye kata moja inaitwa Makibo, lazima afike Tabora Mjini, baadaye arudi tena huku Makibo, ni kilometa nyingi sana anapoteza rasilimali mafuta, lakini angeweza kupita hii barabara basi angeokoa mafuta na hizo fedha zingine akaelekeza kwenye miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya barabara kila mahali ipo, lakini hizi barabara ambazo tunazozipigia kelele, Waziri anaweza kusema TARURA wanatekeleza kwa bajeti iliyopo kiuhalisia TARURA hawawezi kutekeleza bajeti hii. Nimwombe Waziri kupitia mafungu yake akipeleka TARURA fedha za dharura kule, basi wanaweza kuzifungua barabara hizi na hatimaye zikafunguka na wananchi wakaweza kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nije kwenye suala lingine ambalo ni kuhusu TRC, kwangu wananchi wanategemea sana uchumi kwa kupitia reli ya kati. Hata hivyo, tulikuwa tuna urekebishaji wa miundombinu ya reli ya kati ambayo walimtafuata mkandarasi akawa anatengeneza reli ya kutoka Manyoni kuja Tula, Malongwe ikaelekea Goweko mpaka Tabora Mjini. Sasa cha ajabu ninachokishangaa tulikuwa na miundombinu ya njia tatu katika Station ya Goweko, huyu mkandarasi badala ya kurekebisha reli akaanza kung’oa tena njia zingine, ameua njia zingine, zile reli hatujui amezipeleka wapi, sasa wananchi wa Kata ya Goweko wanauliza alikuwa anakuja kubomoa miundombinu au alikuja kurekebisha miundombinu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunategemea zile reli kwa kukuza uchumi wa wananchi wetu kwa kukata mabehewa na kupakia mizigo pale, lakini vile vile, train ikiwa inapita pale ikiweka njia mbili upishano wa train na train wananchi wetu wanapata biashara, lakini sasa leo imekuwa njia moja, train inasimama kwa dakika tano, wananchi hawafanyi biashara. Nimwombe Mheshimiwa Waziri tunataka kujua zile reli zimekwenda wapi? Wananchi wanahitaji pale reli ziwe za njia mbili train ipishane, mabehewa yakatwe, ili waweze kupata uchumi na pale sisi tunatengemea sana uchumi wa train. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, station ile pale tunategemea sana katika uchumi na abiria wapo wengi sana, lakini leo cha ajabu tangu shirika limeanza ile station hatuna choo cha abiria, abiria wakija pale wao wameshajisevia kutoka nyumbani wakifika pale hakuna huduma nyingine itakayoendelea. Kwa hiyo, tunaingiza fedha nyingi kupitia station ile, tunashindwa kujenga hata choo cha shilingi mbili na tuna kampeni nzuri ya choo bora, lakini station yetu kupitia Wizara yetu inashindwa kujenga choo. Niiombe Serikali yangu, Wizara yangu wakajenge choo pale gharama yake ni ndogo sana ili wananchi na abiria wanaowasafirisha wapate huduma nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna changamoto nyingine, Serikali imeleta umeme ambao ni Sh.27,000/=, lakini station ile imekuwa giza miaka yote na umeme upo, lakini mpaka leo tunashangaa kwa nini train zikipita usiku wananchi wanapata adha, pale kuna uwizi unaotokea wakati wananchi wanasubiri abiria iweze kuja pale, giza limekuwa kubwa Sh.27,000 mimi Mbunge wao nitalipa wakafanye wiring.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, naam, muda umekwisha, jamani!

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)