Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Dr. Pius Stephen Chaya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nachukua nafasi hii kukushukuru sana wewe, nimshukuru kipekee kabisa Waziri, Mheshimiwa Eng. Dkt. Chamuliho na vile vile nawashukuru manaibu wake wawili. Nachukua nafasi hii niwashukuru sana ndugu zangu wa TANROAD Mkoa wa Singida, wamekuwa proactive sana tunapopata matatizo sisi Wilaya ya Manyoni hususan panapotokea matatizo ya kuharibika kwa barabara. Kwa kweli hili naomba niwashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina hoja tatu ambazo zinaendana na ujenzi wa barabara, lakini vile vile nina hoja ambayo itahusiana na suala la ujenzi wa daraja na hoja nyingine ambayo nataka kuchangia inahusu Kituo cha Pamoja cha Ukaguzi wa Magari (One Stop Inspection Station) ambacho kipo katika Jimbo la Manyoni Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natoka katika Jimbo la Manyoni Mashariki. Kwanza nichukue nafasi hii nimshukuru sana Waziri, katika bajeti hii ambayo ameiwasilisha kuna daraja ambalo linajulikana kama Daraja la Sanza ambalo limekuwepo ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa miaka 10. Nafurahi na namshukuru sana Waziri kwa sababu tayari upembuzi yakinifu ulishafanyika, tayari usanifu wa kina ulishafanyika na tayari zaidi ya 90% ya wananchi walishalipwa fidia zao. Namshukuru sana Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sanjari na hilo, kwa mwaka huu wa fedha, Waziri ametutengea takribani shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hili daraja. Hoja yangu ya msingi, nataka kupata majibu haya wakati Waziri anakuja kuhitimisha kwa sababu hili daraja limekuwa likipangiwa hela kila mwaka lakini haliendi kutekelezeka. Nitapenda kusikia sasa kutoka kwa Waziri: Je, ni lini sasa huo ujenzi wa daraja utaanza? Wamejipangaje kuhakikisha kwamba wanatangaza hizo tenda ili Wakandarasi waanze hiyo kazi ya kujenga daraja? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nina barabara ambayo Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliiahidi alipokuja wakati wa kuninadi wakati wa kampeni. Barabara ya kutoka Manyoni - Heka - Sanza ambayo inaenda mpaka Chaligongo barabara inaenda mpaka Mbabala - Bihawana inatokea Dodoma. Hii barabara ina umbali wa takriban kilomita 200. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara ina umuhimu mkubwa sana. Kwanza hii barabara inagusa Halmashauri nne. Inagusa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, inagusa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, inagusa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi na Halmashauri ya mji wa Dodoma. Kwa maana nyingine, hii barabara inaunganisha mikoa miwili; Mkoa wa Singida na Mkoa wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi, hii barabara ni muhimu sana kwa ukuaji wa uchumi wa mikoa miwili hususan Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Singida. Tuna wakulima wengi sana ambao wapo katika Jimbo langu la Manyoni Mashariki, Jimbo la Bahi na Jimbo la Dodoma Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hilo tuna Game Reserve ya Kizigo ambayo ni maalum kwa Utalii wa Uwindaji. Hiki ni kitega uchumi muhimu sana ambapo kwa kweli tunahitaji kuhakikisha hii barabara tunaiimarisha, nini hoja yangu? Ni muda muafaka sasa kwa sababu Rais Hayati John Pombe Joseph Magufuli alituahidi na tayari ipo ndani ya hii bajeti, lakini haijatengewa fedha. Sasa napenda kusikika kutoka kwa Waziri ni lini tunakuja kujipanga kufanya upembuzi yakinifu (feasibility study), lakini tunakuja kuanza kupanga na kuweka bajeti kwa ajili ya detail design na vile vile, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa hii barabara angalau kwa awamu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu Wabunge wengi wameeleza kilio chao cha barabara mbalimbali, wote tunatambua hizi barabara ambazo zinaunganisha zaidi ya halmashauri mbili, lakini barabara ambazo zinaunganisha mikoa zaidi ya miwili, ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa Taifa letu. Kubwa zaidi ndugu zangu wa kutoka kwenye haya majimbo manne wanapata huduma zao nyingi za kiafya Dodoma, hususani katika hospitali ya Mkapa lakini hospitali ya Uhuru na hata Hospitali yetu ya General hapa Dodoma. Kwa hiyo, utaona ni kwa jinsi gani Serikali inahitaji ku-invest kwenye hii barabara ili tuweze kukuza uchumi wa maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni hiki Kituo cha Pamoja cha Ukaguzi wa Magari ambacho kinajulikana kama One Stop Inspection Station na kipo katika Kijiji cha Muhalala. Hiki kituo kimefikia asilimia 50 ya ujenzi wake yaani execution rate na kwa mwaka huu tumetengewa milioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa hiki kituo na tayari pale kuna magofu ya majumba zaidi ya miaka miwili yamekaa mradi ulikuwa umesimama. Hoja yangu ni nini? Kwanza nitapenda kujifunza kutoka kwa Waziri je, hii milioni 120 imewekwa kwa ajili ya vitu gani? Ningependa kupata narrative ya hii milioni 120 inaenda kukamilisha asilimia ngapi? Nasema hivi kwa sababu amesema kwamba ni asilimia 50 tu ambayo tayari tumeshakamilisha, bado asilimia 50. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ya pili ningependa kujifunza kutoka kwa Waziri vilevile, atuambie kwamba, je, anategemea huu mradi utaenda kukamilika lini? kama umekaa miaka miwili Serikali haijapeleka fedha, then mwaka huu anatuwekea milioni 120 na tayari ni asilimia 50 tu ndiyo ambayo imeshakamilika, je, hiyo milioni 120 itaenda kukamilisha hiyo asilimia 50. Kwa hiyo, ningependa kupata majibu haya kutoka kwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nirudie tena kumshukuru sana Waziri, lakini vilevile, niwashukuru sana ndugu zangu wa TANROADS Mkoa wa Singida, wamekuwa na mchango mkubwa sana. Tuna barabara yetu ya kutoka Solya kwenda Londoni kwenda Ikungi kwa muda mrefu hii barabara ilikuwa haipitiki kipindi cha masika, lakini hawa ndugu zetu wa TANROADS wa Mkoa wa Singida kwa kweli walikuwa very proactive, tulikuwa tukiwapigia simu wanakuja kutoa ushirikiano mkubwa sana kwa ajili ya kutengeneza

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hii barabara ya kutoka Manyoni kwenda Heka kwenda Sanza kipindi cha masika ilikuwa haipitiki. Hawa ndugu zetu wa TANROAD wa Singinda walitusaidia sana, tulikuwa tunawakuta wamefika site wanakuja kurekebisha. Kilio chetu kikubwa ni hii barabara ya kutoka Manyoni kwenda Heka kwenda Sanza inakuja kutoka Mbambala inakuja kuingia Dodoma, Rais Hayati Magufuli alituahidi kuweka kiwango cha lami, nitapenda kusikia kutoka kwa Waziri anawaambia nini wananchi wa Manyoni sasa hii ahadi ambayo Rais wetu mpendwa hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba niishauri Wizara, kuna ahadi nyingi sana ambazo zimetolewa na viongozi wetu wakubwa, wengi wamesema kuna ahadi kuanzia Awamu ya Tatu, ya Nne na Tano. Ningeishauri Wizara wafanye mapping ya ahadi zote, unajua hawa wenzetu wakubwa wakishaahidi wananchi wetu wanakuwa na imani kubwa sana. Hivyo, ni vizuri tukatengeneza mapping na tukatengeneza planning ya jinsi gani kila mwaka wataenda kupunguza zile ahadi. Hawa ni viongozi wakubwa, wametumikia hili Taifa, tunahitaji kuwapa heshima, lakini tukumbuke ahadi ni deni. Mbaya zaidiā€¦(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele imeshagonga.

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naomba niunge mkono hoja. (Makofi)