Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara yetu ya Ujenzi na Uchukuzi kwanza kabisa nianze kwa kusema kama sitopata haya majibu sahihi sitounga mkono hoja. La kwanza ni kuhusu barabara yangu ya Jimbo la Gairo ambayo inakwenda Jimbo la ndugu yangu Omari Kigua Kilindi. Ile barabara imekuwa na maslahi mapana kati ya Wilaya ya Kilindi, Gairo pamoja na Handeni na ni barabara nyepesi sana hata ya kutoka Dodoma kwenda Tanga, lakini ina kata nyingi sana za upande wa Gairo ziko ng’ambo ile ambayo inakaribiana na Wilaya ya Kilindi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ina madaraja ya Chakwale na daraja la Nguyani viongozi wote wa Wizara ya Ujenzi mmefika pale Waziri kafika, Naibu Waziri kafika, Katibu Mkuu kafika mara mbili mbili, lakini hakuna matumaini ya aina yeyote na mwaka jana yameondoa magari zaidi ya tisa na imeleta vifo zaidi ya nane, lakini barabara hii siioni kwenye huu mpango kila siku upembuzi yakinifu sasa huu sijui mpaka lini utakwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninataka Mheshimiwa akija aniletee majibu ambayo ni sahihi, na kuna barabara ya kumalizia pale Gairo Mjini inayokwenda mpaka pale Halmashauri pamepakia kama kilometa 120 ya lami na sehemu nyingine ya kwenda kuunganisha na barabara kuu zimebakia kama mita 800 na ilipitishwa kwenye bajeti miaka minne lakini mpaka leo haijaguswa nataka na hiyo nayo nipate majibu ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni mfanyabiashara na nimfanyabiashara nyingi lakini mojawapo ni ya usafirishaji wa abiria leo nilikuwa nipo hapa na ndugu yangu Kiswaga hapa alishalizungumza kidogo hili suala baada ya kuja watu wa Kanda Ziwa na sehemu nyingine kutaka kuanzisha mgomo kama mliusikia kipindi cha nyuma kama miezi mitatu nyuma wa mabasi walitaka kugoma lakini migomo mingine wasije wakagoma wafanyabiashara wa mabasi alafu wakaonekana kwamba ni maadui wa Serikali, si kweli kuna mifumo ambayo imeanzishwa na Serikali na hizi mamlaka


ambazo zimepewa kwenye Serikali ya wizi na ya ajabu kabisa ambayo haitekelezeki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kwenye mabasi sheria inayoleta la LATRA sasa hivi unatakiwa ununue kwanza possy kile kimashine kile cha kuuzia kile, kila basi kile kimashine ni shilingi 1,000,000 mpaka shilingi 800,000 na kwenye ofisi zote kwa hiyo kama una mabasi 50 uwe na vile 50 na kama una ofisi 50 uwe na vile 50 kama huna kuna vendor anakukopesha unamlipa percent angalia wizi huo, halafu ukitaka kuuza kama una basi la abiria 57 unataka kumuuzia Mheshimiwa Kiswaga hapa tiketi kwanza ile mashine unahesabu abiria 57 labda 1,140,000 unaingiza kwenye ile mashine kwanza pesa, pesa yako wewe sio ya abiria, unakijaza kwanza fedha ya basi zima alafu ndio uanze kuuza hasa huoni kama ni kituko hicho? Halafu yaani bado ninadaiwa basi alafu tena kama nina mabasi 50 nitafute Milioni 57 za mtaji kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu ukishauza tiketi fedha haiji kwako inapita kwanza database inapita TTCL, inapita.... halafu wao ndio wanakupelekea benki, yaani fedha yangu, gari yangu halafu wewe unishikie fedha inatokea wapi hiyo. Hiyo biashara ya wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ukienda benki ile statement unapewa nauli 5,000, 10,000 lundo namna hii kwa hiyo, ukizubaa kuangalia utakuta haijaingia wiki fedha, nilimwambia Naibu Waziri kaenda Tanga akashuhudia kuna mtu milioni 23 haijaingia, mwenyewe millioni saba hazijaingia kuna wengine milioni 10 hazijaingia, sasa kwa hiyo na hauna dashboard ya kuangalia kila siku kwa hiyo kila siku uwe una re-statement kwanza biashara gani duniani? Nafanya vitu ninauza halafu fedha yangu sipati, hela yangu Serikali ndio ukaniwekee wewe benki?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshindwa kuweka hii jamani muangalie mifumo hii halafu mnasema leo wawekezaji wawepo, mwekezaji gani atakayefanya biasahra ya kipuuzi kama hii hapa, haiwezekani hata siku moja biashara ya namna hii! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nisingelisema hili alafu mimi ninafanya biashara ya mabasi na watu wote wa mabasi wanajua …ya mabasi ningekuwa mnafi hiki kitu hakiwezekani tunajua sisi EFD machine peke yake mnataka leteni EFD mashine watu watumie EFD mashine huwezi ukawa na duka eti unapiga thamani ya mali za duka milioni 300 halafu unaingiza kwenye mashine ndio uanze kuuza duka inawezekana wapi? Halafu hapa katikati kuna ma-vendor wanakukata two percent haiwezekani huu utapeli ni utapeli wa hali ya juu sana, na wafanyabiashara siku ile walimvisia sana Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli pale Ubungo wakati anafungua stendi lakini bahati mbaya walikosa nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walipiga kelele mzee mzee lakini hajawaona lakini kwakweli ilikuwa hatari kubwa sana hii, hii biashara haiwezekani kwa hiyo, wafanyabiashara wa mabasi hawawezi.

Mheshimiwa Naib Spika, kingine Waziri wa Uchukuzi…

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiswaga Taarifa.

T A A R I F A

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba wenye mabasi wakati mwingine basi linaweza kuharibika njiani abiria anatakiwa arudishiwe fedha, na fedha zipo kwa vendor atafanyaje huyu mfanyabiashara wa basi? (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shabiby.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ninaipokea kwa mikono miwili. Kwa hiyo, nilikuwa ninaomba haya mambo yafanyiwe kazi watu wasije wakagoma halafu baadaye watu wakaanza kulaumu kingine, lakini na Waziri ulichukulie vizuri kwa sababu wakati linapitishwa wewe ulikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi kwa hiyo uwe nalo makini na nilipokuuliza ukasema ulikuwa haujui kama lipo hivi na bahati nzuri kulikuwa na Waheshimiwa wengine Wabunge na hata Mheshimiwa Katibu Mkuu wetu wa zamani mstaafu alilikemea sana hili akiwa Katibu wa CCM lakini lilishindikana wakasema huyo mwanasiasa tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kingine stendi zinajengwa kweli za Serikali na zinatumia gharama nyingi ninazungumza hili kwa sababu Naibu Waziri wa Uchukuzi yupo hapa. Stendi ya Dodoma mwanafunzi anasoma chuo au shule anakuwa na nauli wakati mwingine hata mnamsaidia shilingi 20,000 mnaenda kumshusha nanenane halipii chochote halipi fedha ya mapato ya aina yoyote ya kuingia stendi lakini unamlazimisha ashuke akodishe bodaboda au taxi hilo lipo Dodoma lipo Songea, lipo Iringa.

Mheshimiwa Naibu Spika, stendi ya Iringa kilometa 21 kutoka pale stendi wanaposhushwa abiria mpaka mjini na Halmashauri ile Manispaa haiingizi faida yeyote ila tu wanawaambia shule tu hapa basi liende tupu, basi linaenda huko huko mjini lakini haliruhusiwi kwenda na abiri ili umtese abiri ilimradi tu ashuke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilichogundua…

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa!

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge ukiwa unazungumza taarifa ukishasema mara moja unasimama ili nijue uko wapi, ukishasema taarifa unasimama kimya halafu nikishakuona…

MBUNGE FULANI: Tatizo huyo mrefu sana.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Vita Kawawa.

T A A R I F A

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba sio Dodoma peke yake hata Ruvuma ni Kilometa 25 Songea kituo cha mabasi kilipo na mpaka Makao Makuu ya Mji wa Songea ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shabiby unaipokea taarifa hiyo.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ndio hiyo nilikuwa ninaitaka, kwa hiyo Waziri wetu wa Ujenzi na Naibu wako hebu angalieni mnawatesa abiria kama mimi mwenye basi nimeamua kumchukua huyu abiria kumpeleka mpaka anapotaka wewe kinakuuma nini wewe ambaye huna hata basi nini kinakuuma? Na haupati fedha ya aina yeyote labda angekuwa anaingia ungesema unachukue ile shilingi 300 lakini anashuka ila tu unataka kwamba bodaboda sijui taxi wao unawaangalia wapo pale 60 lakini unatesa watu maskini wengine tumewapa mle lifti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ninataka nizungumzie bandari, bandari ya Dar es Salaam mambo mengi yamezungumzwa lakini ninataka niwaambie haitafanyakazi vizuri tusipoangalia hata siku moja, hapa maneno roho ya kuviziana vyeo, chuki ndizo zilizojaa kuna ule mfumo unaitwa TANCIS upo slow sana bandarini, upo slow sana kwa hiyo ubadilishwe au urekebishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, mimi hapa niliongea Bungeni, tulibishana sana wakati ule na akina Mheshimiwa Mwakyembe na wengine hadi tukafanikiwa kuipeleka ile bandari ya pale Vigwaza, inaitwa Bandari ya Kwala (Dry Port).

Nafikiri mimi ndio nilikuwa mtu wa kwanza kuzungumza baadaye nikawa nimeungana na Mheshimiwa Hawa Mchafu. Bahati nzuri bandari ile mpaka sasa hivi imeshajengwa, imebakia vitu vidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TPA, bandari wamenunua vichwa vya treni viwili kwa ajili ya kutoa mizigo yote makontena yote kutoka bandarini yaje na ile reli ya kwenda Arusha, waje washushe Kwala, pale Vigwaza na ile bandari iko tayari, bado kumalizia tu ili malori yote yasiingie kule Dar es Salaam na ili foleni yote ya bandari hii isiwepo. Cha ajabu hii nchi mpaka leo, nendeni mkaangalie jamani, sisi watu wa Kamati ya Miundombinu tumeenda pale, ile bandari imekwisha, TPA wameshanunua treni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutoka pale bandarini treni inaweza kwa mara moja ikabeba kontena 60, 70 na zikiwa treni tatu au nne; na Kadogosa nimemwuliza, anasema yeye anazo treni, anaweza akaweka hata nne au tano pale. Kwa hiyo, kwa siku tunaweza tukatoa kontena zaidi ya 1000 bandarini kuja pale Kwala ili malori yasiende kule mjini. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Muda umeisha!

NAIBU SPIKA: Muda umeisha Mheshimiwa.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Dah, nilikuwa nataka niseme ya ndege. Haya, basi ahsante sana. Ila siungi hoja mkono mpaka nipate majibu ya kutosha. Bandari ya Kwala nataka nijue inaanza lini kazi; na barabara zangu. Pia ndege za Dodoma - Mwanza bado hamna hapa. (Kicheko/Makofi)