Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nichangie katika Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi. Mimi ni muhanga wa barabara, ninyi ni mashahidi, nikisimama hapa ni kulalamika. Pamoja na kuanza hivi vibaya, lakini nataka niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa utendaji mzuri sana wa kazi ambazo zinaonekana na wananchi wanaziona. Miundombinu inayojengwa na Serikali iko bora na kwa kiwango kizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze sana Engineer Chamuriho kwa kupata nafasi hii ya Uwaziri katika Wizara hii. Hata hivyo, nataka nimtahadharishe kwamba amekalia kaa ambalo kidogo lina moto mkali, akifanya vizuri kama Wizara ya Maji inawezekana mwakani bajeti yake nayo ikawa nafuu. Watu wa maji wewe ni shahidi umekuwepo hapa toka 2015, bajeti ya maji, ilikuwa ni miongoni mwa bajeti ngumu kupitisha ukikaa kwenye hicho kiti. Leo bajeti iliyopita ya maji imejipambanua na watu wa nishati wamefanya kazi ambazo zinaonekana. Niombe sana Mawaziri hawa walioko hapa Mheshimiwa Chamuriho na Manaibu Waziri wawili, waone mifano ya Wizara nyingine, walisimama katika kuhakikisha kazi zinafanyika na zinafanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kwangu ambayo nataka niizungumzie ni Barabara ya Mkiwa – Itigi - Noranga inaenda mpaka Mitundu hadi Rungwa. Upande wa Singida ziko kilomita 219, lakini ukiiunga barabara hii kwenda Makongorosi ambako ndio mkandarasi anaishia kuna kilomita 412 kama si 413, ndio barabara pekee iliyobaki nchi hii ya kuunganisha mkoa na mkoa ambayo ni ndefu kuliko zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mbaya zaidi barabara hii imefumbiwa macho. Barabara hii mwaka 2017 ilitangazwa na ikapata mkandarasi na mkandarasi alishafika site akataka kuanza ujenzi. Bahati nzuri…

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Massare kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hussein Amar.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mchangiaji kwamba si barabara hiyo tu katika nchi hii, hata Mkoa wa Geita, Mwanza na Shinyanga kupitia Wilaya ya Nyangh’wale hakuna lami kabisa. (Makofi)

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa yake, lakini kilomita nyingi…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Yahaya Massare unaipokea taarifa hiyo?

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa yake, lakini kilomita nyingi za barabara za kuunganisha mkoa mmoja na mkoa mwingine ziko katika barabara hii. Barabara hii kutoka Mbeya kwenda Arusha kama mtu anasafiri kama ingekuwa lami huwezi kupita Dodoma ni barabara fupi na ambayo kiuchumi itainua uchumi wa nchi hii. Barabara hii ilipotangazwa mwaka 2017 na ikapata mkandarasi, Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alikuja pale akagundua kwamba, katika mchakato ule wa zabuni kulikuwa na upigaji, akazuia barabara hii isiendelee kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hayati Magufuli akataka wakae wazungumze TANROADS na mkandarasi kilomita ziongezeke kwa pesa ile au pesa zipunguzwe kwa kilomita zilizopo. Mwisho walishindana sijui walifikia wapi, inawezekana watu walishachukua chao hakukuwa na namna, ile tender ikafutwa. Mwaka 2020 Mheshimiwa Rais alipokuja kuomba kura pale kwa niaba ya chama chetu na kuniombea kura mimi na Wabunge wa Mkoa wa Singida, Itigi alizungumzia barabara hii kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami lakini ataweka wakandarasi wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunavyozungumza hapa imeonyeshwa ukurasa wa 36, lakini ukurasa wa 171 katika hotuba ya kitabu cha Waziri, lakini kilomita zinazoenda kujengwa inaonekana ni zile 56.9, lakini kwenye kutangazwa nina mashaka zinaweza zikatangazwa chini ya hapo. Niwaombe sana Wizara hii ili na sisi tusije kuwa wapiga kelele na kushika shilingi ya mshahara wa Mheshimiwa Waziri, atoe nafasi ya kutangaza kilomita za kutosha. Barabara ina kilomita 412 kutoka Makongorosi, akitangaza kilomita 20 au 25 ni miaka mingapi atajenga barabara hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana katika vitu ambavyo Waziri azingatie, Mtendaji Mkuu wa TANROADS yuko hapa, anaijua ile barabara, aone namna ya kufanya barabara ya Makongorosi kuja Mkiwa kuunga Mkoa wa Singida na Mkoa wa Mbeya, inawekewa lami. Angalau kilomita zitoshetoshe hamsini hizi na zingine hamsini hata zikianzia kule kufika Rungwa itaonyesha kwamba Wizara ina dhamira njema ya kutenda haki. Wananchi wa mikoa mingine wasije wakasononeka kwamba wengine wanapendelewa na wengine hawapendelewi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapopiga kura tunapigia kura Wabunge wa CCM, mimi nimetumwa hapa, lakini walituma Wabunge wengi kama mimi kwenye Bunge hili na waliondolewa na sababu kubwa walinyimwa kura kwa sababu ya barabara hii. Naomba sasa Mheshimiwa Chamuriho alinde kura zangu za mwaka 2025. Kama asipojenga barabara hii maana yake sasa yeye ndio atakuwa sababu ya mimi kutoka katika Bunge hili na sitokubali katika bajeti ijayo, hii nitakuwa mpole kidogo, nitashika shilingi tu kidogo, lakini ijayo sijui kama tutapita na bajeti ya Waziri hapa, naamini ataendelea kuwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sasa Mheshimiwa Waziri ukaangalie barabara hii lakini kuna barabara ambazo zinaanzia Handeni, Kibalashi, Kiteto, Chemba, Kwamtoro hadi Singida. Barabara hii ambayo inaambatana na lile bomba la mafuta nayo ni barabara muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni barabara ambayo itakuja kuchechemea uchumi kwa sababu ya mahusiano yatakayokuwepo baina ya mikoa hii mitatu. Mkoa wa Singida, Mkoa wa Dodoma na Manyara lakini na Mkoa wa Tanga mikoa minne ambayo inapitiwa na hili bomba la mafuta. Na ile mikoa ya kule Geita, Shinyanga na Mwanza kule ambayo ukijumlisha inakuwa mikoa kama nane au tisa ambayo uchumi wa Nchi hii utaenda kuongezeka na hata makusanyo ya kodi yatapatikana lakini kama barabara ni mbaya mtu badala ya kulipa kodi kubwa atalipa kidogo kwasababu anachelewa kufika mahali ambako anatakiwa afike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja ambalo nitalichangia haraka haraka la ving’amuzi vya mabasi. Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)