Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunirejesha tena kwenye orodha yako. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na kukutana leo katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishukuru na kuipongeza sana hotuba nzuri ya Waziri wetu wa Ujenzi ambayo ameitoa hapa asubuhi, ambayo imeonyesha dira ya kuweza kuboresha miundombinu katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze yeye pamoja na Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara hii ambao wanafanya kazi nzuri sana kusimamia shughuli za ujenzi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wote tunakiri wazi kwamba miundombinu ya barabara reli na usafirishaji ni kiungo muhimu katika uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba maendeleo ya nchi yetu yanategemea sana ujenzi katika miundombinu pamoja na usafirishaji. Tukifanikiwa kuimarisha ujenzi wa miundombinu katika nchi yetu tutaharakisha sana uchumi wa nchi yetu, ndio maana leo tunapopata nafasi ya kuchangia hapa tunatoa ushauri kwa Serikali yetu ili kuboresha namna bora ya kuweza kuongeza miundombinu katika maeneo yote ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali, imekuwa ikiongeza fedha mwaka hadi mwaka katika kuhakikisha kwamba tunaimarisha sana miundombinu. Ushahidi uko wazi, katika trend ya utoaji wa fedha imeonekana katika bajeti hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamoja na juhudi hizi, ninataka nieleze tu kwenye maeneo haya ya barabara kwa maana ya barabara zetu zinazojengwa. Tumekuwa na kikwazo, kumekuwa na utaratibu wa kwamba lazima GN itoke ndiyo ifanikishe ujenzi uanze.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya niwaombe sana Wizara, niwaombe Serikali waondoe urasimu wa ucheleweshaji wa GN kutoka. Hizi fedha ambazo tunasema leo zimetoka haziwezi kuanza kazi mpaka GN itoke. Imekuwa ni kikwazo maeneo mengi, wakandarasi wanakuwa wako tayari lakini wanazuiliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini muda mwingine mradi unakuwa labda una miaka miwili au mitatu. Katika muda wa mwaka mmoja ukiisha ule muda wa lot ya kwanza unakuta haiwezi kuendelea mpaka GN itoke tena, tunatangaza upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana Serikali kwenye eneo hili, niendelee kushauri kwamba waongeze bidi katika eneo hili, inawezekana sisi wenyewe mawasiliano ndani ya Serikali tuweze kuongeza nguvu katika kutoa GN kwa wakati ili kuisaidia miradi hii iweze kutekelezwa kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii ya GN inakwenda sambamba pia na utoaji wa fedha za miradi. Tumekuwa tukipitisha hapa kwenye bajeti hizi za kila mwaka, lakini tumekuwa tunachelewa kutoa fedha. Lakini pia kuna wakandarasi ambao hawalipwi kwa wakati, wameshamaliza wamewasilisha zile certificates zao lakini bado hawalipwi kwa wakati. niiombe sana Wizara, niiombe Serikali wawalipe wakandarasi kwa wakati ili wawe na nguvu ya kuitekeleza miradi hii ambayo tunawapatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili nitaongelea kwenye upande wa viwanja vya ndege. Viwanja vyetu vya ndege huko nyuma walikuwa wanajenga wenyewe Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, kwa mujibu wa sheria walikuwa wao wanasimamia lakini pia wanafanya ujenzi. Lakini baadaye TANROADS walipewa jukumu hili la kujenga viwanja vya ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, sina tatizo kabisa na TANROADS, TANROADS ni wazuri sana kwenye maeneo ya runways, wanajenga vizuri kabisa. Lakini tuna changamoto


ya facilities nyingine katika viwanja vya ndege. Kwa hiyo, eneo hili limekuwa na utata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana Serikali ifikirie upya; wawarudishie Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wajenge wenyewe viwanja vyao kwa sababu sheria inawafanya wao wasimamie viwanja. Ili wasimamie vizuri lazima wajenge wenyewe ikiwemo kuangalia facilities zinazotakiwa katika viwanja hivyo zikiwemo zile airport towers, lounges zile za kuweza kusimamia kwa ajili ya kuchukulia abiria. Kwa hiyo, nilitaka niseme hili Serikali iangalie upya maelekezo haya waliyokuwa wameyatoa huko awali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu upatikanaji wa fedha nimeeleza vizuri. Nieleze kukumbusha barabara muhimu sana za uchumi; barabara ya Singida – Kwa Mtoro – Kiberashi – Tanga ni barabara yenye kilometa 461. Barabara hii pamoja na kuwa sasa tutaitumia na ni barabara ya kihistoria, na ni barabara inayogusa mikoa minne, tunachoangalia kwenye randama hapa, tumetengewa sasa kilometa 20 badala ya 50 hata zilizotajwa mwanzoni. Barabara hii itachukua muda mrefu kuimaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu, ninaomba iongezewe fedha ili iweze kumalizika kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii imeongoza thamani sasa, inapita sambamba na bomba la mafuta linalotoka Tanga kwenda Hoima. Kwa hiyo kiulinzi na kiusalama barabara hii ni muhimu sana. Niombe barabara hii ijengwe kwa sababu imesubiri kwa muda mrefu kuunganisha mikoa hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama haitoshi, barabara ile ya Mkiwa – Itigi mpaka kwenda kule Rungwa kwenda mpaka Makongorosi. Barabara hii nayo imeshatajwa muda mrefu. Niiombe sana Serikali tutenge fedha barabara hii ikamilike ifungue fursa za uchumi katika mikoa yetu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo lile la Wilaya yangu pale Ikungi kuna barabara inaitwa Ikungi – Mang’onyi mpaka kule Kilimatinde. Barabara hii ni ya kiuchumi, kuna kampuni kubwa za madini zitalipa kodi. Niombe barabara hii iangaliwe namna ya kuwekewa lami ili iongeze fursa za uchumi katika eneo letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilidhani nikieleza suala la barabara kwa nguvu sana pia nikumbushe barabara ile ya wenzetu kule Kahama, barabara ya Bulyankulu – Kahama, kilometa 51. Nayo ni barabara muhimu sana ya uchumi ili nayo ikiwekwa lami kwa sababu kodi tunapata nyingi kupitia madini itasaidia kuongeza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, niendelee kusema tena barabara ni muhimu, miundombinu ni muhimu, naomba Serikali iweze kujenga barabara za lami ili kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo, ninaunga mkono hoja iliyoko mbele yetu kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)