Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii ambayo kwa kweli ni kama ya nyota ya jaha baada ya wale wawili uliowataja kutoonekana hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii kuungana na Wabunge waliopita kuipongeza Wizara ya Maji na Serikali kwa ujumla kwa namna wanavyofanya kazi. Mheshimiwa Aweso na Naibu wako mnaitendea haki Wizara hii. Nami niwaombee kwa Mungu muendelee kuwa na afya njema mchape kazi ili hatimaye malengo ya upatikanaji wa maji wa asilimia 90 mjini na asilimia 80 vijijini yaweze kufikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia hoja hii ya Wizara ya Maji, nami niungane na wajumbe waliokwishachangia Wizara hii inahitaji fedha za kutosha. Nimekaa TAMISEMI tulikuwa na uhusiano wa karibu na Wizara ya Maji, wakati mwingine twaweza kuwalaumu lakini wanajitahidi kufanya kazi, maana wao lazima wapate consultant awaonyeshe kwamba hapa pana maji halafu wapate contractor achimbe, changamoto huja pale ambapo consultant ameonyesha pana maji hapa halafu contractor anakuja kaambiwa chimba mita 90, anachimba mita 90 hapati maji. Nadhani ndiyo maana Wabunge wanalalamika kwamba yanakuwa ni mashimo wananchi hawapati maji na imekuwa ni vilio vya muda mrefu tangu kwenye vile visima kumi vilivyofadhiliwa na World Bank miaka kadhaa iliyopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ni kubwa ni utaalamu na wataalamu wa sekta hii ya maji. Mimi nataka niamini kwamba wataalamu wale hawatoshi na Serikali ifanye uamuzi wa makusudi hasa kwenye kipindi hiki ambacho wanatumia mfumo wa force account kuwa na wataalamu wa kutosha kutimiza majukumu ya Wizara hii, vinginevyo itakuwa ni changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona pale Butiama sina hakika kama wataalamu wanazidi wawili wale ambao ni water engineers (wahandisi wa maji), lakini wana wale mafundi michundo (technicians), ambao ndiyo wengi lakini hawana uwezo wa kutelekeza miradi hii kwa utaratibu wa force account kwa sababu panahitajika na uzoefu wa namna fulani. Kwa hiyo, wakati tunazungumzia utekelekezaji huu bila kumwezesha nguvu kazi ya wataalamu itakuwa ni changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la ujumla ambalo nataka niliseme ni mfumo tu wa kuwaunganishia wananchi maji. Mimi hapa naomba nikiri kwamba Engineer Cyprian Luhemeja wa Dar es Salaam amefanya ubunifu mzuri sana ndiyo maana Dar es Salaam inafanya vizuri. Niliwahi kumuuliza kwa nini kasi ya upelekekaji wa maji kwa wananchi imekuwa kubwa, anasema yeye anatumia mapato yake ya ndani kununua vitendea kazi na kusambaza maji mpaka kwa walaji. Kwa hiyo, gharama zile zinakuja kufidiwa baadaye kwenye bill za watumiaji wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini huku wilayani wananchi wanatakiwa walipie vifaa, vifaa vyenyewe mara nyingi vinakuwa vya bei kubwa, wale wataalamu ndiyo wakanunue zaidi ya laki tatu, nne, tano, mwananchi wa kawaida kijijini kuzipata kwa mara moja inaweza ikawa ni changamoto. Kwa hiyo, tunapofika kwenye usambazaji Waziri atusaidie wajenge uwezo wa taasisi zao ziweze kugharamia vifaa hivi halafu wananchi wakatwe kidogo kidogo wanapolipia bill hizi za maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa kwenye Mkoa wa Mara. Mkoa huu una wilaya zake kama nne zinazungukwa na Ziwa Victoria; Wilaya za Bunda, Musoma, Rorya na kwa kiasi fulani Butiama. Hata hivyo, ukiondoa Musoma Manispaa wilaya nyingine zote zilizobaki zina changamoto kubwa ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Butiama pale kwa Baba wa Taifa, Ikulu pale hawana maji ya uhakika. Ni bahati mbaya wakati fulani viongozi wa Wizara walikwenda hadi wakafanya sherehe ya kusaini mikataba ya utekelezaji wa mradi wa maji ya Mgango, Kyabakari, Butiama na vijiji vile zaidi ya 19 vitakavyonufaika lakini haukutekelezwa wananchi walibaki kushangaa. Namshukuru Mungu mwaka huu kwa kasi ya aina yake wame-sign na mkandarasi na vifaa tumeanza kuviona site, kwenye hili tunawapongeza sana Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi letu sisi watu wa Butiama ni vizuri mradi huu utekelezwe kwa kasi ya aina yako Mheshimiwa Waziri. Mimi naomba baada au kabla Bunge halijaisha twende tuone ile kasi kama inalingana na mpango kazi wa utekelezaji wa mradi ule kwa sababu bado wananchi wana mashaka, je, itakuwa kweli? Sasa kweli tupite kule yale mambo unayofanya maeneo mengine Mheshimiwa ufike pale ukohoe ili watu tuwe na imani kwamba kweli mradi ule utatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunaomba mradi ule utekeleze kwa kasi kuna kata zinazoambaa na Mto Mara na Ziwa Victoria hasa pale Nyabange hawana maji ya uhakika. Ukienda Butiama hawana maji wakati wanaulinda Mto Mara. Mmesea vizuri kwenye hotuba yako Mheshimiwa Waziri kwamba kila mwaka tunaadhimisha Mto Mara na sherehe hizo hufanyika Butiama lakini vijiji hivi vinavyokulindia Bonde la Mto Mara havina maji. Hizi kata zote nne za Bwiregi, Namimange, Buswahili, Silolisimba, zinapakana na Mto Mara lakini hawana maji kabisa, haieleweki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunafarijika kama Taifa kwamba maji ya Ziwa Victoria sasa yanaelekea kuja Dodoma maana tayari yapo Igunga na Tabora Mjini wanasema pameshapata ni zaidi ya kilometa 500 lakini wale wanaopakana na Ziwa Victoria zero kilometa hawana maji. Hatuna roho mbaya, lakini haipendezi kwa watu wanaokulindia chanzo hiki kukosa maji kwa muda wote huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu miradi mingine ikiwemo mikubwa hii ya kitaifa na hata ile ya visima, ni ushauri wetu taasisi zenye watu wengi kama shule tuhakikishe angalau tunapoweka miradi hii iwe karibu na hizi shule. Haipendezi shule ina watoto 1,000 au 2000 hawana chanzo cha maji kwenye maeneo ya shule na wakati huo tunaambiwa kuna magonjwa mengi yanayosababishwa na utumiaji wa maji yasiyofaa. Tuna shule nyingi za sekondari, shule za msingi wilaya ya Butiama na wilaya zingine lakini hazina maji. Ni ombi langu wakati tunatekeleza miradi hii ambayo tunashukuru Mkoa wa Mara na Wilaya ya Butiama imepata vijiji kadhaa tukumbuke kuliko na taasisi za elimu hizi ziweze kupata maji mfano vituo vya afya, zahanati na hospitali ziweze kupata maji ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneo hayo, naomba niunge mkono hoja na niwatakie utekelezaji mwema wa bajeti hii. Ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)