Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu. Lakini kwanza naanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema pamoja na Wabunge wote pamoja na watumishi waliopo kwenye jengo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Waziri wa Wizara hii ya Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso, pamoja na Naibu Waziri wake, Mheshimiwa Engineer Maryprisca Mahundi pamoja na Katibu wa Wizara, Engineer Sanga, na watendaji wengine wote. Kwa kweli wanafanya kazi vizuri, ninawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi hizi nizipeleke kwa Mheshimiwa Waziri, aliwahi kufanya ziara kwenye jimbo langu akiwa Naibu Waziri na ziara ile imezaa matunda na huu mradi ambao ulikuwa umekwama takribani miaka mitano unakwenda kukamilika; hongera sana Mheshimiwa Waziri. Kwa nini nampongeza; alivyokuja kule aliwatia pingu wale wakandarasi na kasi ikaongezeka; hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Naibu Waziri amefanya ziara hivi karibuni na kuona mradi wetu ulipofikia na akatia hamasa, na kuna fedha ilikuwa imepungua kidogo ameahidi kuipeleka ndani ya mwezi huu. Na Inshallah kufikia mwezi ujao mradi huu unakwenda kukamilika katika vijiji 12; hongera sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichangie machache sana. Mradi huu unakwenda kukamilika lakini wananchi walio wengi wa Jimbo la Nyang’hwale ambako umepita huu mradi wanahitaji sana kuvuta huduma ya maji kwenye majengo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha ajabu, gharama za uvutaji wa mabomba hayo kuingiza ndani ni kubwa. Kiwango cha chini ni kuanzia laki tatu mpaka laki nane na ni mita kama kumi tu lilipo bomba lile kuingiza ndani, mtu anachajiwa laki tatu; watu wa vijijini watapata wapi shilingi laki tatu kwa ajili ya kuvuta maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ijaribu kuangalia gharama hizi waweze kupunguza ili wananchi walio wengi waliokuwa na hamu ya kutumia maji ya Ziwa Victoria waweze kuvuta maji waweze kuyatumia ndani ili waweze kufaidika na mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukamilika mradi huu wa vijiji 12, nina kata 15 na nina uhaba mkubwa sana wa maji kwenye jimbo langu. Je, Wizara ina mpango gani sasa wa kusambaza maji kwenye Kata zifuatazo; Nyugwa, Nyijundu, Busorwa, Kaboha, Shabaka, Nyang’hwale, Nundu, Mwingilo, Hafita na Nyabulanda? Maeneo yote yale yana uhaba wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa bahati nzuri mradi huu ulikuwa na thamani ya bilioni 15, kwa usimamizi mzuri wa Wizara chini ya Mheshimiwa Waziri Aweso, tumeweza kubakiza chenji zaidi ya bilioni tatu. Kwa nini hizo bilioni tatu zisiwekewe sasa utaratibu ulio mzuri kuanza kuweka utaratibu wa kuweza kupeleka baadhi ya hizo kata.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, nakuomba, mradi huu ili tuweze kuufaidi mradi huu vizuri ninaomba sana Meneja wa RUWASA awe karibu na wananchi. Kwa sababu leo hii Meneja wetu wa RUWASA wanamtafuta wananchi ili waweze kwenda kufanyiwa tathmini ya kuvuta mabomba majumbani mwao, ile ofisi inakuwa wale watu hawapatikani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba Meneja wa RUWASA – ninamsifu kwa kazi yake nzuri – awapokee wananchi wangu, awaambie gharama na ikiwezekana awape muda maalum kwamba ukilipia leo hii baada ya siku fulani maji utayapata. Lakini majibu yamekuwa hayaeleweki, bei zinakuwa ni kubwa lakini hawapewi muda maalum wa kwamba utakapolipa ni muda gani utapata maji; naomba hili lichukuliwe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata asubuhi niliuliza kwenye swali la nyongeza, nilitoa ushauri kwamba kwa nini Wizara isiweke mfumo kama wa TANESCO kufunga mita za kutumia luku ili kupunguza hii sintofahamu na kutengeneza mazingira ya rushwa. Nitatoa mfano; leo hii Dar es Salaam, kila wanapopita wasomaji wa mita lazima kila mwezi nitume mtu wa kwenda kurekebisha. Unaambiwa 180,000 lakini akienda mtu kule kurekebisha anaambiwa kuna makosa ya kiuandishi tunapunguza gharama unalipa kiasi fulani.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Dar es Salaam tufanye mfano ina watumiaji wa maji labda 1,000, wasomaji wa mita wako watano, kwa nini wasifanye haya makosa? Lakini mtakapotumia huu mfumo ambao ni wa kufunga mita ambazo mtu anatumia kutokana na mahitaji yake, akiwa na shilingi 1,000 anunue 1,000 akiwa na 10,000 anunue 10,000 na akiwa hana inakata kuliko haya masuala ya kila mwisho wa mwezi wanapita wasomaji wa mita, wanakuwa wanachoka. Anakwenda chini ya mti anatafakari tu hii nyumba tuiandikie ngapi anaandika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli hili linafanyika na ni mhanga mmoja wapo. Huwa ninalipa bili ya shilingi 50,000 mpaka 60,000 lakini unakuta inaandikwa mpaka shilingi 200,000, ukituma mtu anakwenda kurekebishiwa; hii ni sehemu yangu moja, je ni watu wangapi ambao wanapata shida kama hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hii inajenga mazingira ya rushwa pia. Mtakapofunga hizi mita haya mazingira yaliyopo hayatakuwepo, hata zile foleni za watu kwenda pale kwenye Wizara ya Maji kurekebisha bili zao hazitakuwepo. Chukueni mfano huo upande wa TANESCO, leo hakuna foleni kwenye masuala ya ulipaji, mtu ananunua luku kulingana na uwezo wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii, naomba myachukue haya mawazo yangu myafanyie kazi, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)