Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Martha Festo Mariki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia jioni ya leo katika Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini kipekee sana, ninampongeza sana Mheshimiwa Jumaa Aweso, Waziri wetu wa Maji na dada yangu, Mheshimiwa Maryprisca Mahundi, kwa jinsi wanavyoendelea kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Mpanda ni mji ambao upo katika Makao Makuu ya Mkoa wetu wa Katavi. Mji huu wa Mpanda una fursa nyingi sana zikiwemo fursa za kilimo, kiutalii na kimadini. Lakini Mji wetu huu wa Mpanda una changamoto sana ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, naiomba sana Serikali kwanza kwa kuipongeza kwa jinsi ambavyo wameonesha jitihada zao katika kuhakikisha Mji huu wa Mpanda unakwenda kupata maji ya uhakika ili kuweza kuwakomboa wananchi wake. Naishukuru sana Serikali kwa kutuletea Mradi wa Ikorongo Na. 01, lakini wakaona haitoshi, Mradi wa Ikorongo Na. 01 ulivyokuwa hautoshelezi kwa maji wakatuletea Ikorongo Na. 02. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali kupitia Waziri wa Maji, ije ifanye ziara katika Mkoa wetu wa Katavi ili iweze kuangalia, je, hizi pesa Serikali ilizozitenga na kupeleka fedha hizi katika Mkoa wetu wa Katavi, je, value for money ipo katika miradi hii ya maji? Maana kumekuwa kuna ubabaifu, wanafunga mabomba maeneo mengine maji hayatoki, lakini baadhi ya mabomba yamekuwa yako chini ya kiwango yanapasuka na hivyo kupoteza fedha nyingi sana za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuombe sana kaka yangu, Mheshimiwa Jumaa Aweso, aje katika Mkoa wetu wa Katavi kuhakikisha kwamba anafanya ziara ili aweze kwenda kushughulika na wale wote wanaokwenda kucheza na pesa za Serikali. Hususan tukiangalia kabisa maji ni uhai na wananchi wa Mkoa wa Katavi wengi wanahitaji maji ili tuweze kufikia ile azma ya kumtua mama ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili; niiombe sana Serikali kwa kuwa imeleta miradi mbalimbali ya maji katika Mkoa wetu wa Katavi na maji hayo yameonekana hayatoshi, niwaombe sana Serikali kipo chanzo cha uhakika sana cha Ziwa Tanganyika. Na kutoka Mji wetu wa Mpanda mpaka lilipo Ziwa Tanganyika ni sawa na kilometa 120. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo niiombe sana Serikali kutoa maji katika chanzo cha uhakika ambacho ni Ziwa Tanganyika ili kwenda kumkomboa mama kwa kumtua ndoo kichwani. Mama zetu wamekuwa wakipata taabu sana katika Mkoa wetu wa Katavi kuhangaika kutafuta maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo sasa jamani ni wakati wa kumuaminisha mama wa Mkoa wa Katavi na wa Tanzania kwa ujumla kwamba Serikali yetu Sikivu inayoongozwa na mama yetu Samia Suluhu, kwamba yukotayari kuwatua ndoo kichwani akinamama wa Mkoa wetu wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sana Mheshimiwa Jumaa Aweso, akinamama wa Mkoa wa Katavi wanalalamika sana wenyewe ndio wamekuwa wahanga wakubwa wa kubambikiziwa bills zinazotokana na maji. Niwaombe sana Wizara ya Maji ikiwezekana kwa nini tusitumie utaratibu kama wa luku; kama luku, mtu anakwenda ananunua units zake anatumia umeme na anakuwa habugudhiwi na mtu ni kwa nini tusifanye utaratibu huu katika suala la maji? Mtu anunue units zake za maji atumie maji, zinapokwisha zikate ili kuondokana na usumbufu wa watu kubambikiziwa bili kubwa za maji ambayo hawajayatumia. Maana kumekuwa kuna maeneo mengine unakuta maji hayajatoka hata miezi miwili lakini bado bili za maji zinakuja, sasa bili hizi zinatoka wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri akashughulike sana na watendaji kwani watendaji wamekuwa wakikwamisha sana Wizara hii ya Maji. Kaka yetu, Mheshimiwa Jumaa Aweso, amekuwa akijitahidi sana na Wizara hii ni ngumu kwa kweli, Wabunge wote tunafahamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sana Mheshimiwa Jumaa Aweso akashughulike na watendaji katika Wizara ya Maji kuanzia ngazi ya mkoa, akaangalie kule changamoto ni nini kinachokwamisha. Serikali imekuwa ikitenga pesa, inapeleka pesa lakini bado maji yamekuwa yakikwama katika maeneo mengi, wananchi wake hawapati maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kumpongeza sana dada yangu, Mheshimiwa Eng. Maryprisca Mahundi na Mheshimiwa Waziri. Niwaombe sana muendelee kuchapa kazi, msife moyo, tunafahamu Wizara hii ina changamoto nyingi lakini kwa kuwa ninyi mama yetu Samia Suluhu amewaamini na amewaweka hapo, tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu mzidi kutatua changamoto ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sana Mheshimiwa Jumaa Aweso; kwa kuwa Mji wetu wa Mpanda ambao uko katika Mkoa wa Katavi hivyo katika miji ile 28 itakayokwenda kunufaika, niwaombe sana Mji huu wa Mpanda tunahitaji maji, ni mji ambao una fursa nyingi sana za kibiashara, mji ambao unakusanya watu wengi sana wanaohitaji kufanya mambo ya kibiashara katika mji wetu. Niwaombe sana tupate maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mkoa wa Katavi tuko chini ya miguu yenu, tunawaomba sana mtuangalie katika hiyo miji 28 jamani na sisi mtupe kipaumbele. Mji wetu umesahaulika kwa muda mrefu, Mkoa wetu wa Katavi umekuwa nyuma kwa mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe katika suala la maji wananchi wa Mkoa wa Katavi tunawaomba sana mtuangalie katika ile miji 28 itakayonufaika na mradi kutoka India basi na sisi mtupe kipaumbele ili twende kuendelea na uzalishaji wa mazao, mambo ya kiutalii ambayo yako katika Mkoa wetu wa Katavi. Suluhisho ni kupata maji ili wananchi wale waendelee kuchapa kazi na kuongeza pato katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii, naunga mkono hoja, naomba tupitishe bajeti ya Wizara ya Maji. Ahsanteni. (Makofi)