Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hoja ya Wizara ya Maji. Kwanza nianze kwa kutoa shukrani kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara nzima kwa ujumla. Natambua hivi karibuni ulitembelea mradi wa maji wa Kilolo, Isimani mradi ambao unaendelea na uko asilimia zaidi ya 30 na ninaamini utakamilika. Pia ninaendelea kushukuru kwa sababu ya ukamilishaji wa mradi wa maji ya Ilula ambao ulikamilika kipindi kile kilichopita na nimeshautaja huo mradi huko siku za nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikija kwenye kuchangia, kwanza nianze kwa kutoa ushauri mdogo. Kuna baadhi ya mashirika ambayo yanatoa huduma za maji, lakini siyo kupitia mfumo wa Serikali. Kama pale Iringa, nafahamu kuna shirika linaitwa Waridi na wamefanya kazi nzuri tu, lakini pia sehemu nyingine nchini yapo mashirika kama hayo. Mimi nashauri kuwe na mfumo wa uratibu ili tujue, kwa sababu wakati mwingine ile miradi wakishaijenga wanaondoka. Wakiondoka kwa sababu haikuwa kwenye mfumo wa Idara za Maji, unakuta wakati mwingine nayo inakufa kama wengine walivyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu, tungefanya tathmini ya miradi ambayo imefadhiliwa na watu wengine nje ya mfumo wa Serikali, lakini inafanya vizuri ili iweze kuingizwa kwenye mfumo wa usimamizi na ufuatiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikijikita kwenye eneo la Kilolo yenyewe, jambo la kwanza nakuomba kupitia kiti chako, naomba Mheshimiwa Waziri aangalie ule mradi wa maji wa Ilula ambao nimeutaja, kwamba ulijengwa na maji yamefika pale, lakini usambazaji bado haujafanyika. Kwa hiyo, watu wanaweza kwanza kwenda kuchota kwenye tanki, inakuwa ni kitu kile kile. Mimi natamani sana kungepatikana fedha ili usambazaji ule ufanyike kupitia mifumo ya maji ile na kuondoa kabisa upotevu wa maji ambao kama tukitumia mifumo ile ya zamani sana, maji yale yatapotea na hayatawafikia walengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuongezea, ule mradi unasimamiwa na IRUWASA na sasa RUWASA wana Kata za pembezoni ambazo zinaweza kunufaika. Napendekeza kuwe na mazungumzo kati ya IRUWASA na RUWASA ili Kata kama ya Uhambingeto ambayo iko pale karibu iweze kuchukua maji kutoka kwenye ule mradi. Hili nimeshalifikisha kwa viongozi wa IRUWASA na RUWASA Mkoa na nina hakika ukiwekwa msisitizo, basi litafanyika kwa haraka zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo miradi mingine ambayo inaendelea ambayo ningependa kuitaja. Kuna mradi mdogo wa maji wa kule Kata ya Kimala. Huu mradi ulianzishwa na wananchi wenyewe kwa nguvu zao na unaendelea vizuri na haya maeneo ya milimani, ndiyo ile mnaanza kusema wakati mwingine Iringa kuna udumavu. Ni kuchota maji, kwa sababu ni milima, watu wanaposhuka na kupanda na wamebeba madumu, yanawakandamiza, kwa hiyo, wanashindwa kurefuka. Kama utafiti ukifanyika,0 utaona kwamba uchotaji maji kwenye milima unasababisha watu wafikiriwe kuwa wadumavu au wafupi. Ni aghalabu kukuta watu watu warefu kwenye maeneo hayo kwa sababu ya uchotaji wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata kama ya Kimala, hiyo inatatizo ya maji na wameanzisha wananchi wenyewe ule mradi. Ili utunusuru tuweze kurefuka, tunakusihi Mheshimwa Waziri, tafadhali ule mradi wa maji uweze kukamilishwa pale Kata ya Kimala. utahudumia...

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nyamoga, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa taarifa mzungumzaji kwamba Mkoa wa Iringa na baadhi ya Mikoa mingine inajulikana kwa udumavu ambao unatokana na mambo ya lishe. Sasa akiongea kama Mbunge, akasema ni udumavu wa kubeba maji tu, atakuwa anapotosha hata na ile elimu ya kutoa kule chini ili watu wetu waweze kuendana lishe bora watake, kuachana na udumavu. Inawezekana waliokuwa na udumavu wa juu, yaani baada ya kubeba, ni shingo tu, lakini hudumavu wa Iringa ni wa ukosefu wa lishe bora kwa wananchi wetu. Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Justin Nyamoga, unapokea taarifa hiyo?

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti ukifanyika utadhibitisha kama kuchota maji na kubeba, kunaweza kusababisha mtu kuwa mfupi au kurefuka. Kwa hiyo, siipokei kwa sababu utafiti bado haujafanyika.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Justin ngoja niliweke vizuri. Mtu mfupi haimaanishi ana udumavu, lazima tuwe tumeelewa vizuri. Ufupi hauna uhusiano na udumavu, kwa sababu hata mtu anaweza kuwa ni mrefu na akawa na udumavu. Kwa hiyo, tutofautishe jamani, hayo ni mambo ya kisayansi. Udumavu ni ukosefu wa chakula katika umri fulani hivi; chakula bora, ama lishe bora. Mimi mwenyewe nimeshabeba ndoo Mheshimiwa usiwe na wasiwasi. (Kicheko)

Mheshimiwa Justin Nyamoga, malizia mchango wako.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba niendelee kuchangia. Kwa hiyo, kuna hiyo Kata ya Kimala, lakini pia kuna Kata ya Ukwega, Vijiji vya Mkalanga, Makungu, Uinome, Lukani, vyote hivyo bado havijafikiwa na vina miradi midogo midogo ya maji ambayo ningependa ikamilishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi ambayo inahitaji kukarabatiwa. Hii ni ile miradi unayokuta ina ukarabati, na nimeiona kwenye bajeti, nashukuru; mradi kama pale Kitoo, Mradi wa Ihimbo, Magana Ilindi na Mradi wa Kipaduka. Hiyo ni miradi ambayo ipo; na miradi ya kule mingi, kwa sababu vyanzo vinapatikana, kwa hiyo, siyo miradi mikubwa kwa sababu ni chanzo, halafu maji yake yanatumia gravity, ambapo kwa kawaida ukarabati wake siyo wa gharama. Kwa hiyo, napenda miradi yote ile iliyopo kwenye Jimbo la Kilolo iweze kuangaliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna mradi mkubwa. Ule mji wa Kilolo unakua na ninajua kwamba Mji wa Kilolo hauko kwenye miji 28. Miji hii ambayo wilaya zinaanzishwa ikiwa ni vijiji, inapokua kwa kasi halafu hatuweki miundombinu ya maji, kawaida baadaye tunapata shida ya maji. Kuna pendekezo limeletwa na IRUWASA la Mradi wa Mto Mtitu na limeshapokelewa kwenye Wizara yako; naomba mradi ule kwa sababu ni mkubwa na utakidhi mahitaji siyo ya Jimbo la Kilolo tu, unaenda pia kwa baadhi ya maeneo ya Jimbo la Kalenga na unafika hata katika Jimbo la Iringa mjini. Nasihi ule mradi uweze kuangaliwa kwenye Mfuko wa Maji ili uweze kufanya kazi katika maeneo hayo na wale watu waweze kutua akina mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba suala zima la kumtua mama ndoo kichwani ni la muhimu sana kwenye Jimbo la Kilolo kama nilivyosema. Nimesema kwa kuzingatia sana suala la maeneo yenye miinuko la milima na maji yanakuwa chini, ndiyo maana nilizungumzia kuhusu kupanda na kushuka kila siku; na nimeshangaa Mheshimiwa Naibu Spika, kama nawe ulibeba ndoo na ukaweza kuwa na kimo hicho, lakini kwetu sisi haifikii hivyo mara nyingi. Nami nasema utafiti ukifanyika, tumebeba sana maji, ndiyo maana tunakuwa hivi. Kwa kuwa sasa tuna Waziri makini, nina hakika wananchi wa Kilolo hasa wale wa maeneo ya milimani wataungana nami kwamba baada ya kuacha kubeba maji na baada ya hili tatizo kwisha, tutakuwa nasi tunapata nafuu kidogo au ahueni hata ya kurefuka ili tuweze kuwa kama Watanzania wengine. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, naunga mkono hoja ili hii bajeti iweze kupita na wananchi wa Kilolo waweze kupata maji. (Makofi)