Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Maji. Kwanza nianze kwa kusema, bila maji kunakuwa hakuna uhai tena. Nitachangia kwa kuanzia na gharama ya kuunganisha maji. Tunasema tunakwenda kumtua mama ndoo kichwani, lakini gharama za kuunganisha maji zimekuwa ni kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimewasikia Waheshimiwa Wabunge wengine wakizungumza hapa, hii inamfanya mtu anataka kuunganisha maji, anatamani apate maji safi na salama, lakini anashindwa kuunganisha maji yafike nyumbani kwake kwa sababu ya kutotimiza takwa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri aweze kuangalia katika Wizara yake namna ambavyo wanaweza kupunguza gharama kwa kuwafanya hawa wanaotaka huduma ya maji angalau waunganishiwe kwanza iangaliwe jinsi wanavyofidia bili zao ili waweze kupata maji. Kwa maana wengi wanataka maji lakini wanashindwa kwa sababu ya gharama ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, vifaa vya kuunganisha maji ni gharama kubwa sana. Kwa hiyo, mwone mtakavyoona vifaa hivi viweze kuwa na gharama ndogo ili watu wengi waunganishe maji na tupunguze hii adha ya akina mama wengi kukosa maji kwa sababu ya gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ni kwamba kumekuwa na mabambikizo ya bili za maji. Wakati mwingine maji yanakuwa hayatoki, lakini unakuta bili inakuja kubwa sasa kuna maeneo mengine ambayo tunaishi unakuta angalau wanatoa taarifa hata message kwamba msoma mita amekuja, amesoma unaweza uka-compare na mita ukaona. Basi hii ienee maeneo mengi ili wananchi wengi waache kulalamika kwa sababu kumekuwa na mabambikizo makubwa ya bili za maji wakati mwingine sivyo zinavyokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tufanye kama wanavyofanya TANESCO, pia tuwe na prepaid meters. Zile meter zinasaidia. Katika Mkoa wa Iringa zipo kwa baadhi, mijini, lakini tunapenda angalau ziwepo, maana mtu atatumia maji kulingana na anavyohitaji maji na hatakuwa na malalamiko hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, upotevu wa maji. Wamezungumza wenzangu hapa, wakati tunakua sisi wengine umri umekwenda kidogo. Wakati tunakua kulikuwa na watu ambao wanatazama haya maji yanavyotoka na kuangalia bomba linafunguliwaje, wanafunga na kama bomba limetoboka wana-repair, lakini sasa hivi hakuna hicho kitu. Unaweza ukapita mara tano mpaka mara sita wiki nzima maji yanamwangika tu, hakuna anayetoa taarifa, hakuna anayepita kuangalia haya maji. Inaumiza kwa sababu maji yanapotea na tunapoteza fedha nyingi. Kwa hiyo, mwangalie jinsi ambavyo mnaweza mkaweka utaratibu wa maji haya yasipote ovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi, naomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alisema atabeba ajenda ya maji kuhakikisha wanawake na Watanzania tunapata maji safi na salama. Namshukuru pia Mheshimiwa Waziri, kwani katika Mkoa wa Iringa nimeona kuna miradi 34. Nashukuru sana kwa sababu kwa miaka mitano tulikuwa tunapiga kelele maji yamekwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natokea Kalenga. Nimekuta kuna miradi ambayo itabeba Kata ambazo tulikuwa tunazipigia kelele. Kuna hii Nyamlenge Construction nimeiona, Isupilo, Tanangozi na nyingine za Isimani na Iringa nzima, tunashukuru hiyo miradi. Tunaomba pesa zinazotengwa, basi na zitoke ziende zikafanye kazi hiyo, maji yapatikane. Tutarudi mwakani tutaulizana hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri akasimamie ili pesa hizi zitoke na maji yakapatikane. Wamezungumza wengine pia, lakini pesa pia zikitoka tuhakikishe wale wanaosimamia maji vijijini, hawana mafunzo yoyote wanayoyapata. Hakuna mafunzo wanayoyapata wale wasimamizi wa maji ndiyo maana unakuta miradi mingi inaanzishwa na inakufa. Kwa mfano, Maafisa Elimu huwa wanakwenda mpaka vijijini, tuache mijini. Mganga wa Wilaya anakwenda kuzungukia wilaya yake. Kwa nini tusiwe na watu wa maji wazungukie hivyo hivyo ili wahakikishe maji yanapatikana kila sehemu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, uangalie utaratibu utakaofaa kuhakikisha hawa wanaoendesha maji huku, vikundi vile vipate kwanza mafunzo ya kuona jinsi ambavyo maji yatatoka vizuri na pia wale wasimamazi waende kule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya CAG imezungumzia jinsi ambavyo Wizara hii imepata changamoto kubwa na nivitu gani ambavyo vimesababisha hiyo? Wamesema miradi mingi haikukamilika kwa wakati kwa sababu hiyo, imeongeza gharama ya miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Waziri ahakikishe jeshi lake au kundi lake linakamilisha miradi kwa wakati ili tusiingize pesa nyingine zaidi katika miradi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu hakuna ubora. Unakuta kuna maeneo wamechimba visima, lakini havitoi maji kwa sababu hakuna chanzo cha kudumu cha maji. Sasa tunajiuliza, hawa ni ma-engineer gani wanaokwenda pale kuchimba kisima tupoteze pesa baada ya mwezi mmoja hakuna maji? Hii haikubaliki, lazima usimamizi madhubuti uwepo kwa Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, kumekuwa na ucheleweshaji wa fedha kwa wakandarasi. Wanafanya kazi, lakini pesa haitolewe kwa wakati. Ofisi ya Rais, TAMISEMI ikiwa na Wizara ya Maji, mhakikishe mnatoa pesa kwa wakati ili wale wakandarasi waweze kuendeleza shughuli za utoaji na kukarabati miundombinu yote ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, najua muda umekwenda lakini mengine nitaleta kwa mahandishi ili niweze kutoa ushauri. Ahsante sana. (Makofi)