Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niwe mmoja wa wachangiaji katika mjadala huu wa Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja kwa sababu tangu asubuhi Mheshimiwa Waziri amewasilisha bajeti yake ya Wizara ya Maji na nimepitia alhamdulilahi Jimbo langu la Igalula nimeona vijiji vingi. Namshukuru sana Naibu Waziri na Waziri wake, kweli Jimbo la Igalula tunakwenda kwenye mapinduzi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wiki iliyopita kupitia Bunge lako hili Tukufu katika maswali ya nyongeza niliuliza Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria unaotekelezwa kwenye Jimbo langu la Igalula katika Kata za Goweko, Igalula, Nsololo na Kigwa. Nikasema mradi ule utekelezaji wake umesimama na nikaiomba Serikali iweze kunipatia fedha kwa sababu umesimama kutokana na kutokuwa na fedha. Kwa Serikali Sikivu ya Chama cha Mapinduzi niliweza kuletewa shilingi bilioni moja ili mradi ule uanze utekelezaji wake wa kupeleka maji katika Jimbo langu la Igalula.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuna changamoto katika mradi huu. Nimshukuru Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Tabora ameweza kuuzungumzia. Mradi wa Ziwa Victoria katika Mkoa wetu wa Tabora Jimbo la Igalula halikuwepo katika mpango. Wakati kampeni tulivyokuwa tunanadi sera alipokuja Hayati Dkt. John Pombe Magufuli tulimuomba Jimbo la Igalula liingizwe katika mpango wa kupelekewa maji ya Ziwa Victoria naye alipokea na akatoa maagizo na ule mradi ukawekwa katika mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi ule ni mkubwa sana, unakwenda takriban vijiji 16 vilivyoko katika maeneo hayo na una vituo 100 lakini tangu tumeubariki mradi ule mpaka saa hizi na malengo ya kukamilika mradi kufikia mwezi Desemba, 2021 sasa hivi tuko mwezi wa tano nikuambie kupitia Bunge hili mradi ule umekamilika kwa asilimia 10. Tumekuwa tukifanya ziara mbalimbali kuuliza kwa nini mpaka saa hizi tunakwenda taratibu na wananchi wana hamu na shauku ya kupata maji kutoka Ziwa Victoria, wanasema tatizo ni fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekwenda kwa Mheshimiwa Waziri mara nyingi sana, mradi ule ni wa kiasi cha shilingi bilioni 11 mmetupelekea shilingi milioni 900 ya kwanza mkatuongezea shilingi bilioni moja na kwenye bajeti hii nimeona mmeweka shilingi bilioni 1.4 kwa maana kwamba huu mradi utakwenda kukamilika baada ya miaka mitatu. Nimwombe Mheshimiwa Waziri hebu aliangalie Jimbo la Igalula kwa sababu tangu tumeumbwa hatujawahi kufungua maji yanayotokana kwenye koki. Kwa hiyo, wananchi wa Jimbo la Igalula, kupitia kata hizo nne watafurahi sana huu mradi ukikamilika kama ulivyopangwa Desemba, 2021. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimboni kwangu nina changamoto kubwa sana ya maji na mlifanya juhudi za makusudi kututolea maji ya Ziwa Victoria kuyaleta Tabora, ni umbali mkubwa sana lakini mlitambua kuwa ardhi na eneo letu la Mkoa wa Tabora upatikanaji wa maji ya kuchimba kwa kutumia visima ni mgumu sana. Nimwombe Mheshimiwa Waziri katika kuibua vyanzo vya upatikanaji wa maji hebu tubuni mbinu mbadala kwa haya maeneo ambayo yamekuwa yana changamoto ya uchimbaji wa visima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimboni kwangu mimi naishukuru Serikali imechimba visima vingi lakini vinafanya kazi kwa miezi miwili, mitatu ni kwa sababu ardhi yetu ina miamba haina maji. Vilevile mmekuwa mnapoteza fedha nyingi, mkandarasi mnampa tenda ya kuchimba visima anawaambia eneo hili lina maji akienda kuchimba anasema maji yalikimbia yakahamia upande mwingine sasa fedha inapotea, haileti tija kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali tubuni vyanzo vingine, kwetu tuna majaluba mengi sana, kuna mikondo mingi ya maji yamekuwa yanaleta mafuriko kwa nini tusiyavune haya maji tukatengeneza mabwawa makubwa. Tukiweka bwawa pale katika Kata yetu ya Kizengi ninyi wenyewe mashahidi wakati wa masika kabla hatujatengeneza barabara ya Chaya - Nyaua ilikuwa kila mwaka barabara inakatika eneo la Kizengi kwa sababu ya maji mengi lakini tungebuni pale yale maji yasiende barabarani yakategwa yangeweza kusaidia hata katika shuhuli za kilimo siyo tu matumizi ya binadamu. Katika eneo letu hasa Mkoa wa Tabora Jimbo la Igalula naomba Wizara ibuni vyanzo vingine vya upatikanaji wa maji maana yapo kwa sababu kila msimu mvua inanyesha na maji yanakuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mradi katika Kata yangu ya Tura alishawahi kuja Waziri wa wakati huo Mheshimiwa Prof. Mbalawa Machi, 2019. Alivyokwenda kwenye Kata ya Tura alikuta kuna bwawa ambalo liliachwa na mkoloni ambalo linatumiwa na Railway Station akasema hiki ni chanzo kizuri pale pale akatoa shilingi milioni 300 ili wananchi waanze kutumia maji katika Kijiji kile cha Tura. Wakaahidi baada ya miezi mitatu maji yataanza kutumika katika Kijiji cha Tura leo mwezi wa 18 maji wananchi wa Tura wanayasikia kwenye redio tu, hawajawahi kutumia maji yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sisi tumeenda kufanya ziara pale tukimuuliza mkandarasi anakuambia tulipewa shilingi milioni 300 mradi wa shilingi milioni 800, kwa hiyo tunasubiri shilingi milioni 500 zingine ili tuweze kuukamilisha. Sasa tunakuwa tunamlaumu mtaalamu, engineer tunaanza kumpigia kelele lakini ukija kuangalia tatizo lingine huku fedha Serikalini hazijatoka. Niiombe Serikali ule mradi ni mzuri sana, ni bwawa kubwa sana lina maji mengi tukiutengeneza vizuri hata wananchi wangu wa Vijiji vya Kalangasi, Malema, Kizengi, Maguliati na Migongwa wanaweza kupata maji kwa sababu ni chanzo kikubwa ambacho waasisi wetu walituachia. Katika bajeti hii nashukuru vijiji vyangu vingi umeniwekea fedha lakini kwenye hii miradi inayoendelea hasa ya Ziwa Victoria na ule mradi wa Tura, naomba aniongezee fedha ili niweze kukimbia na wananchi waweze kuona matunda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini namshukuru Mheshimiwa Waziri amenipa visima sita katika Kata za Mmale, Mwaokoyesengi, Migongwa, Mbulumbulu na Misole. Kwa hivi visima amasema atanipa shilingi milioni 156 huyu mkandarasi anayekuja wamlipe baada ya kutumia maji ndani ya miezi sita asije akaniachia mashimo halafu akaondoka na fedha zikaondoka. Anapokuja kuchimba visima katika haya maeneo ambayo umeniainishia tuone tija ya wananchi wetu ya upatikanaji wa maji kwa sababu tunajua kabisa upatikanaji wa maji kule ni tatizo asije akachukua hizi fedha kwa sababu wamezileta akadhani ni gombania goli.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Waziri yeye ni mkali asimamie haya, wamekuwa wakichimba wanaacha visima havitoi maji na ushahidi upo. Kila siku mnatenga hela za ukarabati wakati visima havitoi maji na penyewe mpaangalie, haiwezi kuwa kila siku tunakarabati kisima halafu hakitoi maji wawaambie visima vinavyotoa maji viko wapi? Katika Jimbo langu la Igalula labda bomba moja au mawili ndiyo yanayotoa maji lakini kwenye takwimu za Waziri unaweza kukuta zaidi ya mambo 40 lakini hayatoi maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai maana binadamu kila siku lazima atumie maji, akila chakula atatumia maji, ni lazima tuliangalie hii sekta katika kipaumbele chake. Nakuomba Mheshimiwa Waziri mradi wangu wa Ziwa Victoria wananchi wa Igalula, Kata za Kigwa, Goweko, Nsololo na mimi nimekuwa nikikuambia kila mara mzee nisaidie na kweli nisaidie nipelekee maji kwenye vile vituo 100 ambavyo umeviandika kwenye bajeti hii wananchi wanasubiri maji kwa hamu ili akina mama wapumzike kuamka alfajiri na kwenda kutafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo na mimi niunge mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)