Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia. Kwanza kabisa, naomba nimshukuru Mungu ambaye ametuumba na ametupa kibali muda huu tuko katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania siku hii ya leo. Naomba nimpongeze sana Waziri wa Wizara hii ya Maji, Naibu Waziri, Katibu Mkuu kwa kazi kubwa wanayoifanya, tunajua mnahangaika sana kutuletea pesa na kuhakikisha kila mtu anapata manufaa ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Jimbo langu mimi kusema ukweli kuna miradi Serikali imeleta pesa mbalimbali, lakini miradi yote haiendi, wananchi hawana maji. Miradi ipo lakini imechukua muda mrefu takriban miaka miwili, mitatu mpaka miaka minne mitano miradi ile haiendi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi mmoja wa Mtakuja - Songambele ambao mpaka sasa hivi uko asilimia 70 lakini mkandarasi anadai shilingi milioni 112 mpaka leo hajapata pesa zake mradi umesimama. Naomba nishukuru Serikali tanki na vile vituo 11 vimekwisha lakini hakuna mabomba wala pump ya kusukuma maji katika maeneo yale ili maji yaweze kufika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi wa Stalike – Igongwa, mkandarasi anadai shilingi milioni 68 mradi umefika 80% leo miezi mitatu mkandarasi hajalipwa pesa zake. Kuna mradi Katisunga, huu mpaka leo ulikuwa una takriban shilingi milioni 138, mkandarasi mpaka leo hajalipwa pesa zake miezi sita mradi umesimama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna miradi ambayo Serikali imeleta pesa lakini tumeshindwa kumalizia takriban miaka minne, mitano, wananchi bado wanaiangalia miradi ile tunasema matanki yamekwisha lakini wananchi bado hawajanufaika na miradi ile. Najua kuna kazi kubwa inayofanyika lakini tunaomba mliangalie suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mkurugenzi wa DAWASA wa Dar es Salaam, Mkurugenzi huyu tunamuona site, anatoka ofisini anaenda kusimamia miradi. Sasa Wakurugenzi na ma-engineer wengine wanashindwa nini kwenda site? Kwa usimamizi huu wa Mkurugenzi wa Dar es Salaam matokeo yake Dar es Salaam sasa hivi shida ya maji kila siku inapungua. Wahandisi wengine wanafanya nini maofisini? Kazi yao ni kwenda kuhakikisha wananchi wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Nsimbo kuna Kata ya Ugala wana Mto Ugala uko pale pale kijijini wananchi wale wanaliwa kila siku na mamba, tunashindwa kuchukua maji pale kutoka pale kwenye mto kuwawekea hapa gati ili waweze kupata maji? Tunajua mnafanya kazi nzuri lakini kuna upungufu mkubwa sana ndani ya maeneo yetu, ma-engineer hawatoki tunaomba watoke wakafanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua kuna mradi ambao sasa hivi nimepewa hela wa Kijiji cha Matandarani lakini unachukua Kitongoji cha Magula ambako kuna wananchi wengi sana pale. Mradi wa Magula unaenda mpaka kwenye Kata ya Ibindi lakini pesa zimeletwa toka mwaka jana mpaka sasa hivi mradi huu uko asilimia 10. Mpaka sasa hivi mmetuletea takriban shilingi milioni 100 na kitu lakini umesimama. Kabla sijaingia hapa nimemuuliza Mhandisi wangu kule mradi unaendaje anasema bado ndiyo kwanza tunaanza kujenga tanki, tutafika kweli? Ukiona tuna mradi huu na ule lakini haiendi wananchi wanapata shida. Mfano, Kata yangu ya Litapunga ina vijiji 10, Kijiji cha Litapunga hawajui maji hata bomba hawajawahi kuona. Najua Waziri anafanya kazi nzuri sana lakini tunaomba miradi hii iende. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Katumba yenye vijiji 16 wametuletea kama shilingi milioni 200 lakini mradi umesimama, uko vilevile. Mheshimiwa Waziri anatembea sana katika miradi na shughuli mbalimbali tunamuona anahangaika lakini watendaji wake wamelala. Waziri anahangaika lakini watendaji wake wamelala usingizi. Kama wangekuwa wameamka kufuatilia miradi wala haya mambo yasingetokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Mkoa wetu wa Katavi tuna Ziwa Tanganyika. Suluhisho la maji ndani ya Mkoa wetu wa Katavi ni maji kutolewa Ziwa Tanganyika na kusambazwa kwa sababu hatuna vyanzo vingi vya kuweza kutosheleza maji ya wana Katavi zaidi ya maji kutoka katika ziwa hili. Naomba sana, najua kuna mikakati mingi na mambo mengi najua Mpanda kuna programu ile lakini naomba katika ile programu ambayo mmetuweka maji yatoke Ziwa Tanganyika ili yaweze kusaidia Mkoa mzima wa Katavi. Maji yakitoka kule haya matatizo ndani ya Mkoa wetu wa Katavi tutakuwa hatuna shida tena.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana na naomba niunge mkono hoja. (Makofi)