Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Jonas Van Zeeland

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima afya na hatimaye nimeweza kusimama kuchangia Wizara hii muhimu, Wizara ya Maji. Pia nimpongeze ndugu yangu Mheshimiwa Aweso pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya katika nchi hii, hasa katika kuhakikisha tatizo hili la maji linaelekea kwisha, hasa katika maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu kuchangia katika hizi Jumuiya za Watumia Maji. Mheshimiwa Aweso bahati nzuri alikuja katika Wilaya yetu ya Mvomero, kama sitakosea mwaka 2016/2017 akiwa Naibu Waziri wa Maji. Tulikwenda Kibati, mimi nikiwa Mwenyekiti wa Halmashauri pale Mvomero, tulikuta mradi wa maji, Jumuiya ile ya Watumia Maji hawana hata senti moja na wameendelea kukusanya kila mwezi fedha kwa wananchi wale ambao wanatumia maji, lakini alikuta hawana hata shilingi 100. Bahati nzuri alichukua hatua akatoa maelekezo wakakamatwa, lakini hawajarejesha zile fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Aweso sasa hivi amekuwa Waziri kamili, tatizo bado liko palepale. Hizi Jumuiya za Watumia Maji zinahitaji mafunzo. Hawa ni wananchi wetu ambao wako vijijini, hawajui namna ya kusimamia hii miradi ya maji. Hii miradi inajengwa kwa gharama kubwa sana, lakini Wizara inashindwa kutenga hata siku tatu ama nne kwa ajili ya mafunzo ili hizi Jumuiya za Watumia Maji waelewe namna ya kusimamia hii miradi ya maji. Sasa hivi naongea na Mheshimiwa Waziri ule mradi ambao alikuja Mvomero pale Salawe, Kibati, hizi mvua zilizonyesha juzi miundombinu ya maji imeondoka na maji ya Mto wa Salawe, yaani yameondoka na mabomba ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo jumuiya ile hawana maji, lakini hawana senti moja kwa ajili ya kurekebisha ile miundombinu na walikuwa kila mwezi wanakusanya zaidi ya shilingi milioni moja. Sasa Mheshimiwa Aweso atapata shida sana kila atakapoenda atakamata watu, lakini hawa watu hawana uelewa, lazima wapewe mafunzo ili wajue wanachokifanya ni nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimwambie Waziri, sisi Mvomero tuna vyanzo za uhakika vya maji, lakini ni wilaya ambayo ina shida kubwa sana ya maji. Miradi mingi ambayo iko pale kwetu bado inasuasua; tuna mradi ambao uko pale Doma, tulipata fedha za World Bank, huu mradi ulianza kujengwa 2008 mpaka 2010, una vituo vya kutoa maji 15, lakini mpaka leo nazungumza vituo vinavyotoa maji ni vitatu. Vituo vingine hivi havitoi maji mpaka wasikie kuna ziara ya kiongozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2013 ulipokuja mwenge pale Doma vituo vyote vilitoa maji. Mwenge ulipoondoka vituo havikutoa tena maji. Akija kiongozi mwingine yeyote yule vituo vinatoa maji. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Aweso atuangalie sana sisi Mvomero, tuna miradi mingi kama nilivyosema huu wa Doma ambayo haitoi maji, miradi hii inatoa maji pale wanapokuja viongozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo linguine, unit moja pale Doma, wana-charge kwa sh.3,000 kisingizio wanasema kuna wakati wanatumia generator ambayo inatumia mafuta. Sasa tunashindwa kuelewa maeneo mengine sh.800 na kitu, sehemu nyingine 1,000 sehemu nyingine ndio kama hivi 3,000. Bora kuwe na bei elekezi ambayo Wizara itaitoa ili wananchi wetu wajue wanatakiwa kulipa shilingi ngapi? sh.3,000 kwa mwananchi wa kawaida na pale Doma tunajua kuna tatizo kubwa sana la tembo hakuna pale mkulima yeyote sasa hivi ambaye analima. Hali ni mbaya ya kimaisha, lakini mtu analipa unit moja sh.3,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri walitupa fedha kwa ajili Miradi ya Dihinda, Masimba, Vianzi, Lubungo na Kihondo. Miradi hii imekamilika japo sio kwa asilimia 100, lakini bahati nzuri inaanza kutoa maji, inasuasua kwa sababu ya hizi jumuiya. Kuna Mradi mmoja upo Dihinda kama wiki tatu zilizopita nimetoka kufanya mkutano pale, tatizo ni kwamba jumuiya ile hata kukabidhiwa mradi hawajakabidhiwa, hawajui wasimamiaje ule mradi. Naomba sana Waziri atusaidie, lakini na miradi mingine hii kama nilivyosema bado ina changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa 2021/ 2022, nimeona katika Vijiji vya Rusungi, Mwalazi, Chenzema, Kibuko, Luwale, wametenga fedha kwa ajili ya miradi ya maji, lakini pia tutakuwa na mradi mmoja mkubwa wa kutoka Tandali kwenda Homboza ambao utakwenda mpaka Mlali. Nimpongeze sana Waziri. Pia tuna Mradi ambao nimeona Kibogoji, Pandambili na Ndole Matale; Mheshimiwa Waziri naomba sana hizi fedha zisije zikaondolewa, tupate miradi hii katika hivi vijiji ambavyo nimevisema.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lingine, nimwombe Mheshimiwa Aweso, tulikuwa na ma-engineer wawili wameshahamishwa wote. Mwingine amehamishwa kama wiki mbili zilizopita, pale tuna ma-technician watatu tu. Sasa tatizo na changamoto kama nilivyosema hapa za maji hazitaweza kwisha kama hatuna engineer. Nimwombe sana Mheshimiwa Aweso atupatie engineer pale, lakini pia atupatie na gari la uhakika kwa sababu jiografia yetu sisi ni kubwa sana, lazima awe na gari la uhakika la kuweza kufika maeneo yote kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ile miji 28 na sisi Mvomero katika Kata ya Dakawa, Wami Dakawa Sokoine, tumepata mradi. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri niombe tu pale Dakawa pana shida kubwa sana ya maji, tunategemea huu mradi utakwenda kumaliza tatizo lote la pale Dakawa.

Mheshimiwa Naibu spika kuna Kijiji kimoja cha Sokoine siku moja tuliona kwenye vyombo vya habari ng’ombe na wananchi wanatumia bwawa moja ambalo ni la wafugaji, wananchi na wenyewe wanakwenda kuchota maji pale. Kwa kweli, hali ni mbaya, hali inatisha, tunaomba sana watusaidie, japokuwa tumepata fedha za dharura kwa ajili ya kutoa maji Wami Dakawa kuyapeleka pale Sokoine, lakini bado tatizo lile litakuwepo kwa sababu, mradi ule ni mdogo, hautoshelezi Kijiji kizima cha Sokoine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo lingine kubwa sana la maji katika Kata ya Msongozi. Kata ya Msongozi hawana chanzo chochote cha maji, wanatumia maji ya kwenye mabwawa, wanatumia maji ya kwenye mito, ndio maji yao ambayo wanapikia, ndio maji yao ambayo wanayatumia kwa ajili ya kunywa. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri atuangalie sana wananchi katika Kata hii ya Msongozi, kuna shida kubwa sana ya maji. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kama itakupendeza…

T A A R I F A

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Van Zeeland kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Msongozi.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana Mbunge wa Mbeya Mjini. Nataka tu nimpe Taarifa mchangiaji anayechangia sasa anavyoitaja Kata ya Msongozi ndiyo kata ambayo jina hili ninalolitumia ndio nyumbani kwa mume wangu mimi. Kwa hiyo, hakikisha maji hayo yanakwenda kwenye Kata hiyo ya Msongozi, Morogoro. Ahsante sana. (Kicheko/Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Van Zeeland, malizia mchango wako.

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea Taarifa kwa mikono miwili. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge nitapambana na Mheshimiwa Aweso hadi kuhakikisha pale maji yanatoka, maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimalizie mchango wangu kwa kusema, nimkaribishe sana Mheshimiwa Aweso. Baada ya Bunge hili la Bajeti kwisha Wilaya ya Mvomero iko barabarani, ni lami tupu, twende pale tukazungumze na wananchi. Matatizo ni mengi siwezi kuyaongea yote hapa matatizo ya maji, lakini kikubwa nimkaribishe Waziri Mvomero, karibu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)