Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Edward Olelekaita Kisau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiteto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii na kwa wale ambao hawafahamu Mheshimiwa Naibu Spika ni Mwalimu wangu, alinifundisha Law School of Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda nimpongeze sana Waziri wa Maji; Waziri wa Maji kati ya wageni wangu niliowatambulisha leo, nilitembelewa na waliogombea na mimi, aliyegombea kupitia ACT Wazalendo Ubunge na aliyegombea kupitia CUF, wa ACT Wazalendo Ndugu Kamota amekubaliana na kasi ya Chama cha Mapinduzi na kazi anazofanya Mbunge hapa na amekubali kuungana na Chama cha Mapinduzi. Namshukuru sana kwa uungwana wake mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiteto nilishazungumza hapa ni takribani square kilometa 17,000 ni majimbo mengine kama matano hivi ni jimbo kubwa sana. Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ambayo naongelea kila wakati kwasababu, ndio social contract ya kwetu na wananchi ukurasa wa saba na naomba ninukuu kabisa “Kuongeza kasi ya usambazaji maji safi na salama kwa asilimia 85 vijijini na 95 mijini”.

Mheshimiwa Waziri, kwanza kabisa naomba bajeti ya Kiteto msiipunguze hata nukta moja, tuanzie hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile, kwanza Mkoa wa Manyara overall ni asilimia 58 tunapata maji below national average kwa hiyo, katika kutengeneza vipaumbele hivi tuangalie mikoa ambayo ipo nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiacha Manyara sasa, Wilaya ya Kiteto ni asilimia 52 na Mji wa Kibaya ambao ndio mji wetu kwa miaka 20 sasa, ni asilimia 44 maji na miundombinu pale mjini yamechakaa ni ya mwaka 1980. Mheshimiwa Waziri, ukitutengea milioni 100 tutaweza kufumua mifumo ya maji ile na kutengeneza vizuri sana, ili Mji wa Kibaya ambao ndio sura ya wilaya ipate maji ya kutosha. Kata kama za Njoro Mji wa Matui, Kijungu, Lengatei, Dongo hazina maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Hotuba ya Rais mama Samia Suluhu Hassan, ukurasa wa 29... (Makofi)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Olelekaita kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani.

T A A R I F A

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni mdau wa Wilaya ya Kiteto nalima mashamba yangu kule, Mheshimiwa Mbunge ametaja kata ambazo zinakosa maji kwenye eneo hilo na nilikuwa namkumbusha tu kwamba asisahau Kata ya Dosidosi ambayo nimewekeza pia. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge alikuwa anaendelea kutaja kata zake. Haya unaipokea taarifa hiyo, unakumbushwa kwamba kuna kata inayohitaji.

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea sana sana kabisa na nimkumbushe tu kwamba Katibu wa Mbunge anatoka Dosidosi. Na napokea sana na niseme tu kwa kuwa amenikumbusha, nilipata bahati ya kutembelewa na aliyekuwa Makamu wa Rais ambaye ni Rais wetu sasa Mama Samia Suluhu Hassan, kunitafutia kura na kituo cha kwanza kabisa ni Dosidosi. Dosidosi ni Kijiji cha kwanza tu ukitoka Kongwa na kutokana na ukame wa Jimbo la Kiteto, Mheshimiwa Rais aliahidi mabwawa Kiteto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nakushukuru sana na ni kweli kama alivyosema naendelea kutaja kata zangu ambazo hazina maji; Kata ya Njoro, Kata ya Makame, Kata ya Lolera. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nasema hotuba ya Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan ukurasa wa 29 naomba ninukuu. “Aidha, kwa maeneo yasiyokuwa na vyanzo vya maji tutajielekeza katika ujenzi wa mabwawa ya kuvuna maji ya mvua”. Kutokana na jiografia ya Jimbo la Kiteto mabwawa, na kuna ahadi ya muda mrefu ya Serikali ya bwawa la Dongo, Kata nzima ya Dongo. Bwawa hili likijengwa vijiji sita na kata mbili zitanufaika na mradi huu na wananchi walishatenga eneo kubwa tu. Kwa hiyo, namuahidi Waziri kati ya maeneo ambayo tutakwenda ni Dongo ukaone bwawa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, shida nyingine, kutokana na ukubwa wa Wilaya hii engineer ni mmoja tu na mafundi wako watatu, haiwezekani. Tunaomba engineers wawili tunaomba na mafundi sita, hatutaki wengi sana sisi sio selfish sana hao tu Mheshimiwa Waziri. Tukipata na magari mawili kutokana na jiografia ya jimbo hili utatusaidia sana na maji yatapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji wanaoumia sana ni wakina mama kwa hiyo, kama tutaweza kutimiza takwa hili la Chama Cha Mapinduzi tutakuwa tunawasaidia wakinamama wengi sana nchini. Baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa nafasi hii, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)