Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii ya Maji. Kwa kuanza napenda nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anafanya katika Taifa letu, katika kuhakikisha kwamba Watanzania tunapata maji ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waswahili wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, Mheshimiwa Aweso anafanya kazi kubwa sana. Sisi kama Wabunge tutaongea masuala mengi humu Bungeni, lakini yote ni katika kushauri, haiondoi ukweli kwamba Wizara ya Maji ipo vizuri na inafanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, sote tunafahamu kwamba kwa miaka mingi tangu nchi yetu ipate uhuru, miradi mingi sana ya maji imeshapelekwa kwenye maeneo yetu. Kama haitoshi ni fedha nyingi sana ambazo zimepelekwa kwenye miradi ya maji na miongoni mwa Wizara ambazo zimeshapelekwa fedha nyingi ni Wizara hii ya Maji, lakini bado kilio ni kikubwa sana, unapokuja suala la maji kilio ni kikubwa sana huko kwa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii inasikitisha zaidi kwa sababu vilio hivi vinatoka kwenye maeneo yale yale ambayo tayari Serikali imeshapeleka miradi mikubwa ya maji. Ukiangalia chanzo cha haya yote ni kwa sababu hakuna usimamizi wa kutosha kule chini kwenye mikoa yetu, wilaya zetu na kata zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2019, Bunge lako Tukufu lilifanya marekebisho kwenye Sheria ya Maji na mojawapo ya kipengele ambacho kilikuwa ni muhimu sana kwenye hiyo sheria ni kuzipa mamlaka zile jumuiya za maji ziweze kuajiri lakini vile vile kufukuza wataalam wa maji endapo watakuwa hawajafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni jema, lakini ni lazima kwamba Serikali iweze kutia mkono wake. Serikali pamoja na kwamba ina dhamira kubwa na nzuri ambayo inayo lakini watambue kwamba bado ina kazi ya kufanya ili kuweza kufikia malengo ambayo tumejiwekea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunafahamu kwamba Sera ya Maji ya mwaka 2002 imesema wazi kwamba jukumu la maji si la Serikali peke yake, wananchi wanajukumu kubwa la kuchangia huduma za maji. Lakini vile vile hizo fedha ambazo zinapatikana kwenye hiyo miradi ya maji lazima ziende kwenye uendeshaji, kwenye upanuzi, lakini vile vile ziende kwenye ukarabati wa miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa tafsiri hiyo, ili sasa sheria pamoja na sera ziweze kufanya kazi, hatupaswi kuachia jumuiya za maji peke yake ndiyo ziajiri wataalam wa maji. Nasema hivi kwa sababu tumeshuhudia maeneo mengi ambapo kuna Jumuiya za maji, wataalam wengi ambao wanaajiriwa kwenye hayo maeneo ni wale ambao wengi wao hawana uzoefu wa kutosha. Lakini wengi wao hawana ujuzi wa kutosha. Kwa hiyo unakuta kwamba miradi ile pamoja na kwamba Serikali imeweka pesa nyingi, lakini ile miradi inakuwa haina sustainability, ndani ya muda mfupi tunaona miradi imekufa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile ile dhana kamili ya kuweka Sera ya Maji ili basi wananchi waweze kuona matunda ya fedha zao ambazo wanachangia kwenye miradi, inakuwa haipo. Pia sote tunafahamu kwamba, ili miradi ya maji iweze kuleta tija ni lazima kuwepo na usimamizi mzuri wa miradi ya maji. Kwa hiyo tutaongea mambo mengi sana hapa Bungeni, lakini kama hakuna usimamizi mzuri itakuwa ni sawa na kazi bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kutokana na hayo nataka nishauri masuala machache na kwa sababu najua Mheshimiwa Waziri wa Maji ni kijana ambaye ni msikivu, naamini atafanyia kazi ushauri wa Wabunge. Ushauri wangu wa kwanza; ni vema sasa Serikali ikachukua hili suala la hizi jumuiya kuweza kuajiri wataalam wa maji liwe ni suala la Serikali. Kwa maana ya kwamba Serikali iwatafute hawa ambao ni wataalam, iwaajiri, lakini vile vile iwalipe, kwa sababu jumuiya nyingi zimeshashindwa kuwalipa na inapelekea miradi kusuasua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo zuri ni kwamba Wizara hii inayo Chuo cha Maji na kile chuo kimekuwa kinazalisha wataalam karibu kila mwaka na wale wataalam wapo tu mtaani hawana kazi. Kwa nini sasa Wizara isifikirie kwamba wawaajiri hawa watalaam angalau kwenye kila kata ili basi kila kata kuwe na usimamizi mzuri wa miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Rais wetu wa Awamu ya Sita alizungumza alipokuja hapa Bungeni, alisema kwamba Serikali yake imejipanga kuweka usimamizi mkubwa wa fedha za Serikali ambazo zinatoka Serikalini kwenda kule chini kwenye miradi. Hata hivyo, swali la msingi la kujiuliza ni kwamba, hizo fedha zinapoenda kule chini je, ni nani ambaye ni mtumishi wa Serikali anayewajibika moja kwa moja? Kwa sababu hawa ambao walikuwa wanaajiriwa na hizi jumuiya hawawajibiki kwa mtu yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawawajibiki kwa Serikali na kuna baadhi ya maeneo tumeshuhudia kabisa kwamba wamekusanya pesa na wakakimbia nazo kwa sababu hakuna sehemu wanapowajibika. Kwa hiyo nataka niombe, pamoja na kwamba Serikali italifanyia kazi hili suala, lakini kuna ulazima mkubwa sana wa Serikali watakapoajiri hawa wataalam kila kata waangalie sasa namna gani ambavyo watatekeleza ile sera ambayo tunasema kwamba ni muhimu hawa wataalam waweze kupatiwa mafunzo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wapatiwe mafunzo namna gani ya kuweza kusimamia miradi ya maji, kwa sababu good governance ndiyo kitu pekee ambacho kinatakiwa ili miradi ya maji iweze kuleta tija. Kwa hiyo mafunzo ni suala ambalo ni la msingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, linguine, tunatambua kwamba wanahitaji pia kupata uzoefu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa naambiwa hapa kengele ya pili imegonga.

MHE. JULIANA D. SHONZA: Aah! Mara hii imeshagonga.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba dakika moja niweze kumalizia. Pia katika Mkoa wetu wa Songwe, naomba sana Serikali iweze kutusaidia, mkoa ule ni mpya lakini mpaka sasa hivi hatuna mradi wa kimkakati ambao tayari umeshafanyika katika Mkoa wa Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunao mradi ambao unaweza kuhudumia Miji ya Tunduma, ikahudumia Mji wa Vwava pamoja na Mji wa Mloo kwa kutoa maji Ileje, kwa hiyo napenda kumwomba sana Mheshimiwa Waziri, aweze kuliangalia vizuri suala hili la Mkoa wetu wa Songwe ili uweze kuwa na mradi mmoja wa kimkakati kuliko kuwa na miradi mingi ambayo haina tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)