Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa mara nyingine kwa kunipa fursa ya kuzungumza katika sekta yetu hii muhimu sana ya maji. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu wake pamoja na wataalam wengine, hususan wa pale kwetu Mufindi na katika Mkoa wetu wa Iringa kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru pia Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, kwa hotuba yake aliyoitoa alipokuja hapa Bungeni. Kwenye ukurasa wa 29 alizungumzia vizuri sana sekta ya maji. Moja ya changamoto alizozizungumza ni usimamizi thabiti kwa lengo la kufikia malengo yaliyowekwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza, lakini pili, napenda kushauri kwenye baadhi ya maeneo. Pale kwangu nikiri kabisa Mheshimiwa Waziri ameanza kwa speed kubwa na nzuri sana. Unaona miradi kichefu chefu ambayo ilikuwa kero kwa muda mrefu, inaanza kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajielekeza mchango wangu kwenye eneo langu la Mufundi Kusini, Jimbo ambalo limejitolea kutunza vyanzo vya maji kwa kupanda miti mingi ili Watanzania kwa ujumla waendelee kunufaika na mvua na hatimaye maji tuendelee kuyapata kwa wingi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na mradi wa Sawala. Nakuomba Mheshimiwa Naibu Waziri, umekwenda pale; huu ni mradi wa muda mrefu sana na kuna miradi kama mitatu ambayo imeanzishwa kwa muda mrefu lakini bado haijakamilika japo speed yake kwa sasa inaridhisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nina maombi mawili; moja, napenda kupata commitment yako Mheshimiwa Waziri, utusaidie ili ikamilike haraka iwezekanavyo, ikiwezekana mwaka huu hii miradi iishe. Pili, mradi huu ulikuwa katika vijiji vine; una Vijiji vya Lufuna, Sawala, Mtwango na Kibao. Katika Kata hiyo kuna Kijiji kinaitwa Mpanga na Kitilu, haufiki. Namwomba Mheshimiwa Waziri kupitia atusaidie mradi huu ufike maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tunao Mradi wa Kimilinzowo, nao huu ni sehemu ya miradi kichefuchefu; kwa miaka mingi huko nyuma tangu ulipoanzishwa haukukamilika. Nimeona kasi yako na wataalam, na nimemwona Meneja wa Maji wa Mkoa na Meneja wa RUWASA wa Wilaya wanavyohangaika. Mheshimiwa Waziri toa timeframe, mwaka huu mradi huu ukamilike tumalize kabisa hii kazi. Pia na vijiji Jirani kama Ihawaga vipate maji, Kinegembasi kipate maji, Nyigo napo unasuasua; tusaidie Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, namba tatu, tuna mradi wa Nyororo. Bahati nzuri miradi hii yote Waziri wetu sio mgeni, amefika. Huu mradi wa Nyororo ni mradi ambao unagusa watu wengi kama miradi mingine nilivyoizungumzia, na uko barabarani pale. Changamoto ya mradi huu pia katika Kata yenye vijiji vinne unazungumzia kijiji kimoja. Moja, haujakamilika; naomba pia miradi hii mitatu hebu ikamilike basi. Hii story ya kuzungumziwa mradi umeanza, umeanza, iishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nampongeza Mheshimiwa Waziri, tulizungumza hapa kwenye simu, akazungumza na Katibu Mkuu wake wa Wizara ya Maji, akazungumza na wataalam, wamekwenda site, Meneja wake wa Mkoa na Wilaya wamekwenda kwenye vijiji vingine ambavyo viko katika Kata hiyo; wamekwenda Njojo, wamekwenda Ving’ulo na Nyororo shuleni kufanya design ili iwe extended katika Kata nzima. Nakupongeza sana, lakini wakaenda mpaka na jirani ya Maduma na vijiji vyake vya Honga Maganga, Maduma na Ihanganatwa. Lengo ni kwamba Kata hizi mbili zinufaike na mradi huu. Naomba sana, hebu ukamilike basi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuzungumzia mradi maarufu kwenye Jimbo letu wa IMAI. Huu ni mradi unaogusa Kata tatu za Ihowanza, Malangali na Idunda. Ni mradi wa muda mrefu sana. Changamoto ni moja tu; miundombinu imechakaa. Nashukuru kuona kwamba katika mwaka huu wa fedha mmezungumza kwamba mtatutengea fedha kwa ajili ya kuufanyia marekebisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, mradi huu, moja, angalau na wenyewe ukikamilika vijiji zaidi ya kumi vitanufaika. Pili, kama mkianza kuufanyia matengenezo ya miundombinu iliyochakaa, naomba sana Mheshimiwa Waziri aende ukaguse mpaka Kata ya Mbala Maziwa ambako changamoto ya maji ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo ningependa kukugusia miradi mipya. Hapa nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa jinsi alivyoiitikia kwenda kusaidia kuanzisha miradi mipya mitatu katika Jimbo letu la Mufindi Kusini Mungu akubariki sana. Wanamufindi Kusini wanamshukuru kwa jinsi alivyoanza design katika Kata ya Igowole mradi wa kupampu maji ambao utagusa Vijiji vya Ibatu, Nzivi, Igowole mpaka Kisasa. Nimwombe sana, kwanza ni hatua ya kwanza kumaliza jambo linguine, ikianza itimie ndani ya muda mfupi ili wananchi waweze kupata maji katika jimbo letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimshukuru Mheshimiwa Waziri, nimeona ameweka Mradi wa Gravity hapa wa Mgogoro ambao unakwenda mpaka Kata ya Kihohela. Nimshukuru sana kwa sababu eneo hili ndiyo kila siku naongea na Waziri wetu wa Ujenzi hapa, ni eneo ambalo kuna viwanda vingi, barabara ni mbovu, maji ni changamoto, lakini Mheshimiwa Waziri wa Maji, umekuwa msikivu, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ombi langu, Vijiji vingine kama Kitasengwa sijaviona, nimwombe aende Kitasengwa, Lole, Lugema mpaka Mabaoni pamoja na Makungu ili wote wanufaike. La pili, Mheshimiwa Waziri anapokwenda kwenye Kata ile ya Kihohela ambayo ni sehemu ya jirani atusaidie, sijaiona Magunguri kwa sababu bado mradi wake haujakaa vizuri, Magunguri na Isaula pia inufaike.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, lakini kabla sijamaliza, nizungumzie kidogo Mradi wa Idete, Kata ambayo ipo kama kisiwani, imeachwa kwa mara ya kwanza wanakwenda kuweka historia ya Mheshimiwa Waziri wetu, maji hayakuwahi kufika pale. Waziri amepeleka visima, nimwombe vile visima alivyopeleka pia apeleke na mabomba ya usambazaji maji ili wananchi wa Idete waendelee kumshukuru Rais wao kwa jinsi alivyomtuma na yeye ameelewa na wasaidizi wake wameelewa, sasa wanakwenda kuwapelekea maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamaliza nina maombi madogo mawili, madogo tu na nita-mention kwa sababu ya muda wako, najua wachangiaji ni wengi katika sekta hii. Moja, tunayo changamoto kwenye miradi iliyokuwa imeanza kwenye Kata za Kasanga, lakini pia kuna Kata ya Mtambula na vijiji vyake, pamoja na Kata ya Mninga na Luhunga. Nimwombe sana Waziri akajaribu kutazama maeneo haya pia. Namwomba Mheshimiwa Waziri apeleke wataalam pale wakatusaidie ku-design ili kero ya maji iishe. Mto Ruaha unaanzia pale, wao ndiyo wanatunza kwa nini wawe na shida ya maji? Halafu watu wengine wanufaike na maji hawa si ni Watanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia sasa, nipende pia kuwaombea wenzangu wa jirani kwa sababu mradi huu kwa muda mrefu umezungumzwa, mradi wa vijiji 14 ambao unagusa Kata ya Iswagi, Ihalimba na Ikongosi, namwomba sana Wazri ukakamilike mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)