Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Tumaini Bryceson Magessa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Elimu. Kwa sababu ya muda nitachukua maneno machache ya kuchangia hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee elimu bure. Hii elimu bure ambayo tuliianza mwaka 2016 ilikuwepo siku nyuma inatupelekea mwaka 2022 kuwa na wanafunzi wengi watakaoingia sekondari. Nashukuru kwamba Wizara ya Elimu ambayo ndiyo Wizara ya kisekta ikishirikiana na TAMISEMI imekuja na mpango ambapo kutakuwa na shule 1,000 zitakazoongezwa kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukweli ni kwamba ukigawanya kwenye halmashauri zetu utaona kila halmashauri itapata karibu shule tano, kama unafanya ugawaji sawia ule. Mahitaji halisi yaliyoko kwa wananchi wetu sasa ni karibu kila kata inahitaji sekondari nyingine kutokana na wingi wa hawa wanafunzi. Kwa mazingira hayo niishauri Wizara pamoja na mpango mzuri waliokuja nao Waziri na Naibu Waziri na hata TAMISEMI wa shule 1,000, zitakuwa hazitoshi kuhimili wingi wa wanafunzi ambao tutakuwa nao baada ya elimu bure kuingia sekondari, karibu kila kata lazima iongezewe sekondari nyingine moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine ambacho nasimama kuishauri Wizara ya Elimu hapa kama nchi tatizo letu ambalo tumekuwa tunalisema hapa ni uadilifu. Uadilifu ni tatizo kubwa, je, ni mahali gani kwenye mitaala yetu tunaweza kuingiza watu wajifunze uadilifu. Kwa sababu kama nchi tatizo kubwa ni uadilifu na tumekuwa tunalisema hata hapa Bungeni, je, kwenye mitaala yetu ni mahali gani kwenye shule tulizonazo wanafunzi wetu wanaweza kuwa wanapata huu uadilifu. Nafikiri Wizara iangalie ni mahali gani tunaweza kutengeneza uadilifu wa watu wetu. Uzalendo tunaweza kuupata hata JKT na mahali pengine, je, uadilifu huu tuuingize wapi ili watu wetu wawe waadilifu na tufike safari yetu ya maendeleo tunayoenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ambalo nataka niliseme ni kutoka kwenye Jimbo langu Busanda na hata kwa jirani zangu Mbogwe, kuna majimbo makubwa kabisa ya kata 25 hayana high school hata moja. Kata 25 kubwa au kata 30 kubwa hazina high school hata moja na mpango wa Serikali ni kuanzisha shule moja, shule moja haiwezi kuwabeba hawa wanafunzi wote hata kama wanatoka sehemu za jirani na sehemu zingine ikawa ni high school ambayo itawachukua wanafunzi. Niombe sana na niishauri Wizara kwamba kwenye maeneo tuliyonayo sasa wafikirie namna ya kuanzisha high school kwenye shule za zamani na hawa ndugu zetu wa Udhibiti Ubora waende wakaone vitu gani vinatakiwa kule badala ya kwenda tu na kuonesha mapungufu waoneshe vitu gani vinatakiwa vije Serikalini na hizo high school ziweze kuanzishwa.

Mwisho kabisa kwa sababu ya muda sasa tupo tunashughulikia maendeleo ya nchi yetu, tunapeleka umeme na maji vijijini, tunaanzisha viwanda kule vijijini, wataalamu wako wapi? Tunatakiwa kwenye majimbo yetu huu mpango uliokuwepo kwenye Wizara ya Elimu wa kuweka VETA kwenye maeneo mbalimbali hautoshi. Tunatakiwa sasa hivi kwa mahitaji tuliyonayo na ongezeko la wananchi kila jimbo liwe na VETA siyo kila wilaya. Kila Jimbo liwe na VETA kwa sababu watu wataendelea kuongezeka na mahitaji ya wataalamu yataendelea kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)