Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninapenda niende moja kwa moja kwenye hoja kwasababu ya muda, lakini naomba tu kwanza kwa kusema kwamba ninatangaza mapema kabisa kabla ya wakati kwamba nitashika shilingi kwenye mshahara wa Waziri wakati utakapofika kwasababu ya suala zima la RPL- Recognition of Prior Learning ambayo Wizara iliifuta na hatimaye inawanyima watu ambao hawakupata nafasi ya kupata elimu ya Sekondari kuweza kupata elimu ya chuo kikuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaielezea baadaye vizuri zaidi wakati wa kushika shilingi utakapofika, naomba nizungumzie suala zima ambalo ninaliona kama changamoto kwenye Taifa langu, changamoto namba moja ninayoiona ni utekelezaji wa mambo tunayozungumza ndani ya Bunge, tangu nimefika hapa nikisikia michango inayotolewa hapa ndani najiuliza tatizo lipo wapi? Hapa ndani kuna michango very constructive watu wanaongea vitu vya maana tatizo kubwa kabisa ni utekelezaji na ninaomba namuomba Mheshimiwa Waziri haya yanayozungumzwa hata kama sio yote akayafanyie kazi ni kufanya kazi peke yake itatutoa tulipo kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tusijekuwa Taifa la watu tunaozungumza watu tumeacha shughuli zetu kuja hapa tunaongea alafu hayafanyiki, haya yanayosemwa hapa yakifanyika nchi hii inabadilika. Tatizo kubwa kabisa ninaloliona katika nchi hii na ambalo ninaamini ni solution la matatizo ya nchi zote za Afrika ikiwemo Tanzania ni mabadiliko ya mind set ni mabadiliko ya akili za watu namna wanavyotazama mambo, shinda kubwa kabisa tuliyonayo bado hatujabadilika jinsi tunavyotazama mambo na namna tunavyofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumnukuu Dkt. Gwajima mara ya mwisho alipozungumza aliongea suala la human resource is far better above natural resources. Alisisitiza kwamba kinachohitajika katika nchi yoyote duniani ni watu kuwa na akili. Watu wakiwa na akili wataweza kutafsiri Liganga na Mchuchuma kuwa barabara, watu wakiwa na akili wanaweza kutafsiri utajiri walionao uweze kuwa elimu au huduma za afya, changamoto yetu ndiyo iko hapo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ya vyuo vikuu, shule za msingi inachangia kuweka akili kwenye vichwa vya watu. Kama siyo shule basi ni familia, kama siyo familia basi ni society tunazoishi ndani yake. Tunatia akili kwenye vichwa vya watu wetu ili waweze kutusaidia kutatua changamoto zetu. Ndiyo kazi ya shule, kazi ya vyuo vikuu ni kuweka akili na ufahamu kwenye vichwa vya watu ili waweze kuwa na uwezo wa kutatua changamoto zinazowazunguka.

Mheshimiwa Naibu Spika, tofauti na hapo hatutaweza kuhama mahali tulipo. Ndiyo maana leo nimesimama hapa kusema kwamba naona kuna tatizo kubwa sana kwenye mtaala wa elimu ya Tanzania. Hii ndiyo inasababisha nchi hii isiende mbele kwa kasi. Simaanishi kwamba hakuna kilichokwishafanyika, mambo mengi mazuri yamefanyika na yanaendelea kufanyika lakini mimi naomba mtaala huu ufumuliwe upya na kama ilivyoamuliwa uweze kupangwa upya ili uweze kupeleka Taifa letu mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano na mfano huu ni wangu mimi mwenyewe niliyesimama hapa. Mpaka mwaka 2017 nilikuwa darasa la saba, sikuwahi kusoma sekondari mahali popote kwenye nchi hii. Baadaye nikasema bora nirudi shule nikasome ili niweze kupata elimu ya kuniwezesha kufanya kazi zangu ofisini. Nikaenda TCU nikapeleka vitabu ambavyo nimeviandika nikawaonyesha walipoona vitabu vyangu wakasema unaweza kusoma chuo kikuu, nikapewa mtihani nikaufanya nikafaulu nikaingia degree ya kwanza Tumaini University, one of the best University in the country kutoka darasa la saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma pale miaka mitatu nimemaliza mwaka jana chuo kikuu, nina degree yangu safi, kutoka darasa la saba mpaka university na nimemaliza. Fuatilia pale utaambiwa nimemaliza na GPA 4.8 nikiwa best student katika chuo kile kutoka darasa la saba. Kilichonipeleka chuo kikuu mimi ni RPL lakini Mheshimiwa Waziri kaifuta. Kwa kuifuta anawanyima watu wengi sana fursa ya kupata elimu. Leo hii nimekaa hapa nasema kama RPL hairudishwi shilingi mimi sitaitoa, nataka kusema wazi hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme hapa mambo anayotakiwa kufanya Mheshimiwa Waziri kwa ajili ya elimu ya nchi yetu, naomba Waheshimiwa Wabunge hapo mlipo muandike neno UKUTA kwenye karatasi zenu, nataka kusema nini kifanyike kama solution.

Kwanza, lazima mtaala utakaokuja ufundishe ujasiriamali na uzalendo kwa taifa letu. Watoto wetu wafundishwe uzalendo kwa Taifa na ujasiriamali, itawasaidia sana baadaye hata wakikosa kazi waweze kuajiri wenzao. Mimi nimeajiri watu katika taifa hili na elimu yangu ndogo niliyokuwa nayo nimefanikiwa kuajiri watu ofisini na wanafanya kazi mpaka leo, jambo hilo lazima liwefundishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, U tumeizungumzia K ni Komputa, lazima watoto wetu wafundishwe komputa tangu wadogo. Haiwezekani Taifa hili hatufundishi watoto wetu elimu ya computer. Kuna shida gani tukifundisha coding kwa watoto wetu ili waweze kuwa na uwezo wa kutengeneza software na application mbalimbali? Taifa letu linaenda kwenye digital economy, dunia imebadilika sasa hivi digital economy ndiyo inayotawala dunia bila kuwapa watoto wetu elimu ya computer watawezaje kushindana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu ni U, nimesema UKUTA, U inayofuata hapo ni uamuzi either Kiswahili au Kiingereza basi. Hatuwezi kuwafundisha watoto wetu Kiswahili mpaka darasa la saba halafu form one tunaanza Kiingereza, ni uongo. Wabunge wote walioko hapa ndani anyooshe mkono Mbunge yeyote ambaye mtoto wake anasoma Kiswahili, tunawadanganya wananchi wetu. Sisi hapa wote watoto wetu wanasoma international schools na shule ambazo zinatumia Kiingereza kufundisha; wakulima wetu tunawafundisha Kiswahili akifika form one wanafundishwa Kiingereza watoto wana-fail masomo, hatuwezi kuendelea namna hiyo.

Mheshimiwa Spika, jambo la nne ni T ambayo ni tuamue, practical ni lazima iwe 70% na theory iwe 30% ili watoto wetu waweze kuwa-competent. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona muda haunitoshi lakini naomba niseme kwamba nitawasilisha mchango wangu kwa maandishi, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)