Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, Nikushukuru kwa dhati kabisa lakini niipongeze Wizara hii ya Katiba na Sheria ina Waziri mahiri kabisa, mbobezi wa masuala ya sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze mchango wangu kidogo nikumbushe jambo kama binadamu. Katika jambo ambalo ni gumu na linahitaji umakini mkubwa kwenye maamuzi ni suala la utoaji wa haki. Nadhani kama unafanya ranking, suala la utoaji wa haki linashika number one duniani; kwasababu ni jambo ambalo mungu ameamini mamlaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Sheria hizi mbili ya Utakatishaji wa Fedha na Uhujumu Uchumi, Bunge letu Tukufu lilitunga hizi sheria kwa nia njema kabisa; changamoto inayotukuta sasa ni utekelezaji wa sheria hizi. Naomba nikumbushe, wanadamu hapa duniani kwa Mujibu wa Biblia kizazi chetu ni cha nne, na uhai wetu hapa duniani ni miaka 70 hakuna anayeishi hapa milele.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sitaki kujua umri wa kila mmoja kila mmoja anaweza kutafakari aangalie miaka 70 a-minus umri wake sasa aone kipande alichobaki nacho duniani. Mtume Paulo kwa Habari ya Wakorinto aliwaeleza habari hii, aliwaeleza kwamba nikiitazama dunia ni ubatili mtupu. Hapa duniani tuwe na mali, fedha na kila kitu ni ubatili mtupu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze kwenye Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali. Ofisi hii kama ni chakula ndio mpishi, akikosea huyu hii haki pale haitendeki na akipatia haki inatendeka.

Mheshimiwa Naibu Spika kuna jambo moja la ajabu sana limetokea pale jimboni kwangu yamkini ni kweli wananchi wale wamefanya makosa, vifaa vyao matreka yamekutwa kwenye hifadhi na inasadikika kwamba wamekutwa wakifanya shughuli za kilimo kwenye hifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii wananchi hawa wapo mahabusu na kesi walizonazo ni Uhujumu Uchumi ni jambo la kushangaza kweli! Jambo la kushangaza kweli! Duniani kwamba kuna jambo linalohitaji umakini narudia kusema, ni jambo la utoaji wa haki. Kama mwanadamu akionewa, kama alitenda kosa mungu ametuumba lakini ndio guilty conscious yaani kuna adhabu ukipewa na umetenda nafsi yako hata kama hutasema inasema kweli nilikosea, nafsi inasema. Lakini ukionewa nafsi ina masikitiko na manung’uniko hakika aliyefanya makosa haya anachangamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, manung’uniko ya wanadamu mungu anasikia; leo hii kuna watoto, wake, Mheshimiwa Waziri, wake, watoto; hawasomi walikutwa tu kwenye hifadhi, matrekta hayo wanalima uhujumu uchumi, eeeh! Tumefika hapo! Kwa hiyo, ofisi ya DPP tusaidie, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali tusaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimekuwa kiongozi wa taasisi tena kubwa tu; ukiwa kiongozi wa Jiji la Dodoma tena nafasi ya Mkurugenzi ni nafasi kubwa ya juu. Sasa nataka kusema nini? Kuna umakini mkubwa unatakiwa kwenye ushauri wa wasaidizi wetu kama husomi documents aaah! Unaletelewa tu, kuna wengine wana compromise rushwa huko, wameshindwa kupata rushwa anasema ngoja nimkomeshe huyu anakuletea na wewe unakubali. Kwa hiyo kuna jambo la umakini sana Ofisi ya DPP tusaidie. Watanzania wanalalamika, watanzania wananung’unika hasa wananchi wa Jimbo la Mlimba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri na yeye binafsi alifuatilie, kama ikisadikika wananchi ni kweli wana makosa sheria ichukue mkondo wake. Mimi nishauri, Mheshimiwa Waziri ikikupendeza usiende tu kutembelea magereza nenda kalale! Usiende kutembelea kama visitor, nenda kalale, amka asubuhi utaona habari ya kule ndani. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna jambo gumu ni magereza. Ukimpeleka mwanadamu kule hana hatia kilio na masikitiko yake hutabaki salama. Kwa hiyo, naomba tuwe na umakini mkubwa katika suala zima la utoaji wa haki. Sheria hazina makosa, makosa ni namna ya utekelezaji wa sheria. Narudia kusema Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, tafadhali!

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye Mabaraza ya Ardhi. Yameelezwa hapa na Kamati imeshauri…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa hebu weka vizuri hiyo sehemu ili tuwasaidie hata upande wa Serikali inapokuja kujibu hoja. Katika maelezo yako nilikuwa najaribu kufuatilia nijue unaelekea wapi lakini umeeleza kwamba matrekta yamekutwa kwenye hifadhi.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Naam!

NAIBU SPIKA: Ni uhalisia kwamba yamekutwa huko?

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Sasa hayo ndiyo yanayoelezwa kwenye ile…

MBUNGE FULANI: Charge sheet.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Not charge sheet, nilipitia taarifa ya DPP, pamoja na mambo mengine kwenye facts alikuwa akitoa taarifa…

NAIBU SPIKA: Sawa.

Waheshimiwa Wabunge, ndiyo maana nilieleza mwanzoni yale mambo yaliyoko kule ukiyaleta hapa na sisi hatunayo unatupa wakati mgumu sana. Hata Serikali ukitaka ikujibu itakujibu kwenye hoja ipi? Kwa sababu katika maelezo yako wewe mwenyewe unayewatetea wale watu walioko ndani unasema hivi; wamekutwa na matrekta kule kwenye hifadhi. Sasa kama amekutwa na trekta kwenye hifadhi, lile trekta kwenye hifadhi linafanya nini?

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika.

NAIBU SPIKA: Ngoja, ngoja, nakuelezea hoja simaanishi uanze kujibizana. Ni hivi; ukiwa na jambo mahsusi waeleze wakalifuatilie. Ukilieleza wewe kwa namna ya kwamba na wewe unalifahamu kwa kadri Ofisi ya DPP inavyofahamu, Serikali inavyofahamu utapata wakati mgumu ndiyo maana hata hapa umeanza kusema ndicho walichoeleza maana yake ndicho walichoeleza Serikali lakini watu wako wewe walikutwa kule au hapana? Rekodi za Bunge hapa zitaonesha kwamba Mbunge umesema walikutwa na matrekta kule kwenye hifadhi.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Nimesema inasadikika.

NAIBU SPIKA: Mimi nilikuwa nasikiliza na huwa nasikiliza kila neno ndiyo maana nakueleza. Sasa mchango kama huo ukibaki hapa halafu wale wakaamua kwamba ni ushahidi Mbunge wenu mwenyewe alisema kwamba imekutwa kule. Kwa hiyo, ndiyo maana huwa najaribu kuonesha kwamba tuchangie kwa namna ambayo unaieleza hoja hiyo kwamba Serikali ikafuatilie. Taarifa za ziada waache wao watazipata na wewe kama Mbunge ni haki yako kabisa kwenda kwenye ofisi ya DPP, kwenda kwa Waziri kumueleza watu wangu wako kule hawajafanya kosa ama kwa namna yoyote ile unayotaka kuwatetetea. Ukiiweka humu kwa mtindo huo inaonekana kwamba katika taarifa rasmi na wewe unasema wamekutwa kule. Mimi nilikuwa nasikiliza kwa makini kabisa.

Nenda kwenye hoja yako ya pili, hii ya kwanza nakushauri uonane na DPP kwa sababu ofisi yake iko wazi Mheshimiwa Waziri pia yuko hapa. Karibu sana umalizie mchango wako.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa ufafanuzi na kama Hansard iko sawasawa nimetumia neno inasadikika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye eneo hili la Mabaraza ya Ardhi. Mengi yameelezwa hapa kwa habari ya Mabaraza ya Ardhi kwamba yawe sehemu ya Mahakama. Mimi nitakuwa na mchango wa tofauti kidogo, isingefaa Mabaraza haya yawe sehemu ya Mahakama isipokuwa Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria atusaidie kama kuna eneo kwa mujibu wa Kanuni kwenye ile sheria iliyoanzisha Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya liongezwe kabla hajatoa maamuzi Mwenyekiti wa Baraza ni lazima athibitishe kwamba amefika eneo la tukio.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto inayojitokeza kwenye haya Mabaraza kwenye utoaji wa hati unakuta Mwenyekiti wa Baraza anajifungia kwenye chumba anatoa maamuzi na mgogoro wa ardhi ni lazima ufike eneo la tukio, ndiyo changamoto hiyo tu. Kwa bahati mbaya ukienda Mahakama Kuu inayoshughulika na masuala ya ardhi, haina nafasi ya kukusanya ushahidi. Kwa hiyo, hata maamuzi ya Mahakama Kuu ukimueleza mlalamikaji au mlalamikiwa, mdai au mdaiwa akate rufaa Mahakama Kuu haina nafasi tena ya kukusanya ushahidi. Kwa hiyo, matokeo yake huyu mtu atendewe haki tu, hata rufaa bado ni changamoto tu. Kwa hiyo, msingi wa jambo lenyewe ni pale linaposikilizwa kwa mara ya kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na sasa hivi inakuwa ni utashi tu tena mlalamikaji anaambiwa nipe fedha ya kwenda site, Mtanzania wa kawaida hana. Sasa namna gani haki inatendeka, changamoto iko hapo. Kwa hiyo, ushauri wangu kwa mujibu wa Kanuni au sheria yenyewe kuwe na eneo linalosema kwamba kabla hajafanya maamuzi ya mwisho ahakikishe amefika eneo la tukio. Ndiyo essence ya migogoro ya ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nikushukuru kwa dhati na Mwenyezi Mungu akubariki sana. (Makofi)