Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. RESTITUTA T. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, nakushukuru. Kwanza kabisa, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai leo tupo hapa Bungeni tunachangia mada kwenye Wizara ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia mambo mawili matatu, lakini napenda kwanza nianze na suala la sheria ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu, zimetungwa muda mrefu, lakini nafikiri zilipokuwa zinatungwa kwa wakati ule zilikuwa zinahitajika kwa namna hiyo lakini sasa zinahitaji mabadiliko. Labda sababu ilizofanya zitungwe kwa wakati ule zilihitajika zitungwe kwa namna ile, lakini kwa sasa hivi zinahitaji mabadiliko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971. Ilipotungwa mwaka 1971 sheria hiyo ilikidhi mahitaji ya mwaka 1971 kwa kuonyesha kwamba mtoto wa kike anaweza akaolewa na miaka 15. Kwa sasa hivi watoto hawa wa kike wanasoma, wanakwenda shule, wanakwenda kozi mbalimbali na pia Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejenga mashule mengi mpaka vijijini.

Kwa hiyo basi, mahitaji ya wakati ule wa mwaka 1971 siyo mahitaji ya sasa hivi ya kuwepo na sheria hiyo ambayo ina kipengele hicho ambacho kinaweka tofauti ya mtoto wa kiume na mtoto wa kike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipengele cha 13 cha Sheria ya mwaka 1971 na Kipengele cha 17 kinatoa ile tofauti ya mtoto wa kike kuolewa na mtoto wa kiume. Sasa ili twende na usawa na kwa sababu tulimsikia pia Mheshimiwa Rais pale alisema kwamba akili za mtoto wa kike na wa kiume ni sawa, naomba kipengele hiki kibadilishwe umri wa kuoelewa wa mtoto wa kike uwe sawa na umri wa kuoa wa mtoto wa kiume. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni Sheria ya Mirathi ambayo kwa wakati ule mila zilikuwa zimeshamiri na zilikuwa zinafuatwa sana nchini kwetu Tanzania. Miaka ya 1963 wakati wa Uhuru, tulihitaji sana kufuata mila. Maamuzi mengi ya Mahakama yalikuwa yanafuata mila za eneo lile au mila za kabila ile, ndiyo maana kukaja na hiyo customary Law, sheria zikaletwa wale watawala wetu wakaona watahukumu zile sheria kufuatana na mila na desturi za eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hiyo Sheria ya Kimila ina section ambayo ina ubaguzi wa hali ya juu kwa mwanamke.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano nikichukua Section ya 27 ambayo inaelezea kwamba, mwanamke anaweza akatumia zile mali za familia, lakini hawezi kurithi mali za familia. Ijapokuwa Mheshimiwa aliyechangia aliyepita, alijaribu kuzielezea, lakini naomba nidadavue kidogo. Sheria hiyo inamfanya kwanza, mwanamke aji-feel ni inferior kwa mwanaume kwa sababu, katika ubongo wake anakuwa anaelewa kwamba mali hii anahitajika kuitumia tu, lakini sio kuirithi. Pia, sheria hii imekuwa ikiendeleza ule ubaguzi wa jinsia ya kike na ya kiume. Tunayo Tume ya Kurekebisha Sheria lakini haijachukulia ule mkazo thabiti wa kubadilisha sheria hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu, nimekuwepo hapa Bungeni miaka mitano iliyopita, niliona sheria ambazo zililetwa na tukazibadilisha humu Bungeni, lakini kwa sheria hizi mbili kumekuwa na kigugumizi cha aina fulani kuchelewa kuletwa kuja kubadilishwa. Kwa hiyo, niombe kwa sababu, hiyo Tume ya Kurekebisha Sheria ipo izifuatilie hizo sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, zipo pia sheria nyingine nyingi tu ambazo siwezi nikazitaja humu Bungeni lakini pia, either zinawanyima haki wananchi au vile vile labda zinatengeneza mazingira magumu kwa wananchi ambao wanakuwa hawawezi kupata haki zao vizuri. Kwa mfano, Sheria ya Usalama Barabarani nayo pia ina vipengele ambavyo mwananchi anakosa haki pale anapogongwa na gari au ajali inapotokea barabarani.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sasa kuzungumzia suala la Wanasheria wa Serikali. Wanasheria wa Serikali wanafanya kazi ngumu sana kuhakikisha kwamba, wanaitetea Serikali mahakamani. Naomba miundombinu yao iboreshwe, Wanasheria hawa wa Serikali wanakwenda mahakamani kutetea kesi za pesa nyingi, lakini unakuta anapotoka pale anakwenda kukaa kwenye nyumba ya kupanga na unakuta hata usafiri hana. Naomba waboreshewe makazi yao, lakini pia waboreshewe mishahara yao. Hawa watu wanatetea Serikali, lakini wanatetea kesi kubwa za madawa ya kulevya, za ugaidi hivyo wanahitaji kuwa na ulinzi na wanahitaji wafahamike wanakaa wapi ili angalau hata inapotokea jambo waweze kusaidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye mahakama zetu. Kama alivyosema hata Mwenyekiti wa Bajeti hapa, mahakama nyingi hasa zile Mahakama za Mwanzo zimechoka. Wizara ya Katiba na Sheria ichukue jukumu la kuziboresha hizi mahakama either kubomoa zile mahakama ambazo zilijengwa na watawala wetu na zijengwe mahakama ambazo tutasema sisi tumejenga. Litengwe fungu zijengwe mahakama, zinazohitajika kuboreshwa ziboreshwe. Vile vile miundombinu ya mahakama iboreshwe, kwa mfano, niliuliza swali hapa Bungeni Hakimu na Jaji anachukua jukumu la kusikiliza kesi, kukusanya ushahidi na pia anakuja kuandika ile hukumu yeye mwenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini isianzishwe division ya stenographer ili wawe pale mahakamani waweze kuandika yale mambo ambayo yanazungumzwa pale mahakamani. Hii itasaidia sana wananchi kupata hukumu zao mapema, sasa hivi kumekuwa na usumbufu kesi inahukumiwa leo tarehe 28, lakini hukumu mpaka iandikwe ni baada ya mwezi mmoja. Mwananchi anatembea anakanyaga kwenda kule mahakamani kufuatilia hukumu hii. Hii inaweza ikatengeneza mazingira ya rushwa kwa sababu, unaweza kusema kwamba, naomba uniandikie hukumu yangu ili niweze kwenda kufuatilia. Labda una kesi ya madai, sasa itabidi ufatilie ile hukumu, upate ile hukumu ili uweze ukatekeleze ile kesi yako ya madai. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliomba sana hiyo division wangejaribu kufikiria hii Wizara ya Katiba na Sheria ili kuwarahisishia kazi hawa Majaji na Mahakimu, wanafanya kazi kubwa sana. Mishahara yao iboreshwe, wanahukumu kesi nzito na wanafanya kazi ngumu sana pale mahakamani, vile vile wanakuwa na jukumu la kukaa kuanza kuandika ile hukumu ili kumpa mwananchi. Ukiangalia na sasa hivi tunakwenda kutafsiri hizi sheria kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili, basi jukumu lao la kazi litakuwa ni kubwa mno wanahitaji kuwa na hiyo division. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumza leo, ningependa kuwaambia wananchi lakini pia kujiambia sisi wenyewe kwamba, tuishi kwa kutii sheria. Tukiishi kwa kutii sheria nchi yetu itaendelea kuwa na amani lakini pia, sisi wenyewe tunakuwa na uhuru zaidi. Naamini kwamba, Polisi au mtu hawezi akapelekwa mahakamani na akawekwa rumande kwa muda mrefu kama hana kosa. Kwa hiyo, naomba tunapokwenda kusema kwamba, sheria kwa nini imefanya hivi, tujaribu pia na sisi kujielekeza kwamba, tuishi kwa kutii sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana kwamba, tusiishi kwa kufanya makosa ili tukitegemea kutafuta upenyo wa kutolewa kwenye lile kosa. Ukivunja sheria, sheria itakushughulikia, lakini pia sheria ndio inayoweza kudumisha amani nchini kwetu, vinginevyo humu barabarani Mwenyezi Mungu asingeweka sheria sisi tusingepita barabarani, wewe ungepita barabarani yaani mtu angekutemea mate, mtu angekugonga, kwa hiyo, sisi wenyewe tufuate sheria na tuziheshimu sheria zetu ili tusiweze kuvunja sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)