Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami kwa uchache niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Katiba na Sheria. Mchango wangu utajikita katika mafungu mawili tu, kwa maana ya Fungu la 59 na Fungu la 35.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Magereza yetu nchini kumekuwepo na changamoto kubwa ya mlundikano wa wafungwa pamoja na mahabusu. Mlundikano huu siyo kwamba Tanzania tuna wahalifu wengi sana, siyo kwamba Watanzania hatutekelezi sheria ambazo tunaelekezwa. Sababu kubwa sana ya milundikano ni kwa sababu kesi au tuseme mashauri yanachukua muda mrefu sana kufanyiwa upelelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mlundikano huu, wakati mwingine mahabusu yanazidiwa nguvu na kupelekea watoto wa chini ya miaka 18 kwenda kuungamanishwa au kuchanganywa katika Magereza au Mahabusu ya Watu Wazima. Inawezekana ikaonekana kwamba ni maajabu ninaposema kwamba inafika wakati watoto wa chini ya miaka 18 wanawekwa pamoja na mahabusu watu wazima, lakini hii inatokea kwa sababu kama mahabusu yamezidiwa na kuna watoto ambao wanapaswa kuingia mle ndani, automatically kwa sababu mabweni hayatoshi, tutajikuta watoto wetu wanaingizwa, wanachanganywa na watu wazima na mwisho wa siku wanajifunza tabia mbaya ambazo hawakuingia nazo katika yale Magereza au Mahabusu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu nyingine inayopelekea mlundikano mwingi katika Magereza haya ni kwa sababu kumekuwepo na kubambikiziwa kesi nyingi sana za jinai, yaani kila inapoitwa leo unasikia fulani ana kesi ya uhujumu uchumi. Ukisikia mtu fulani amepigana tu na mwenzake; ni mke na mume wamepigana nyumbani wakifikishwa tu kule Mahakamani unaambiwa umehujumu uchumi. Kwa sababu mambo haya yapo katika jamii na tunayaishi, ni wazi kabisa kwamba mlundikano hauwezi kumalizika katika Magereza na Mahabusu zetu. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu nyingine na mlundikano katika Magereza zetu inatokana na uwepo wa masharti magumu ya upatikanaji wa dhamana. Najaribu kuangalia au kuwaza huko vijijini, tuachie kwanza mjini; huko vijijini ambapo changamoto hizi za watu kubambikiwa kesi, hivi na vile, zimeshika kasi sana kuliko mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najaribu kuwaza kwamba ili mtuhumiwa aweze kudhaminiwa, anapaswa kuwa na watumishi wawili wa Serikali kwenda kumdhamini; na ikumbukwe kule vijijini ni ngumu sana, siyo rahisi sana kama mjini kwamba utapata Watumishi wa Umma, ni ngumu sana. Hata ukiwakuta hao wachache, hawana utayari wa moja kwa moja wa kudhamini watuhumiwa, kwa sababu unakuta mtu ametolewa Tanga anakwenda kufanya kazi huko Kagera kwetu huko ndani kabisa, hafahamiani na mtu, hana ushiriki mzuri wa moja kwa moja na wale watu, kwa hiyo, ni ngumu sana kumdhamini mtu ambaye hamfahamu vizuri kabisa. Hili linakuwa ni changamoto sana, nimesema zaidi sana vijijini kwa sababu mjini unaweza ukapata kidogo unafuu wa kumpata mdhamini kwa sababu Watumishi wa Umma wapo wengi ukilinganisha na vijijini. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiweka pembeni hilo la uhaba wa watumishi vijijini kwenda kuwadhamini watuhumiwa, sheria inamtaka mtuhumiwa aweke dhamana ya hati ya nyumba, kwa maana ya mali isiyohamishika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapowaambia watuhumiwa hao kwamba wanapaswa kuwa na hati ili waweze kujidhamini wakati tunafahamu kwamba hati hizi siyo tu vijijini, hata mijini ni less than fifty percent ya watu ambao wana hati za nyumba. Kwa hiyo, unaweza kuona mlolongo huu ambao nimeweza kuulezea, sababu hizi chache kati ya nyingi ambazo nimeweza kuzielezea zinazopelekea mlundikano mwingi katika Magereza yetu unatokana moja kwa moja na kuwepo kwa masharti magumu ya dhamana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu katika hili, Tume ya Kurekebisha Sheria ilete maboresho hapa Bungeni; kwanza, tupitishe sheria ya kuwepo na ukomo wa upelelezi wa hizi kesi ambazo zinachukua muda mrefu. Tukifanya hivyo, tutapunguza moja kwa moja mlundikano usiokuwa wa lazima katika Magereza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja sasa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)