Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 –Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia hoja ya Wizara ya Katiba na Sheria. Nianze kwa kuishukuru na kuipongeza sana Wizara kwa wasilisho zuri, nina imani kabisa kwamba mwalimu wangu, Mheshimiwa Prof. Kabudi, pamoja na timu yake, watakwenda vizuri katika kuiendesha Wizara hii ambayo inabeba sehemu kubwa sana ya maisha ya kila siku ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze pia Wizara ya Katiba na Sheria kwa ajili ya maboresho mbalimbali ambayo yamefanyika ya kutenganisha ile Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka. Naamini kabisa kwamba hatua hii italeta ufanisi mkubwa sana kwa sababu itakuwa imepunguza mzigo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze pia maboresho ya miundombinu ya Mahakama, hasa suala la majengo. Nadhani tumemaliza wakati ule sasa wa kuona kwamba Mahakama lazima zikae kwenye majengo machakavu na yaliyochoka, sasa yanajengwa majengo mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru hata katika Jimbo langu la Mwanga ujenzi wa Mahakama ya Wilaya umeanza, tunasubiri sasa kama ambavyo wenzetu wa Kamati ya Bajeti wameomba kwamba sasa Mahakama za Mwanzo ziboreshwe kwa sababu ndiyo zipo karibu zaidi na wananchi. Hivi sasa kwa vile Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wanapelekwa wale wenye shahada, naamini kabisa mambo sasa yatakwenda vizuri na Mawakili watakwenda, haki itatendeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado ziko changamoto na malalamiko mengi sana juu ya suala zima la utoaji haki, hasa katika maeneo haya ambayo yamekuwa yakilalamikiwa ya watu kuwa na kesi ambazo hazina dhamana na hizi kesi za utakatishaji fedha ambazo watu wengi wanazilalamikia. Mara nyingi malalamiko haya yanapotokea watu wanalaumu kwamba sheria ni mbovu lakini kuna wakati fulani Mheshimiwa Jaji Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Barnabas Samatta, aliwahi kusema kwamba tunahitaji zaidi Mahakama imara kuliko sheria kali. Sheria zinaweza zikawa kali sana lakini kama hatuna Mahakama ambayo iko thabiti ikatusumbua.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama yetu ni nzuri, ina uwezo mkubwa sana na mimi nimefanya nao kazi muda mrefu lakini hapa katikati Mahakama yetu imeingiwa na katatizo fulani, Mahakama yetu imeishiwa na wivu. Nasema hivyo kwa sababu wote waliosoma sheria wanafahamu iko kanuni moja inayotumika katika sheria inasema kwamba The Court must be jealous of its jurisdiction (Mahakama lazima iwe na wivu na mamlaka yake). Hata hivyo, hapa katikati Mahakama imekosa wivu na mamlaka yake, imeachia mamlaka yake ifanywe na watu wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakuta shauri linakuja Mahakamani, ile Sheria ya Utakatishaji Fedha inasema kabisa kwamba lazima kuwe na kosa la msingi halafu ndiyo la money laundering lifuate. Hata hivyo, shtaka la money laundering linakuja, Mahakama inaona kabisa kwamba hapa siyo sahihi na wale washtakiwa wanalia na kuomba kwamba jamani mbona hapa hakuna kesi ya money laundering, lakini zinaendelea na zinaendelea kuumiza watu. Ukweli wa mambo ni kwamba Mahakama hapa inatakiwa ikae kwenye sehemu yake ili twende mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 107A ya Katiba ya Jmahuri ya Muungano wa Tanzania, imeipa mamlaka Mahakama kuwa ndiyo yenye kauli ya mwisho pale ambapo kunakuwa na jambo lolote linalolalamikiwa. Sasa Mahakama irudi kwenye nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala hili kwa mfano la certificate ya DPP inayozuia dhamana. Mahakama inafahamu kabisa kwamba mkija Mahakamani watu wawili, mmoja ni DPP ambaye ni mshtaki na mshatakiwa, hawa watu wote wawili wako sawa mbele ya Mahakama ili iwaamulie shauri lao. Sasa mmoja anatoa wapi mamlaka ya kumzuia mwenzake asipate dhamana kwa certificate? Yule analalamika kwamba jamani huyu mwenzangu ni party, yaani amekuja mbele ya Mahakama kama mimi; anapata wapi yeye mamlaka ya kunizuia mimi dhamana kwa certificate? Sheria kweli inaweza ikawa inampa mamlaka lakini sheria inayompa mamlaka haizidi Katiba, Mahakama bado ina uwezo kabisa wa kuingilia kati na kusimama kwenye nafasi yake na kuweza kutenda haki. Sisemi kwamba lazima wapewe dhamana, lakini kama wananyimwa wanyimwe na Mahakama.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tadayo.

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, naam.

NAIBU SPIKA: Kaa kidogo.

Waheshimiwa Wabunge, napata changamoto kidogo na mchango wako maana unauzungumzia Mhimili wa Mahakama na kwamba kuna mambo mhimili ule haufanyi sawasawa. Sasa kwa taratibu tulizonazo humu ndani, Serikali huwa inasemwa kwa sababu inao hapa watu wa kuisemea, sasa tukiingia huko kwenye kuisema Mahakama kwa namna ambavyo unachangia, ni tofauti na kama ungekuwa unatoa ushauri kwamba kuna jambo fulani labda unaona liko hivi.

Kwa sababu ikiwa kuna watu ambao wameonewa na Mahakama wote tunafahamu utaratibu; unakata rufaa kulekule Mahakamani. Kwa sababu ukiileta kesi ambayo iko kule, mtu hakutendewa haki kule, ukaileta hapa Bungeni, hapa Bungeni siyo chombo ambacho Kikatiba kimewekwa kusikiliza mashauri ambayo Mahakama haijafanya sawasawa.

Sisi wenyewe tumeapa hapa kuilinda Katiba, kwa hiyo, kama ambavyo sisi Wabunge hatutegemewi huko nje tukaanze kujadiliwa kwa namna fulani hivi, ni vilevile mihimili mingine pia haiyumkiniki. Kama sheria ina shida, ni kazi yetu sisi kubadilisha sheria, siyo kazi ya Mahakama, ni kazi yetu sisi.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Tadayo, mwanasheria mbobezi kabisa, hebu jielekeze mchango wako kwa mipaka ile ambayo tunawekewa na Katiba yetu.

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa maelekezo yako na nayapokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kulizungumzia, nilishawahi kulitaja tena hapa Bungeni ni juu ya suala la Wizara mbili kuzungumza, Wizara ya Sheria na Wizara ya Ardhi ili Mabaraza yale ya Ardhi yaweze kurudi chini ya Mhimili wa Mahakama. Nasema hivyo kwa sababu ukienda Mahakama Kuu, pamoja na kwamba kuna Kitengo cha Ardhi ambacho kilianzishwa lakini pia Mahakama Kuu hii ya kawaida inapokea mashauri ya ardhi. Sasa tunapata changamoto kwenye zile Wilaya ambazo hazina Mabaraza ya Ardhi ambazo ni nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba Wizara hizi mbili zizungumze ili mashauri ya ardhi yaweze kusikilizwa kwenye Mahakama za kawaida kupunguza mzigo mkubwa wa mashauri ya ardhi ambayo ndiyo yanayoleta matatizo na changamoto nyingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikifika hapo naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja; ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)