Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia uhai na kutuwezesha kufikia mwisho wa mjadala wetu wa bajeti yetu hii wa ofisi yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, namshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maelekezo aliyoyatoa siku ya jana kuhusu masuala yanayohusu ofisi yangu wakati akilihutubia Bunge lako Tukufu. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa maelekezo yake tumeyapokea, tumeyaelewa, tutayazingatia na kuyafanyia kazi kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia uniruhusu niwashukuru kwa dhati Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kuunga mkono hoja niliyoiwasilisha jana katika Bunge lako Tukufu. Vilevile niwashukuru Waheshimiwa Wabunge ambao hawakuweza kuchangia kwa sababu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuhitimisha hoja, naomba kusisitiza kuwa ofisi yangu na taasisi zote zilizo chini yangu tumejipanga vizuri kutekeleza yale yote tunayoyapanga kuyafanyia kazi mwaka ujao wa fedha ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kukuza uchumi na ustawi wa Watanzania. Ninatambua umuhimu wa mchango wenu katika jitihada za kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025, lakini pia maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi iliyonadiwa katika uchaguzi uliopita, lakini pia Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/2022-2025/2026) na Hotuba ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyoitoa siku ya jana katika Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vita dhidi ya rushwa, tumeendelea kujidhatiti na kukabiliana na vitendo vya rushwa nchini, hali ambayo imeongeza nidhamu, uadilifu na matumizi bora ya madaraka na fedha za umma. Mafanikio ya juhudi zetu yamedhihirishwa na taasisi mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa. Kazi iliyo mbele yetu ni kuhifadhi mafanikio hayo na kuongeza juhudi ili kutokomeza rushwa na ufisadi nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufikia malengo hayo tumejipanga vyema kuandaa na kutekeleza mkakati mpya wa mapambano dhidi ya rushwa hapa nchini utakaozingatia changamoto zinazojitokeza sasa. Vilevile tunakusudia kuongeza ufahamu kwa wnanachi kuhusu masuala ya rushwa, kuboresha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa na kuimarisha utendaji wa Taasisi yetu hii ya TAKUKURU.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya wanyonge, ofisi yangu itaendelea kuimarisha utekelezaji wa Mpango wa MKURABITA ili manufaa yake yawafikie wananchi wengi zaidi. Wakati huo huo, tutaendelea kusimamia maadili na mwenendo wa watumishi wa umma, uwe ni mwema na uendane na miongozo mbalimbali ya watumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka ujao wa fedha, tutaendelea kuimarisha utendaji wa Mamlaka ya Serikali Mtandao ili kuboresha na kuimarisha usalama wa mifumo ya Serikali ili iweze kubadilisha taarifa tunazozipata. Matumaini yetu ni kuwa hatua hii itaongeza ufanisi wa utendaji kazi Serikalini na kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ofisi yangu itaendelea kutekeleza jukumu lake la kuimarisha utawala bora katika uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa kubuni sera, kanuni, na sheria za uendeshaji wa shughuli za utumishi wa umma na kuwajengea uwezo watumishi waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua hilo tutaendelea kulinda haki za watumishi wa umma kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo. Aidha, tutahakikisha kuwa ngazi za mishahara na madaraja ya watumishi yanapandishwa kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais siku ya jana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapenda kuona watumishi wanalipwa stahiki zao kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Stahiki za mtumishi ni haki yake mtumishi husika na siyo huruma, ni right, siyo privilege kama ambavyo nimekuwa nikisisitiza mara kwa mara. Tunataka kuondoa kero za kimaslahi zinazowakabili watumishi wa umma na uonevu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi nitaweka utaratibu wa kupokea malalamiko ya watumishi na nitachukua hatua kali za kinidhamu kwa wale wote watakaoshindwa kuwahudumia watumishi na wananchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ofisi yangu itaendelea kuratibu, kusimamia, na kukuza jitihada za Serikali, Serikali mtandao pamoja na kuhimiza utekelezaji wa sera, sheria, kanuni na viwango vya miongozo ya Serikali Mtandao kwa taasisi zote za umma hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kumaliza naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa kutoa maoni yao na pengine lazima nikiri kwamba maoni tumeyapokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo hoja chache ambazo pengine ningependa kuzitolea ufafanuzi. Kuna hoja hii ambayo imezungumzwa sana kuhusu Idadi ya Wakurugenzi saba, Ma-DAS pamoja na Ma-RAS ambao walikwenda kwenye kugombea kwenye nafasi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hii kama Wizara tumeipokea. Kama ambavyo nimesema Rais wetu amejikita katika kuhakikisha kwamba haki inatendeka kwa kila Mtanzania.

Kwa hiyo tutalichukua jambo hili tutakwenda kulifanyia kazi kama kutakuwa na mtumishi ambaye pengine alikuwa Mkurugenzi, alikuwa RAS au alikuwa DAS na alikwenda kugombea na kama alifuata taratibu zote ambazo zinatakiwa za kisheria na kikanuni zilizowekwa basi mtumishi yule kama haki yake itamtaka arejeshwe kazini, atarejeshwa kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe kwa sababu tunatambua kwamba wapo watumishi ambao tayari walirejeshwa kazini na jukumu la Serikali hii kuhakikisha kwamba inafanya kazi zake kuondosha double standard, kwa hiyo tutalichukua jambo hili, tutakwenda kulifanyia kazi kwa wale watumishi ambao wana haki ya kurejeshwa kazini watarejeshwa kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niwaombe na kama kuna Mbunge yeyote Mheshimiwa Mbunge yeyote anataarifa au watumishi hawa wapo basi wafike ofisini kwangu ili tuweze kupitia taarifa zao na yule mweye haki ya kurejeshwa kazini atarejeshwa kazini. Kwa sababu huu ndiyo msimamo wa Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha kwamba inatenda haki kwa wakati ili kila mmoja wetu aweze kupata haki zake stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kuhusu suala hili la upandishwaji wa madaraja limezungumzwa kwa kina sana. Naomba niseme kwamba tumeziagiza Taasisi na Maafisa Utumishi wote nchini kuhakikisha kwamba wanatuletea taarifa za watumishi wote katika maeneo yao. Tayari wizara yangu imekwishatenga nafasi za upandishwaji wa madaraja. Kwa sasa tunao watumishi zaidi ya 91,841 ambao wataigharimu Serikali zaidi ya shilingi 73,402,166.926. Kwa hiyo, tumejipanga kuhakikisha kwamba tunawapandisha madaraja watumishi kwa mikakati ambayo tumejiwekea sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na kuhusu hili suala la ajira mpya tayari Wizara yangu imejipanga kuhakikisha kwamba tutatoa ajira mpya 40,737 ambazo zitawagawinyika katika kada mbalimbali za utumishi wa umma. Tunazo ajira za elimu ambazo tunategemea kuzingataza hivi karibuni, ajira 9,667 na katika sekta ya afya tunategemea kutangaza ajira 10,467 na hivi karibuni tutatangaza ajira 2,116 za afya tukisubiri taarifa ya bajeti ambayo tutatangaza ajira zitakazopungua kutokana na hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika sekta ya kilimo tutatangaza ajira 1,046 kulingana na bajeti tutakayoipata. Katika sekta ya mifugo ajira 758, katika uvuvi 175, katika polisi 1,346 na katika magereza ni ajira 427. Jeshi la Zimamoto ni ajira 510, uhamiaji ajira 404, hospitali na mashirika ya kidini na hiari 1,486 na ajira nyinginezo ni 13,192. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niwatulize Waheshimiwa Wabunge watambue kwamba Serikali yao ya Awamu ya Sita imejipanga kuhakikisha kwamba tunakwenda kupunguza maeneo ambayo tunajua yanachangomoto nyingi za ajira katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mahusiano kati ya Ma-RC, Ma-DC, na Ma-DAS hili nimelizungumza kwa kina kabisa. Ni vyema kila mtumishi wa umma akatambua kwamba mtumishi yeyote wa umma hapa nchini yupo chini ya Wizara ya Ofisi yetu. Wizara hii ambayo inasimamia nidhamu za watumishi wote wa umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niwaombe Ma- RC, Ma-DC na Naibu Wakurugenzi na wale wote wanaoangukia kwenye Wizara hii kujikita katika kuhakikisha kwamba wanalinda viapo vyao ambavyo wamekula mbele ya Mheshimiwa Rais. Lakini pia nichukue fursa hii kuwataka viongozi wote wa Chuo cha Uongozi kujipanga vyema katika kuhakikisha kwamba wanatoa semina kwa viongozi wote wa umma ambao wanaangukia katika nafasi ya Naibu Wakurugenzi, Wakurugenzi, Ma-RC, Ma-DC na viongozi wengine wote wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hili suala la utolewaji wa nyaraka, suala hili nimelizungumza kwa kina. Ofisi yangu itakwenda kujipanga, tutakwenda kupitia nyaraka zote, zile nyaraka ambazo tunaona zimetolewa na zinakiuka sheria nyaraka hizo zote hizo tutazifuta. Nataka niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge, lakini naamini kwa kipindi ambacho nimekaa katika ofisi hii binafsi sijaona nyaraka ambayo imetolewa imekiuka sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama kuna taarifa ya nyaraka yoyote ambayo imetolewa na inakiuka sheria tutakwenda kujipanga na kuhakikisha kwamba nyaraka hiyo tunaiondosha na kuifuta ili sasa kwa namna ile ile ya misingi ya tasfiri ya sheria tunakuwa na Katiba, tuna sheria, tuna kanuni pamoja na miongozo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafuu ya muda ninaomba sasa pamoja na michango mizuri ya Waheshimiwa Wabunge iliyotolewa ninaomba kutoa hoja. Ahsante. (Makofi)

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa naibu Spika, naafiki. (Makofi)