Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Florent Laurent Kyombo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkenge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa nafasi, niungane na wenzangu kuwapongeza Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa na Mheshimiwa Deo Ndejembi, kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais.

Naomba niongee machache kwa sababu ya muda, lakini pia niwaombe Mheshimiwa Waziri na Naibu wake naona ni vijana ambao wana kesho nyingi njema na hivyo wakichukua fursa hii ya kupata ushauri na kuiboresha Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora basi tutakuwa na watumishi wenye hali ya kazi na hivyo malengo mahususi ya nchi yetu yataweza kufikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua nitatoa case study katika local government na najua mwongozo ambao unasimamia maadili ya utumishi wa umma ni Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2009 yaani Standing Order of 2009.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujikita kwenye fursa sawa kwa watumishi wote. Halmashauri inazo Idara 18 baada ya moja ambayo ilikuwa Idara ya Maji kutolewa na kuanzishwa Taasisi ya RUWASA. Lakini katika maeneo hayo watumishi wote hawahudumiwi sawa na kanuni za utumishi wa umma. tunaona katika OC inayopelekwa katika Halmashauri hizo suala la leave, suala la likizo zime- concentrate katika baadhi ya idara na idara hizo ni Idara ya Elimu ya Msingi, Elimu ya Sekondari na Afya na huko hazitoshi lakini idara zote zilizobaki hakuna mtumishi anayeweza kukuambia kwamba nilishawahi kulipwa hela ya likizo, hakuna mtumishi anayeweza kukuambia kwamba nilishawahi kulipwa hela ya kusafirisha mizigo kurudi kwetu kutoka kwenye OC. Na idara hizo nyingine OC inaenda shilingi milioni moja Idara ya Kilimo, Idara ya Mifugo, Idara ya Mazingira, Idara ya Mipango. Niombe Wizara iangalie kwa sababu yeye ndio baba, mama wa watumishi wote na Standing Order sasa ya mwaka 2009 iweze kuzingatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni suala la OPRAS, mimi nimshukuru Mheshimiwa Rais jana ni kama alifungua kifua changu na kunifanya nipumue vizuri baada ya kuiona pia OPRAS ni tathmini ya utendaji kazi ya watumishi kwamba haiko vizuri inatakiwa iboreshwa. Najua kutakuwa na forum mahsusi kwa ajili ya kuchangia vizuri, lakini niombe kushauri tunazo taasisi za Serikali, mimi nishawahi kuwa mtumishi wa TFDA leo ni TMDA iliboresha ile OPRAS tukaingia kwenye TASA - TFDA Staff Appraisal ambayo ilikuwa kwa kweli inatumika hata kumpata mfanyakazi bora wa Mei Mosi anapatikana kupitia hiyo. Lakini leo OPRAS haipo na Mei Mosi mtumishi bora anapatikana kwa zamu, kwamba tupeane zamu, sijui ni nani maaarufu zaidi naomba kwa hiyo niombe sana iweze kuboreshwa kama Mheshimiwa Rais alivyoshauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nilitaka kushauri kwenye suala la uhamisho. Tumekuwa na utaratibu wa kuhamisha watumishi na tumepewa maelekezo kwamba watumishi wahame kadri inavyowezekana, lakini niombe chain of command, chain ya mawasiliano ya viongozi wetu izingatiwe, yule ambaye tumemkasimu kusimamia watumishi katika eneo lake basi m-consult hata kidogo, leo unakuta Halmashauri imetumia fedha kumuhamisha mwalimu kwa gharama wa sayansi, amefika hapo barua inatoka Utumishi au inatoka TAMISEMI bila taarifa Mkurugenzi kujua. Tunaiweka Serikali katika gharama kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niombe chain of command mamlaka haipingwi, lakini wasiliana na wale wanaokusaidia kusimamia watumishi kule chini. mtaongea lugha moja na tunajua kwamba kila mtumishi atapata haki yake ya kuhama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho niungane na hoja ya Mheshimiwa Husna Sekiboko na Mheshimiwa Ndulane, ni watumishi ambao walikuwa watumishi wakaenda kugombea katika nafasi za siasa. Katika eneo hili lilikuwa na ukakasi na grievance nyingi sana, mimi niwaombe Wizara hii ilifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna post nyingine ni political post akimaliza anapewa gratuity yake, anafungasha, anaondoka, lakini post nyingine kama walivyosema za Wakurugenzi na watumishi wengine zilikuwa ni za kiutumishi, wamepewa ajira, wamethibitiswa kazini na walipoondoka walitakiwa sasa wapangiwe vituo vingine na hii tumeiona, hata kipindi cha nyuma wapo Ma-RAS ambao walitolewa kazini, wapo Wakurugenzi walitolewa kazini, lakini walipangiwa RS, wapo wanafanya kazi na taasisi nyingine za Serikali wengine wameletwa katika Wizara zenu. Kwa hiyo, tuombe hao wenzetu ambao wapo mtaani, wanazurura hawajui la kufanya, niombe sasa Wizara ifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)