Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kutoa pole sana kwa familia ya aliyekuwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, ambaye alifariki dunia tarehe 17 ya mwezi wa Tatu. Natoa pole nyingi sana kwa familia, pole nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan; pole sana kwa Waziri wetu Mkuu; viongozi wengine wote na wananchi wote kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Jemedari, mwanamke shupavu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwenyezi Mungu amjalie kila kheri ampe kila namna iwezekanayo ili aweze kusimama imara katika uongozi mzima wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, leo nina mambo matatu tu ya kuchangia katika Mpango huu wa Maendeleo. Nianze na suala nzima la Sekta ya Kilimo. Mara nyingi sana nimekuwa nikisimama hapa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nazungumzia sana suala la kilimo hasa tunapokwenda kufungamanisha kilimo na masuala mazima ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri shahiri, pasipo shaka yoyote, bila kuimarisha Sekta ya Kilimo hatutaweza kufikia malengo tunayokusudia katika mpango mzima wa kukuza uchumi katika nchi yetu ya Tanzania. Hivyo basi, naomba Serikali yangu sikivu kwamba mpango huu wa kilimo uende sambamba na kuhakikisha kwamba masuala mazima ya mbegu kuelekea katika uwekezaji kwenye kilimo kuwe na mpango Madhubuti, yaanzishwe mashamba ambayo yataweza kuandaa mbegu nzuri ambazo zitauzwa kwenye maeneo mbalimbali kwa bei nafuu ili uwekezaji huu ufanyike na uwe na tija kwa Taifa na pia katika kuinua masuala mazima ya kiuchumi katika nchi yetu na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, suala la kilimo ni lazima pia liambatane na masuala mazima ya masoko. Masoko imekuwa ni tatizo. Uwekezaji ni mkubwa sana unaofanywa na wananchi wakitumia nguvu nyingi na wakati mwingine wananchi wanafanya kazi kwa kutumia mikono yao, hawana hata zana za kilimo zilizo bora ili kuweza kuwezesha Sekta hii ya Kilimo na uwekezaji wao.

Mheshimiwa Spika, pia kumekuwa na tatizo la masoko, masoko ni tatizo. Mkulima alime mwenyewe na atafute soko mwenyewe. Naomba sasa Serikali yangu kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara wajipange vizuri kuhakikisha kwamba wanatafuta masoko ili wawekezaji wetu kwenye masuala mazima ya kilimo wafanye uwekezaji wenye tija.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kumekuwa na mikoa ambayo imekuwa ikizalisha sana mazao ya nafaka ambayo kimsingi inasaidia sana katika kuweka uimara na kuhakikisha kwamba tunakuwa na akiba nzuri ya chakula. Unapoitaja mikoa hiyo, huwezi kuacha kuutaja Mkoa wa Ruvuma ambao umeshika nafasi ya kwanza mara nne mfululuzo katika uzalishaji wa mazao ya nafaka, ukifuatiwa na Mkoa wa Songwe, unafuatiwa na Mkoa wa Rukwa na mikoa mingine.

Mheshimiwa Spika, mikoa hii inafanya vizuri sana. Sasa endapo kama mikoa hii inafanya vizuri, itoshe tu leo niongee mbele yako dhidi ya Waziri wa Fedha aweze kutoa tunu kwa mikoa hiyo kwa kupeleka Benki ya Kilimo. Benki ya Kilimo hiyo itafanya uwekezaji maeneo hayo ili waweze kuwakopesha. Pia iende sambamba na mikoa mingine inayolima pamba, Mkoa wa Dodoma unaolima zabibu na maeneo mengine yote ambayo katika nchi yetu yanafanya vizuri waweze kwenda kupelekewa Benki ya Kilimo ili iweze kuwasaidia wananchi katika kuwainua zaidi kwa sababu wananchi bado wanauhitaji, lakini wanapata wapi mitaji ili wawekeze vizuri zaidi kwenye kilimo. Unakuta Benki ya Kilimo ipo pale Dar es Salaam inashangaa shangaa tu, nani anayelima pale Dar es Salaam. Ni vizuri basi Waziri wa Kilimo apeleke Benki hizi kwenye maeneo husika yanayofanya vizuri ili weweze kuwainua kiuchumi na waweze kufanya uwekezaji mzuri katika masuala mazima ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, sasa naenda kwenye suala la barabara; tumekuwa tukizungumza sana kuhusiana na masuala ya barabara. Lengo ni kuhakikisha kwamba maeneo yote ya nchi yetu ya Tanzania yanafunguliwa na barabara zetu zikiwemo barabara za kawaida ambazo zinasimamiwa na TARURA, lakini pia zikiwepo barabara ambazo zinasimamiwa na TANROADS ili kuweza kurahisisha uchukuzi na kurahisha uzalishaji ambao utapelekea ukuaji wa kasi wa uchumi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, sasa hapa naomba niende moja kwa moja kwenye suala la PPP (Public Private Partnership). Suala hili na wewe umelidokeza hapo, ni jambo zuri kabisa, Serikali isijilimbikizie miradi mikubwa kuhenyeka nayo, kutabika nayo, badala yake wafungue fursa ili taasisi na mashirika mbalimbali na sekta binafsi zinazoweza kuja kuwekeza basi zije kuwekeza katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Sheria Na. 18 ambayo ilifanyiwa marekebisho katika Bunge lako Tukufu hili mwaka 2010, sheria hii haijamnufaisha mwananchi wa Tanzania, bado sheria hii haijamnufaisha mwanaumma wa Tanzania. Nasema hivi kwa sababu sheria imefanyiwa marekebisho kwamba sekta binafsi sasa ziungane na Serikali ili kuweza kutanua wigo na waweze kuwekeza kwa maslahi ya Watanzania, lakini bado sheria hii haijafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, unakumbuka tarehe sita Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amelihutubia Taifa akiwa anaapisha watendaji mbalimbali pale Ikulu, ameeleza Mama samia na ameonesha dhahiri pasipo shaka kwamba anahitaji sekta binafsi zije ziwekeze katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, sasa ni wajibu wa viongozi mbalimbali wanaohusika katika sehemu mbalimbali kuweza kutoa ushirikiano ili wawekezaji hawa waweze kuja na kuwekeza ili sheria hii Na. 18 iliyorekebishwa mwaka 2010 iweze kufanya kazi na kuleta tija kwa Watanzania ambayo itasababisha ukuaji wa uchumi. Wawekezaji hao watalipa kodi, lakini itaongeza ajira na pia itainua uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, utengenezaji wa barabara; nakumbuka mwaka 2017 ulinipa fursa ya kwenda Nchi ya China kikazi kwa majukumu ambayo ulitupa sisi kama Wabunge wako, tulikuwa Wabunge 20. Nilijifunza jambo kubwa sana na Mungu akubariki sana wakati mwingine sasa naomba unipe fursa hiyo kwa nchi nyingine, nitakuja na mchango hapa ndani ya Bunge. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, jambo nililiona China mwaka 2017, leo hii ninachangia ndani ya Bunge kwamba niliona kuna barabara ambazo zimetengenezwa kwa mtindo wa PPP ambazo zimekuwa zikisaidia sana katika Nchi ya China ambayo miundombinu ya barabara imezagaa kila mahali. Vile vile imekuwa ikisaidia pato la nchi linaendelea kukua na wananchi walioko wanaendelea kunufaika na kurahisha shughuli zao za kuendeleza uchumi.

Mheshimiwa Spika, hukunipeleka bure kule, nimepata hiyo exposure na leo nasimama ndani ya Bunge lako Tukufu kuweza kuchangia hilo na kwamba kuona kwa macho.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani kwamba….

SPIKA: Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Msongozi anasema kwamba fursa ya Waheshimiwa kutembeatembea kidogo ina faida. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Jacqueline malizia dakika zako.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, sasa hili suala la PPP kwenye barabara zetu tungeweza kuchukua watu wa NSSF wakatengeneza barabara hapa na zikawa zinalipiwa, Serikali inapata mapato yake, NSSF watapata mapato yake na pia wananchi watapata ajira na nchi yetu itaendelea kiuchumi. Hali kadhalika tunahangaika hapa kuzungumzia barabara za kufungua baina ya nchi na nchi, kwa mfano kuna barabara yetu ya Likuyufusi - Mkenda ambayo inaungana na Nchi ya Mozambique. Barabara hii ikitengenezwa kwa mtindo wa PPP itasaidia sana kurahisisha kufungua uchumi huo.

Mheshimiwa Spika, pia kuna barabara ambayo ipo Kakonko barabara hiyo ina urefu wa kilimita 40, inatoka Kakonko halafu inakwenda Muhange. Kwa hiyo hii barabara ingeweza kufungua na mahali pale nimekwenda wakati wa kampeni, nimekuta wananchi wa eneo hilo wana soko kubwa sana pale. Kwa hiyo ikiunganishwa hii barabara na wananchi wale wakawa wana zile movements za kulipia hiyo barabara, ni wazi kwamba Serikali itaongeza mapato makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye suala la tatu na la mwisho, sasa nizungumzie uwezeshaji wanawake kiuchumi, mama ni mama tu, kwa kweli ukimwezesha mwanamke umewezesha familia na umewezesha jamii kwa nzima kwa ujumla. Wanawake wamekuwa wakiwezeshwa kupitia halmashauri zetu mkopo wa asilimia 10 kwa mgawanyo wa 4, 4, 2. Halmashauri zingine hazina uwezo wa kuwakopesha wanawake hawa wakaweza kufanya uwekezaji wenye tija kwenye maeneo yao. Sasa niiombe Serikali yangu tukufu iweke utaratibu mzuri ambao utasaidia wanawake wengi kukopeshwa wakiwepo wanawake wa Jimbo la Kongwa, kule Kongwa wanawake wale wakiwezeshwa vizuri kwa vyovyote vile hata familia zao zitaimarika zitaboresheka na mambo yatakwenda barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho suala la mifugo,

SPIKA: Ahsante, muda umekwisha.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.