Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa kuwa mchangiaji wa kwanza kwa siku ya leo. Nina kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na sisi sote Wabunge ambao tumepata fursa ya kuwepo leo mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Bajeti. Kwa hiyo, nimepata fursa ya kutosha katika kuchangia mawazo ambayo yameboresha Mpango. Hata hivyo, naomba niendelee kujazia katika baadhi ya maeneo ambayo naamini Serikali itakuwa tayari kuendelea kuya-accommodate ili Mpango wetu uwe ni ambao utaleta tija kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nina kila sababu ya kuipongeza Serikali yetu, imefanya kazi kubwa na nzuri sana katika suala zima la miundombinu. Hata hivyo, tunapofanya kazi nzuri tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba kasi ileile tuliyokuwanayo ya kujenga miundombinu inaendelea na inaendelezwa kwa kasi kubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, nina kila sababu ya kuipongeza Serikali yetu imefanya kazi kubwa nzuri sana katika suala zima la Miundombinu; lakini tunapofanya kazi nzuri kuna wajibu wa kuhakikisha kwamba kasi ile ile tuliyokuwa nayo ya kujenga miundombinu inaendelea na inaendelezwa kwa kasi kubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, tumeweza kuunganisha karibu mikao yote Tanzania, imebaki Mikoa michache, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba kasi ya kuunganisha miundombinu kwa maana ya barabara inaenea katika Mikoa yote, maeneo ambayo yamebaki na twende kuunganisha Wilaya zote.

Mheshimiwa Spika, iko haja ya kwenda kutazama barabara za kimkakati na hasa zile barabara ambazo zinaunganisha nchi yetu na nchi Jirani. Kwa mfano barabara iliyoko katika Jimbo langu la Kalambo kutoka Matai kwenda Katesha Boda ni miongoni mwa Barabara muhimu sana, ni vizuri Serikali ikatilia maanani ujenzi wa barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuna barabara ambayo inaunganisha nchi yetu na nchi ya Mozambique iko Ruvuma kule maarufu kwa jina la Likuyufusi Mkenda, ni vizuri kabisa Serikali ikahakikisha katika mpango barabara hii ikawekwa ili fursa ya kiuchumi kama nchi tuweze kuipata kwa majirani zetu wa Mozambique.

Mheshimiwa Spika, kama haitoshi kwenye suala la barabara kazi nzuri ambayo inafanywa na Serikali katika ujenzi wa Reli yetu, tena ya Standard Gage, ni kazi ya kutiliwa mfano ya kupigiwa mfano, ni kazi ambayo imeanzwa, si vizuri tukaishia katika maeneo hayo; ni vizuri sasa tukaanza kufikiria networking kwa Taifa letu kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, tunayo Reli ya kutoka Dar es Salaam kwenda mpaka Zambia Kapiri Mposhi, lakini reli ile imejengwa kwa kiwango cha Standard Gauge.

Mheshimiwa Spika, tutumie fursa ya ujenzi ambao tumeianza kwenda mpaka Mwanza na Kigoma. Tutumie fursa ya Reli ya TAZARA. Kwanza tuondoe makandokando yaliyopo katika uendeshaji, kwa maana ya Management, lakini ni vizuri pia tukaendelea kuongea na wenzetu wa Zambia. Sisi tuna eneo kubwa, na hili eneo ambalo tunalo sasa tuanze kutazama uwezekano wa kuanzisha vipande vingine kutoka Tunduma pale kwenda mpaka Kasanga Port ili tuweze kutumia fursa ya kuunganisha na DRC kwa ajili ya mizigo yetu; wanahitaji sana mizigo kutoka kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Lakini kama hiyo haitoshi, hata ukitazama kuna hii habari ya Mtwara Corridor suala limeongelewa muda mrefu sana. Ifike mahali katika mpango wetu tujue kwamba tunataka network kwa nchi yetu ili kusiwe na sehemu hata moja katika nchi hii ambayo inakuwa disadvantage. Ni vizuri na ni wakati muafaka kwa Serikali kuhakikisha kwamba eneo hilo nalo reli inajengwa ili tuweze kutumia fursa ya kuunganisha na Lake Nyasa pale.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tuna mradi wetu ambao umeongelewa muda mrefu kuhusu Liganga na Mchuchuma tukiwa na uhakika wa usafiri wa uhakika kwenda kufika kule hakika nchi yetu tutakuwa tumefungua kila eneo, ni vizuri Mheshimiwa Waziri ukatilia maanani masuala haya ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie kuhusiana na suala zima la Afya. Naipongeza Serikali imefanya kazi nzuri sana katika kujenga vituo vya afya vingi vya kutosha. Sasa tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba sasa wataalamu na vifaa vinakuwepo vya kutosha ili hicho ambacho kimekusudiwa kiweze kutoa matunda kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na wewe ni shuhuda, umekuwa ukilisema mara nyingi kwamba tusipokuwa na Bima kwa watanzania hawa hakika juu ya Mwananchi kupata matibabu kuanzia Januari mpaka Disemba itakuwa kwenye mashaka.

Mheshimiwa Spika, ni wakati muafaka sasa wa kuja na mpango na ukamilike haraka juu ya universal health coverage kwa watanzania hawa, ndio namna ambayo itatuhakikishia afya kwa watu wetu bila kujali kwamba mtu ana kipato au hana. Kwa sababu katika hali ya kawaida ugonjwa hauna muda, kwamba mtu atajiandaa na kuwa fedha ambayo ameitenga kwamba nikiugua nitakwenda kuitumia hii. Window pekee ambayo itatusaidia ni universal health coverage kwa Watanzania, tuanze sasa. Mheshimiwa Waziri wa Afya unasikia, ndicho kipimo chako katika kuhakikisha kwamba Watanzania wote watakukumbuka kwa kazi nzuri ambayo utakuwa umewafanyia kwa kuwaanzishia mfuko na ukamilike.

Mheshimiwa Spika, alianza Waziri aliyetangulia na eneo alilofika sasa ni wajibu wako kuhakikisha kwa maana wewe unaenda kumalizia kipande ambacho kilianzishwa na mwenzako.

Mheshimiwa Spika, naomba pia nichangie kuhusiana na suala zima upande wa Kilimo. Safari hii tumepata wake- up call, kwamba uhitaji wa mafuta ya kula ni jambo ambalo halibishaniwi, kila mtu atahitaji mafuta ya kula kinachotofautia ni kiasi gani na wingi ndicho mtu atatumia lakini hakuna mtu ambaye atasema hata tumia mafuta ya kula. Na sisi kama Taifa tumekuwa tukitumia fedha nyingi sana za kigeni kuagiza mafuta kutoka nje ambayo wakati mwingine hatuna hata uhakika na juu ya ubora wake.

Mheshimiwa Spika, nilishawahi kulisema hata siku moja hapa; kama kuna mambo ambayo enzi zile yalifanywa vizuri na the so called SIDO ilikuwa ni pamoja na uanzishwaji wa viwanda kwa ajili ya kukamua mafuta ya alizeti na mafuta ya karanga. Hivyo viwanda na mawazo hayo ni wakati muafaka kwa kutoa hamasa kwa watu wetu kuhakikisha kwamba mbegu zilizo bora ambazo zitakuwa zinatoa mafuta ya kutosha (extraction rate) iliyo nzuri ebu tuhimize kila kaya; kama ambavyo ilitokea kipindi Fulani. Kwamba ilikuwa kila familia ijitosheleze katika chakula. Sasa ifike pahali ambapo hamasa itolewe kila familia walau kila mwananchi akawa na hata nusu heka akalima alizeti, ama karanga, kulingana na hali ya mahali Fulani. Ifike pahali ambapo tujitosheleze kwa mafuta ambayo tunazalisha sisi wenyewe. Kwanza tuna uhakika na ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilishawahi kusema siku nyingine hapa, hivi ile super G ambayo tulikuwa tunaiona imeenda wapi? Nini ambacho kilitokea Tanbond imeenda wapi? Nini ambacho kimetokea? Yale mafuta ambayo tunayapata kutokana na mbegu za pamba yameenda wapi? Nini kimetokea? Kama Taifa tuna kila sababu ya kujifanyia tathmini sehemu ambazo tumekosea turudi katika mstari ili wananchi wetu wawe na uhakika wa mafuta yaliyo bora, lakini pia ni chanzo kizuri cha mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe, kwa ujumla wake kazi ambayo imefanyika ni nzuri. Ni wajibu wetu sisi Watanzania tukahakikisha kwamba tunakuwa na spirit ya kupenda kufanya kazi; na ubunifu tukiupata kwa mtu tuulee, si kwamba inakuwa kama vile anafanya mtu kwa ajili ya manufaa ya Taifa lakini hatumuungi mkono kwasababu kama vile hatunufaiki wote.

Mheshimiwa spika, nakushukuru na Mungu akubariki sana. (Makofi)