Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru kwa kupata nafasi hii kwa ajili ya kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Mwaka Mmoja na Miaka mitano. Kwa kuwa mimi ni mfuasi sana wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli, kwa uzalendo wake napenda niendelee kumpongeza kwa kazi nzuri anayofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwakumbushe Watanzania na wenzangu waliomo humu kwamba baba yetu huyu amefanya kazi kubwa. Wakati anaingia mwaka 2015 nilimsikia akisema ninyi TANESCO acheni mchezo, nafahamu huu mgao wa umeme mnafanya biashara. Mnafungulia maji ili watu waweze kuuza majenereta halafu wauze mafuta. Alivyokemea, kweli sisi tuliokuwa tunaishi Mbeya na Dar es Salaam, taabu ya umeme tuliyokuwa tunapata na kelele za majenereta ziliisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuendelee kumtia moyo. Hao wanaombeza, waendelee kubeza, lakini kwa sababu hata Mungu aliyetuumba wengine tunamkataa, tunampenda shetani. Kwa hiyo, ni jambo la kawaida. Kwa hiyo, namtia moyo aendelee hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mpenzi wa kilimo, siku ile kwenye hoja nilizungumza kidogo sikumaliza. Wakati tukiwa kwenye mpango kazi wa Wizara, mimi pia kama Mjumbe wa Kamati tulizungumza baadhi ya mambo. Moja ambalo linanigusa sana ni kuona Serikali sasa inakwenda kuwekeza kwenye suala la maabara za utafiti wa udongo. Ni muhimu sana. Wajerumani walifanya portioning ya nchi hii, wakasema hapa tutalima pareto, hapa tutalima kahawa, kwa sababu walipima udongo katika nchi hii na wakaweza kutoa mawazo yao kwamba tukilima hiki hapa tutafanikiwa. Najua ni nia ya Serikali kuhakikisha kwamba tunainua kilimo, lakini naona kwamba tuwekeze kwenye maabara za utafiti wa udongo, ni muhimu sana kwa sababu tutatoa mwongozo na tutaweza kuelekeza watu walime namna gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine pia upande wa mifugo, tumekuwa tuna shida ya chanjo. Chanjo nyingi ambazo tunazileta nchini zinatengenezwa kutoka katika nchi mbalimbali na hizi chanjo wanasema kwamba zinatibu magonjwa mengi na magonjwa mengine ambayo zinatibu hapa Tanzania hayapo. Sasa ningependa kuona Serikali inashirikiana na hiki Kiwanda cha Health Bioscience kuona kwamba kinakamilika kwa haraka, kama kuna vikwazo vyovyote vya kikodi au vya kivibali, basi viondolewe ili kiwanda hiki kianze kutengeneza chanjo hapa hapa nchini kwa sababu tutatengeneza chanjo zinazolingana na mazingira yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo, tutaweza sasa kuzalisha mazao ya wanyama ambayo tunaweza kuyauza hata Nchi za Ulaya pamoja na Nchi za SADC, kwa sasa tunashindwa kwa sababu ya ubora wa mazao yetu. Kama hizi chanjo tutazizalisha hapa, tutadhibiti magonjwa na tutaweza kuongeza tija kwenye mifugo. Najua muda utafika, baba yetu akishamaliza hii miradi ya umeme tutakwenda kumwomba fedha za kimkakati ili tuwekeze kwenye utafiti wa chanjo, kwenye maabara, kwenye mifugo pamoja na mazao, najua haya mambo yatakwenda vizuri, kwa sababu haya mambo ni ya kupanga tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tumesema kwamba utalii, ecology kule Arusha inaharibika. Sasa naona sasa ni wakati muafaka tuweze kufungua milango ya utalii wa Nyanda za Juu Kusini. Baba yetu Magufuli pale Iringa ametuletea pesa, tutajenga Kituo cha Utalii (Tourism Hub). Sasa ili haya mambo yaende vizuri tungehakikisha kwamba hizi barabara, kwa mfano ya Ruaha, ya kutoka Udzungwa kuja Iringa Mjini pale, tutengeneze ring fence tunavyotoka Mikumi tunaingia Udzungwa, tunaingia Kalenga kwenye Jimbo langu tunakwenda Ruaha Mbuyuni. Kwa hiyo haya mambo yatakwenda vizuri tukifanya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la umeme, kaka yangu Mheshimiwa Muhongo alisema kwamba tuwe na vyanzo vingi vya umeme. Sasa kaka yangu pale Mheshimiwa Kalemani tuliongea juu ya hawa RP Global ambao wanataka kuleta umeme kwenye jimbo langu umeme wa solar. Namshukuru amelipokea, nimwombe watakavyokwenda kumwona…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)