Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyenijalia afya njema hata siku ya leo ikampendeza niwepo hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimshukuru Mheshimiwa Rais lakini eneo kubwa nimpongeze, kwa kiwango kikubwa sana amefanya uwekezaji kwenye mtaji kama taifa. Mheshimiwa Rais anavyoelekeza jitihada kubwa katika ujenzi wa reli ya SGR anafanya capital investment (uwekezaji wa mtaji), anavyoimarisha bandari anafanya capital investment, anavyonunua ndege pamoja na jitihada za ujenzi wa Bwawa la Umeme la Nyerere anafanya uwekezaji katika mtaji. Maana yake nini? Maana yake Mheshimiwa Rais anatuandalia taifa ambalo miaka hamsini ijayo sisi akina Kunambi vijana wa leo na vijana wa kesho tutanufaika na mtaji huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme tu kwamba nimesoma mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano. Nianze kwa kusema mpango ni zao la malengo, unavyotengeneza mpango lazima uanze na lengo ambalo litakupa mpango, mpango utakupa mkakati, mkakati unakupa mbinu, mbinu zinakupa mafanikio. Unavyokuwa na mpango lazima ujiandae na mikakati na mbinu za kutekeleza mpango ili tuweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite kidogo kwenye sekta ya kilimo na kaka yangu Mheshimiwa Bashe ni msikivu sana na naomba katika eneo hili anisaidie kidogo. Ukisoma ukurasa wa 88 mpaka 89 unaeleza habari ya sekta ya kilimo. Sote tunafahamu asilimia 65 ya Watanzania tunapata kipato kutokana na kilimo. Kama hiyo haitoshi kilimo kinachangia takribani 27% kwenye pato la Taifa na kati ya asilimia 27, asilimia 24 ni mauzo ya nje ya nchi na haya yameelezwa kwenye mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado tuna kazi kubwa kwenye sekta ya kilimo, lazima tukubali. Kilimo chetu tunafanya subsistence agriculture, ni kilimo kwa ajili ya kula, not for surplus is for consumption kitu ambacho bado tuna safari ndefu sana. Nchi kama Tanzania yenye ardhi kubwa yenye rutuba lakini bado hatujaitumia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata fursa ya kwenda training ya quality structure system ya mwezi mmoja nchini Japan, nilishangaa sana. Nilikutana na Vice President wa JICA alinieleza maneno haya kwamba Japan kwa mwaka mzima wananunua chakula kutoka nje ya nchi ikiwemo Afrika lakini aliitaja Zimbabwe, why not Tanzania? Kama kuna nchi imebarikiwa ukiondoa Kongo inafuata South Africa na Tanzania ni nchi ya tatu kwenye rasilimali za nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, itoshe kusema pamoja na kwamba tuna changamoto ya funding kwenye sekta ya kilimo, lakini tatizo siyo funding inawezekana tukafanya mageuzi makubwa sana kwa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais. Changamoto kwa Watanzania kuu ni tatu na siyo tu kwa level fulani, Watanzania wote tuna changamoto kuu tatu. Ya kwanza ni mindset. Marcus Garvey alisema neno moja, ukiwaza juu ya jambo lolote umeshindwa. Ukianza kwa kuwaza tu, mmh, nitaweza kweli umeanza kushindwa mapema na hutashida. Ni mindset kwa maana ya positive thinking. Ndiyo challenge tuliyonayo kwamba inawezekana, yes it can be done, kwa Mtanzania hiyo ni changamoto, unaanza kuwa na hofu kabla hujaanza safari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ya pili ni uzalendo, tulio wengi hatuipendi nchi yetu. Ndiyo maana utaona hata kwenye Utumishi wa Umma watu hawawajibiki. Ile OPRAS ningetamani iende kwa nafasi zote hata kwenye teuzi za Mheshimiwa Rais, kila mtu awe na OPRAS. Kama mtu anateuliwa apewe miezi sita hamna matokeo aondolewe tu. Unakuta kama ni Mkurugenzi, Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa anafika anakuta kiti kilekile na analazimika kukaa kiti kilekile mpaka anaondoka hata kubadilisha kiti hawezi, hata kubadilisha mkao wa kiti hawezi, wengi tuna changamoto hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni commitment, utayari juu ya jambo fulani. Itoshe kusema I am not speaking from without, I am speaking from within, nazungumza mambo ambayo nayafahamu. Naomba niseme hapa bayana lengo ni kujenga nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo kwenye suala zima la umwangiliaji bado tuna changamoto.

MWENYEKITI: Bado la tatu, umetutajia mawili.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni commitment (utayari). Tuna changamoto ya uzalendo, pili mindset kwa maana fikra chanya, tatu ni commitment, haya mambo matatu ndiyo changamoto ya Mtanzania siyo fedha, hatuna shida ya fedha hii nchi ni tajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya kilimo tunatakiwa kufanya mageuzi makubwa sana. Kaka yangu Mheshimiwa Bashe pale Mlimba, Kata yangu ya Mgeta ina shamba ya hekta 5,000 mpaka leo zimetekelezwa. Serikali imewekeza kuna miundombinu ya umwangiliaji ndani ya hekta 3,000 na hekta 2,000 ndiyo bado na huu mradi hadi Baba wa Taifa miaka ya 1985 alipewa msaada na Serikali ya Korea lengo ni kuifanya Tanzania ipate uwezo wa kujikimu kwenye chakula. Ule mradi wamekwenda wajanja wajanja fulani mpaka leo umetelekezwa, Serikali imewekeza hekta 3,000 zina miundombinu ya maji ya kumwangilia hekta 2,000 ndiyo bado, hiyo ni fedha ipo pale, tungeenda kule tungefanikiwa. Kaka yangu Mheshimiwa Bashe naomba nimpeleke pale Mgeta, Jimbo la Mlimba akaone jinsi gani Serikali inapata hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni sekta ya ardhi, tuna changamoto ya kodi lakini ardhi ya Tanzania inaweza kutupa fedha nyingi sana. Bado sekta ya ardhi haijafanya kazi. Naomba niseme bayana na Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri naomba mnisikilize. Nchi hii inaweza kupimwa, tuna halmashauri 185 lakini leo hii Wizara ya Ardhi hata kupima halmashauri 50 hatuwezi, kuna haja ya kuendelea kuwepo hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina mfano bora, Dodoma hii tunayoona leo, ndiyo maana nimesema naeleza nachokifahamu, Dodoma hii miaka mitatu iliyopita ilikuwa haijapimwa. Mimi ni mfano, Jiji la Dodoma tumepima viwanja 2,000 bila kupata fedha benki wala ya Serikali Kuu. Tukipima nchi hii kwenye halmashauri zote kazi ndogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaeleze jinsi gani wanaweza kupima nchi nzima, Naibu Waziri ananisikiliza. Umesajili kampuni za vijana wa Kitanzania ambao wamesoma, wakajiajiri, ukizipeleka zile kampuni zaidi ya 180, unazo Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye ofisi yako, zikapime kwenye halmashauri zote, ardhi ikipimwa ni mtaji tunaongeza wigo wa kodi. Nitasema kweli daima, kuna pesa tunaiacha kwenye ardhi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ndiyo maana nchi jirani, si mnajua tuna jirani nchi moja tu, tunazo nchi nyingi lakini moja ndiyo jirani zaidi, yule pale Kaskazini, ndiyo maana bajeti yao ni twice comparing with ours kwa sababu ardhi ya Kenya all most yote imepimwa ukiacha lile jangwa. Kwa hiyo, wanalipia every year ardhi yetu haijapimwa, nakuunga mkono. (Makofi)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Anachoweza kufanya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi ni jambo moja tu, kuna vijana waliosoma land management na amewasajili, anazo kampuni zaidi ya 180, leo hii ana- discourage kampuni zisipime nasikitika sana. Namshauri aruhusu kampuni za vijana hawa wakapime kwenye halmashauri zote nchini. Yeye kazi yake wale vijana wakipima ardhi ile mwananchi atapata hati miliki, atakopesheka, uchumi wake utakua, kama ni shamba atakopa mkopo benki atalima. Vilevile wigo wa kodi unaongezeka yaani tax base ya nchi inaongezeka. Hizi kodi tunazokusanya ni ndogo sana sekta ya ardhi peke yake inatupa utajiri wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalize kwa kusema, leo nimesema maneno haya Mheshimiwa Naibu Waziri ikimpendeza kuna ule mfumo wa ILMIS awekeze pale, atafuta fedha awekeza kwenye mfumo, hizi kampuni binafsi ziende kwenye halmashauri zikapime. Waziri hana haja ya kupeleka fedha pale, hakuna haja ya hela, nimepima Dodoma viwanja 2,000 bila hela ya Serikali Kuu na kila mtu amepata ardhi hapa Dodoma viwanja bure inawezekana.

WABUNGE FULANI: Tunanunua.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Ndiyo unanunua lakini nimepima Dodoma karibia asilimia zaidi ya 50, kama kuna mbishi asimame hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihitimishe kwa kusema kama kweli tunataka kumsaidia Mheshimiwa Rais Wizara ya Ardhi ijitathimini. Kwa kiwango kikubwa tunataka nchi hii iwe tajiri. Naomba kuwasilisha. (Makofi)