Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nianze kwakumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa na kwangu mimi ni mara ya kwanza kuzungumza katika Bunge lako Tukufu. Niwashukuru pia wana CCM na hasa Wajumbe wa Butiama kwa kuniwezesha kupita kwenye kura za maoni na baadaye vikao vya chama vikaleta jina na baadaye nikapita bila kupingwa. Watu wa Butiama nawaahidi mtumishi bora uliotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishukuru familia yangu kwa kunipa moyo wakati wote wa harakati na wanaponipa moyo ninapohudumia wananchi wa Butiama kupitia Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hotuba za Mheshimiwa Rais zote mbili, napenda nianze kusema naunga mkono hoja hiyo, lakini nianze kwa kusema moja kwa moja zinapaswa kuwa rejea kwetu sote hususani wasaidizi wa karibu sana wa Mheshimiwa Rais kwa maana ya Mawaziri wetu na watendaji wote wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hotuba hizi hakuna jambo aliloliacha kwenye sekta ya kilimo, kwa mfano imezungumzwa kwa kirefu kuanzia ukurasa wa 13 mpaka wa 15 lakini imekwenda kutaja mifugo mpaka ukurasa wa 17 ambapo Mheshimiwa Rais amesisitiza umuhimu wa kuongeza tija katika mazao ya ukulima, ufugaji na uvuvi. Sasa ushauri wangu kwenye hili baada ya Rais kulizungumza kitaifa,ni jambo jema sasa wasaidizi wake warudi kwenye ngazi za utekelezaji ili kweli kilimo hiki kiweze kuleta tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya Wabunge wamezungumza hapa kiwango cha chini cha uzalishaji kwa heka, nimehudumu pale Simiyu, wastani kwa hekari moja ya pamba wananchi wa kawaida wanapata kilo mia sabini, lakini pale pale Simiyu Wilaya ya Maswa wapo wakulima bora wanaweza kupata kilo 1,200 kwa hekari moja. Sasa kumbe upo uwekezano wa kuongeza productivitykwa heka badala ya kufikiria kuongeza ukubwa wa mashamba ni muhimu wataalamu wetu wajikite kuwaelekeza wananchi hasa wakulima namna ya kuongeza uzalishaji kwa hekari moja, mbili kuliko kuongeza ukubwa wa mashamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye mifugo, nilikuwa naongea na wananchi wajimbo langu nilifanya ziara baada ya vikao vilivyopita, unakuta ukubwa wa ng’ombe kwa maana ya uzito ng’ombe anaweza akawa na kilo 90, tukawa tunatania baadhi ya wananchi wanakilo 150, 120 kwa uzito, ina maana mtu anamzidi ng’ombe uzito, jambo ambalo halikubaliki. Sasa Wizara ya Mifugo na Wizara ya Kilimo tunaona wameanza vizuri na kasi nzuri, nampongeza Waziri na Wasaidizi wake, lakini zaidi na Katibu Mkuu kwa kazi ambayo wameanza kwa kasi kwenye sekta ya kilimo, ambapo wameshakutana na wataamu lakini wamesogeza huduma za ugani karibu na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Simiyu kwenye viwanja vya 88 Nyakabindi utaalam wote wa sekta ya mazaoupo pale, kwa hiyo wananchi wetu wa mikoa ya jirani wamekuwa wakienda pale kupata elimu ya namna ya kuongeza tija kwenye mazao yao. Vile vile nimeona kwenye sekta ya mifugo Waziri na wataalam wanajitahidi kuhamilisha mifugo (artificial insemination)ili tuweze kupata koo bora na hivyo tuweze kupata uzalishaji wa mifugo iliyokuwa bora zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amezungumzia miundombinu na mimi kwenye hili namuunga mkono sana na naomba Watanzania wengine tuendelee kumuunga mkono kwenye hili. Nakumbuka kabla ya Rais wetu hajaingia kwenye sekta ya ujenzi watu wa Kanda ya Ziwa wakitaka kwenda Dar es Salaam ilikuwa inalazimika wapite Bukoba, waende Kampala, waende Nairobi ndiyo wafike Dar es Salaam, unaenda kwenye nchi yako unapita kwenye nchi nyingine mbili, lakini leo mtu anatoka Bukoba anaingia sehemu yoyote ya Tanzania kwa lami, hivi ni vitu vya kumpongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Jiji la Dar es Salaam tafiti za World Bank, nakumbuka niliwahi kutoa taarifa iliyokuwa inaonesha kwambakwa ile foleni tuliyokuwa nayo, tulikuwa tunapata hasara, tunapoteza karibu shilingi bilioni 40 kwa siku kwa ile foleni tu, leo Rais amesaidia kufungua hizo barabara, kuweka hizo flyover, kupanua ukubwa wa barabara,efficient ya usafiri umeanza kuiona, frustration ambazo wananchi walikuwa nazo, wawe wanafunzi kuchelewa shule, wawe wagonjwa wanaopelekwa hospitali, wawe wasafiri wanaoenda airport walikuwa wanakumbwa na msongo wa mawazo kwenye foleni za barabarani, lakini leo tunaona Dar es Salaam inavyopitika, tunataka mikoa yote iwe hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba Rais wetu aendelee, nina imani hata nchi jirani wanatuonea gere kwa namna tulivyopambana kuboresha miundombinu yetu. Ushauri wangu kwenye sekta hii ya usafiri na usafirishaji ni kushuka kule chini, Waheshimiwa Wabunge wamesema karibu wote kwamba kiwango cha fedha wanazopewa TARURA hakitoshelezi sekta ya TARURA kuboresha barabara za halmashauri na za vijijini. Nafahamu sababu, wakati wanaweka hivi viwango vya asilimia 30 kwa 70 kiwango cha barabara za halmashauri kilikuwa ni kilometa 58, leo tunazungumza zaidi ya kilometa 120,000 za barabara za vijijini, sasa kuendelea kuwapa kiwango cha asilimia 30 kwa kweli ni kuwatweza wataalam wetu wa TARURA na kufanya walaumiwe pasipo na sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunazungumzia hizi barabara kuu, naomba pia barabara za wilaya zetu zizingatiwe. Nafahamu tunayo barabara kutoka Ziroziro kwenda Bukabwa, Bwiregi, Nyamimange, Silolisimba hadi Serengeti, ushauri wetu hizo barabara zisaidiwe. Naona sekta ya ujenzi wanajenga kilomita mbili mbili kila mwaka,kwa kasi hii itachukuwa miaka makumi kabla hatujafika mwisho. Piai ipo barabara ya kutoka Mazami kupitia Butiama kwenda Nata, hii nayo ikamilike, maana ni ya muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sekta ya nishati…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA:Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. JUMANNE A. SAGINI:Mheshimiwa Naibu Spika, basi nashukuruna naunga mkono hoja. (Makofi)