Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nami nichangie bajeti hii ya Wizara hii muhimu ya TAMISEMI kwa kuanza na maneno yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyezi Mungu Subhanahu-Wataala anasema kwenye kitabu chake kitakatifu cha Quran, “antum shuadaau fil-ardhwi.” Kwamba wenyewe nyie binadamu hapa hapa duniani mnajuana na mnafahamiana kwamba huyu anafanya nini na huyu yupo vipi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila anayesimama ndani ya Bunge hili anaanza kwa kupongeza. Sisi Wabunge tunafahamiana, nani anayepongeza kwa dhati na nani anayepongeza kwa ajili ya kutaka kuonekana kwamba naye anaiunga mkono Serikali, lakini kinafsi tunafahamiana sisi binadamu wenyewe humu ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuzungumza kwa dhati kabisa kwamba Mheshimiwa Jafo mimi ninampongeza. Pongezi zangu hizi ni za dhati kabisa kwa sababu sinaga unafiki siku zote. Ninalozungumza, kama kuna ukweli nazungumza ukweli kwamba hapa natakiwa nizungumze ukweli, kama kwenye kukosoa ninakosoa ukweli. Mimi ni miongoni mwa watu ndani ya Bunge hili ambao tunazungumza ukweli panapotakiwa kuzungumza ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Jafo tunakushukuru sana kwamba uliweza kuleta fedha pale Mtwara shilingi bilioni 21 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Mtwara ikiwemo ujenzi wa baadhi ya barabara pale Manispaa ya Mtwara Mikindani ambapo Mbunge wake ndio mimi ninayezungumza, Mbunge wa Mjini Kanda ya Kusini pale. Zile fedha zimefanya kazi ile ambayo Mheshimiwa Jafo ulikusudia iweze kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kuzungumza ndani ya Bunge hili kwamba wakati tunapitisha wale Waheshimiwa Madiwani, wameenda kusaini ule mkataba, walienda kusainia Dar es Salaam na yule Mkandarasi ambaye anafanya kazi ya ujenzi wa ule mkataba. Sasa sijui kulikuwa na nini? Niliwahi kuuliza hapa ndani ya Bunge Mheshimiwa Jafo nikamweleza kwamba kwa nini wale wahusika walikwenda kusainia ule mkataba Dar es Salaam? Kwa sababu taarifa tulizokuwa nazo ni kwamba kulikuwa na ujanja ujanja kidogo ulifanyika ili baadhi ya fedha ziweze kuchotwa na kutumika kwa maslahi mengine ambayo siyo ya ule ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kwenye hizi fedha, ujenzi unaendelea vizuri, lakini unachelewa kukamilika, sasa hatujui tatizo ni nini? Tatizo ni wewe TAMISEMI au tatizo ni yule Mkandarasi ambaye ni Kampuni ya Kichina? Barabara kadhaa zimejengwa, nyingi bado hazijakamilika pale Mtwara Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba msukumo wako Mheshimiwa Jafo, kwa sababu ni mtu ambaye unasikia tukikueleza, tunaomba umsukume yule Mkandarasi, barabara zile za Mtwara Mjini eneo la kupumzikia wananchi wa Mtwara pale Mashujaa, tunajenga pale Hide Park, eneo la kupumzika lile, paishe, pakamilike kwa wakati ili vijana wetu waweze kupumzika siku za weekend na sisi wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini. Kwa hiyo, tunaomba huu mradi uufuatilie uweze kukamilika kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni hili suala la ugonjwa huu ambao Mheshimiwa Jafo ameugusia, ugonjwa wa Corona, ni ugonjwa ambao ni hatari sana. Ugonjwa huu hasa kwenye Halmashauri hizi ambazo zipo pembezoni huko kwa mfano Mtwara, kule Kitaya maeneo ya Masasi, Nanyumbu na wapi ambapo tumepakana na nchi ya Mozambique wananchi wanaingiliana sana na sijaona utaratibu wa Serikali kwamba inawapima wale watu wanaokuja kupitia zile njia za panya. Kwa sababu maeneo yale ya Kitaya, Mahurunga na Kivava watu wanapita usiku na mchana kutoka Msumbiji kuja Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nashauri Wizara ya TAMISEMI iweke mpango maalum wa kuhakikisha kwamba mipaka ile (njia zote za panya) zinazibwa na wale watu wanaoingia wanapimwa sawa sawa. Hiki kitendo ambacho kinafanywa na Serikali kwa kumulika tu, unachukua kitu kama tunavyofika hapa Bungeni unamulikwa usoni, halafu joto lako sijui likiwa 32 wewe hauna Corona. Wenzetu nchi za nje ukienda Kenya hawapimi kwa kipimo hicho tu kimoja wakaweza kugundua kwamba huyu mtu anaumwa Corona, wanapima damu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tulikuwa tunaomba sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, weka fedha za dharura kwa ajili ya kushughulikia watu wote wanaoingia Tanzania na Watanzania kila Halmashauri waweze kupimwa damu tuweze kugundua ugonjwa huu wa Corona.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipimo cha kumulika joto tu kwamba joto limepanda au halijapanda, mtu mwingine anaweza akapanda joto lake kwa sababu ya mazoezi, ametembea sana kwenye jua, joto lake likapanda. Ili tuweze kugundua kweli kuna wagonjwa wa Corona Tanzania, tufuate nchi za wenzetu; majirani zetu hapa Kenya na Uganda wanatumia vipimo maalum, kila mwananchi anapimwa kipimo cha damu ili aweze kugundulika kama ana Corona au hana vimelea hivi vya Corona. Tunaiomba Serikali ichuke suala hili seriously. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kuna suala hili la Hospitali za Wilaya. Niliwahi kusema mwaka 2019 kwamba maeneo mengi wenzetu wamepewa Hospitali za Wilaya, Manispaa ya Mtwara Mikindani sina Hospitali ya Wilaya na niliongea na Mheshimiwa Jafo tukakubaliana kwamba atatenga fedha kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Mtwara Mikindani, lakini mpaka leo zile fedha hazijaletwa na tulishatenga eneo pale Kata ya Ufukoni ambapo kuna wakazi wengi sana, nikazungumza na Mheshimiwa Waziri Kata ya Ufukoni ina wakazi wengi sana, hatuna Kituo cha Afya lakini pia Manispaa nzima haina Hospitali ya Wilaya. Tunaomba itengwe fedha tujengewe Hospitali za Wilaya, pale Mtwara Mikindani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, hii ni bajeti yangu ya mwisho kuzungumzia suala la TAMISEMI mwaka huu 2020. Mheshimiwa Waziri kwa kuwa uliniahidi kwamba Mtwara Mjini utaleta fedha tujenge Hospitali ya Wilaya, naomba basi mwaka huu utuletee zile fedha, wananchi wa Mtwara nilishawaeleza kwamba tayari Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ameahidi na ameiandika kwenye diary yake kwamba miongoni mwa maeneo ambayo Hospitali za Kanda zitapelekewa fedha kujengwa ikiwemo ni Manispaa ya Mtwara Mikindani, mwaka huu tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, tulipata zile fedha kwa ajili ya kuboresha Kituo cha Afya cha Likombe. Tulipata shilingi milioni 500 pale Mtwara. Sasa kituo kile kinatumika sasa kama Hospitali ya Wilaya kwa sababu hatuna Hospitali ya Wilaya. Wananchi wa maeneo mengi hata maeneo ya vijijini kule Mtwara Vijijini, Jimbo la Nanyamba na wengine wanatoka Mozambique wanakuja kujitibu kwenye Hospitali ile ya Likombe, lakini ile hospitali haina capacity kubwa ya kuweza kupokea wagonjwa wengi kwa kiasi hicho ambacho wanafika pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, bado tunaomba kile kituo kama mpango wa Hospitali ya Wilaya bado unachelewa, basi kipewe vitendea kazi maalum; kiwekewe X-Ray, kiongezewe watabibu na kipelekewe madaktari bingwa kwa sababu kile kituo kinafanya kazi kama Hospitali ya Wilaya. Mheshimiwa Jafo kwa kuwa ni msikivu sana tunaamini na wananchi wa Mtwara wanaamini kwamba haya yote ambayo wamenituma kuja kukueleza utayafanyia kazi mwaka huu 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala hili la fedha, Kamati ya TAMISEMI imezungumza na imeshauri Serikali kwamba fedha ambazo zinatengwa na Halmashauri ambazo sisi wabunge tulipitisha hapa kwenye Bunge hili ikawa ni sheria sasa kwamba ile asilimia 10 ni lazima iende kwa wahusika; walemavu na vijana waweze kupata ile fedha, lakini Kamati imeeleza hapa kwamba zipo baadhi ya Halmashauri hazipeleki zile fedha. Nyingine zinapeleka 3% tu. Imetajwa hapa Halmashauri ya Simiyu na Halmashauri nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huku ni kulidharau Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo ndiyo tulipitisha hii sheria kwamba ile asilimia 10 itengwe na kila Halmashauri itenge kwa mapato ya ndani kwa ajili ya kuhudumia hawa watu wenye ulemavu na vijana. Tunaomba sana Halmashauri ambazo hazitengi hizi fedha, Serikali, Mheshimiwa Jafo aje atueleze anazichukulia hatua gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inachukua hatua gani kwa Halmashauri ambazo hazitengi fedha hizi asilimia 10 kwa ajili ya kuwagharamia, kuwapa hawa vijana na watu wenye ulemavu kwa sababu ni sheria ambayo tulipitisha sisi kama Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Kutokuitekeleza hii sheria maana yake ni kulidharau Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii mtaani kuna walimu wengi sana ambao wame-graduate takribani miaka mitatu, minne hivi sasa na hawana ajira. Ukipitia shule za sekondari na msingi ambazo Serikali inajinasibu kwamba tumeweka elimu bure, wanafunzi wamekuwa ni wengi, ikama ya walimu imekuwa ni ndogo. Yaani ukilinganisha walimu na masomo, walimu ni wachache masomo yaliyoko na pia wanafunzi ni wengi kuliko walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba ile ratio sasa ya walimu kwa masomo iweze kuzingatiwa. Hili haliwezi kupatikana kama Serikali inawaacha walimu mtaani wanahangaika, hawana ajira. Shule hazina walimu, lakini walimu wanahangaika, wanatembea mitaani, Serikali haitaki kuwaajiri. Tunaomba kasi ya kuajiri ambayo Serikali imekuwa inadonoadonoa iweke utaratibu maalum wa kuwaajiri hawa walimu ambao wapo mitaani, shule zetu ziondokane na upungufu wa walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walimu wapo wengi sana Mheshimiwa Jafo unawajua huko mitaani. Ukitembelea shule hata hapa Dodoma, nenda kaangalie ikama ya walimu kwa masomo, bado walimu hawatoshi wakati Serikali imesomesha walimu wengi wapo mitaani. Shule za private huko, nazo zimejaa. Kwa hiyo, hawa walimu tumewafundisha kwa kazi gani? Wamesoma kwa gharama kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati nzuri kwenye ule mkopo wa Serikali hawa walimu wote wanasomeshwa na wanakopeshwa, wengine wanapewa grant, walimu wa sayansi wanasomeshwa bure na Serikali. Leo tunawasomesha, tunaenda kuwaacha mtaani. naomba Wizara ya TAMISEMI, kwa sababu tuna uhitaji wa walimu, shule zetu za msingi na sekondari hazina walimu, tuongeze walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, nizungumze kidogo suala hili la TARURA. Wenzangu wamezungumza kwamba TARURA ina maeneo mengi ya kufanyia kazi ikiwezekana kuliko hata TANROADS kwa sababu miji yote, vijijini huko na mijini wamepewa usimamizi wa TARURA. Fedha wanazopewa ni asilimia 30, TANROADS wanapewa asilimia 70. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunaomba atleast iweze kuongezwa hii fedha asilimia 30 ifike asilimia 50 angalau iwe nusu kwa nusu kati ya TANROADS na watu wa TARURA ili hawa watu wa TARURA waweze kujenga barabara zetu. Barabara zetu ni mbovu na mafuriko ndiyo hivyo kama unavyoona tena na ofisi ambayo inashughulikia suala la maafa mwaka 2019 haijapewa hata senti tano. Ofisi ya Mheshimiwa Jenista hapa haijapewa hata senti tano kwenye suala la maafa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tulikuwa tunaomba, ili kuokoa barabara zetu, maafa haya ambayo yanatokea mijini na vijijini, TARURA ipewe fedha itasaidiana na Wizara ya Mheshimiwa Jenista ili kujenga barabara ambazo zimebomoka huko mijini na vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)