Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nimshukuru pia Mwenyezi Mungu kutujaalia uzima na atujaalie atuvushe na janga hili la corona na naomba Watanzania wasikilize maagizo yaliyotolewa na Serikali pamoja na wataalam.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni miaka mitano sasa, hii ndiyo bajeti ya miaka mitano tangu tumeingia hapa Bungeni. Mimi nilibahatika pia kuwepo katika miaka mitano iliyotangulia. Nimeona utumishi uliobadilika sana nikilinganisha na vipindi hivi viwili ambavyo nilikuwepo kwenye Bunge.

Katika kipindi hiki ni lazima niseme mambo yafuatayo ili Watanzania wajue na wananchi wajue kwamba mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Mheshimiwa Rais katika maeneo ya utumishi wa umma yameleta heshima kubwa sana kwa Taifa na sasa wananchi wanahudumiwa vizuri kupita wakati wowote ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumeona ameokoa pesa nyingi sana katika fedha za umma kwa kufuta safari za nje, kwa kurekebisha Sheria ya Manunuzi ambayo ilikuwa inatumika vibaya, lakini vilevile amesaidia sana kuhakikisha kwamba rasilimali hizi zilizokuwa zinaokolewa zinakwenda kwenye uwekezaji wa wananchi kama vile madawa yameongezeka, shule nyingi zimejengwa na kwa uchache nitaelezea shule zangu zingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba ipo pia miundombinu mingi na ya nguvu iliyojengwa kwa kipindi hiki. Kwa mfano, ujenzi wa reli katika kiwango cha standard gauge, ujenzi wa Bwawa la Nyerere ni miradi ya kimkakati ambayo ingeweza kujengwa katika Awamu ya Pili, ingeweza kujengwa katika Awamu ya Tatu, ingeweza kujengwa katika Awamu ya Nne lakini huyu Bwana kwa sababu ana maamuzi magumu na anachukua hatua za mara moja ameamua yeye mwenyewe. Ndiyo maana tunamuita sasa ni Bulldozer kwa sababu miradi yote hii Mungu akimsaidia sana atakaa miaka 10 tu kwenye nafasi hii lakini miradi hii itadumu kwa karne, Watanzania watakuwa wamepata Mtu wa pekee kwa sasa kuliko wakati wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Watanzania wajue, leo tuna Rais ambaye anatolewa mfano ndani ya Tanzania, nje ya Tanzania na duniani pia. Sasa ni wakati wa kumtumia vizuri na wakati mwingine kumpa nafasi zaidi na katika miradi amesema yeye mwenyewe kwamba katika suala la maendeleo hakuna siasa wala itikadi na wenzangu wa upande wa pili nimekuwa nikiwasikia wanasema amechukua ajenda zetu, sasa kiongozi afanye nini? Ameona kwenu kuna jambo zuri na ya kwake mazuri akayachukua, pamoja akatekeleza. Kwa hiyo, ni nafasi sasa tumwache katika miaka mitano ijayo ili atende kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ujio wa Mheshimiwa Magufuli kuwa Rais haukutarajiwa na watu wengi. Ni kama maongozi ya Mwenyezi Mungu kwa sababu tumekuta nchi yetu iko katika hali ngumu sana; rushwa, madawa ya kulevya na vitu vingine. Ameingia mtu ambaye amekuwa jasiri katika mambo hayo na ameyashughulikia sawasawa na sasa Taifa liko na Heshima. Tanzania imepata heshima miongoni mwa Mataifa, anasikika kila mahali. Kwa hiyo, kiongozi wa namna hiyo ukimpata, ni vizuri Watanzania kufikiri mara mbili. Ni wachache kupatikana hawa watu. Watu wanaothubutu, wenye uthubutu wa nguvu kama huu na kwa kweli watu wote mmeona madawa ya kulevya kwaheri, rushwa nchini kwaheri, maliasili zetu zimetunzwa vizuri, miundombinu inajengwa kwa nguvu zote. Kwa hiyo niseme tu kwamba miaka mitano hii iliyopita Serikali yetu imefanya jambo kubwa sana miongoni mwa Watanzania na miongoni mwa Mataifa yanayotuzunguka na ndiyo maana nchi zote ambazo zinatuzunguka wanasema tupate Magufuli wetu. Kwa hiyo tumepata kiongozi ambaye ni mfano katika Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hilo, niseme tu kwamba, katika Jimbo langu nimepata pesa za kutosha katika elimu. Katika elimu tumepata pesa za kutosha, Shule ya Sekondari ya Milundikwa nilisimama hapa kuomba na kila mtu alisikia nimepata zaidi ya milioni 700 na ni shule ya mfano kabisa. Shule ya Sekondari ya Hundi tumepata zaidi ya milioni 130 na tumejenga, Chuo cha Maendeleo-Chala ambayo sasa ni VETA ambayo inapiganiwa tumepata milioni 636 na sasa tayari majengo yanaisha. Miundombinu, barabara yetu ya kutoka Sumbawanga kwenda Kanazi, kwenda Kibaoni imekwisha kuwekewa lami. Tunamaliza hivi, tumeanza Shule ya Sekondari mpya ya Myula na tumepata pesa, kwa hiyo kila mahali tumeweza kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, naomba kueleza matatizo yafuatayo yaliyopo Jimboni kwangu.

(Hapa baadhi ya Waheshimiwa walizungumzia bila kufuata utaratibu)

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni changamoto, lazima yawepo hakuna wakati matatizo yote yatakwisha. Naomba fedha zaidi katika ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kasu ambacho tumekuwa tukikisema kila wakati, naomba fedha zaidi katika Kituo cha Afya cha Kala ili kiweze kufanikiwa.

Naomba vilevile niweze kupata fedha katika Kituo cha Afya cha Ninde ambacho tayari wametupatia pesa milioni 200 waongeze hela nyingine kiweze kukamilika lakini kwa vyovyote vile tumefanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, naomba matengenezo ya barabara ya Nkana-Kala, Milundikwa- Kisura, Namasi-Ninde, Kitosi-Wampembe, naomba umeme katika Kata ya Kala, Kata ya Wampembe, Kata ya Kizumbi na Kata ya Ninde. Kazi hii nzuri najua kwa maombi haya na Serikali yetu yote haya yatawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, nawashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)