Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu. La pili, naomba niwapongeze sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waheshimiwa wote kwa kazi kubwa wanayoifanya na hatimaye kuhakikisha Tanzania yetu inasonga mbele.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana pamoja na timu yako nzima kwa kazi kubwa uliyoifanya na hatimaye sasa tunakwenda mwaka wa tano ukituongoza kwa umahiri, kwa ujemedari mkubwa na hatimaye Bunge letu limefanya kazi kwa ufanisi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nina ajenda moja tu ambayo naomba unisikilize vizuri na Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba alipe nafasi jambo hili. Nitaongelea suala la wavuvi.

Mheshimiwa Spika, tumelalamika sana kuhusiana na wakulima na hatimaye Serikali ikatusikiliza. Hata hivyo, kwa sababu Mkoa wa Rukwa umezungukwa na maziwa; Ziwa Rukwa na Ziwa Tanganyika na Wanasumbawanga wengi ni wavuvi na wakulima leo nitaongelea kuhusu wavuvi. Kwa hiyo, kwenye sekta hii ya uvuvi nataka Mheshimiwa Waziri Mkuu atusaidie kwa sababu ameongelea kwenye ukurasa namba 49.

Mheshimiwa Spika, suala la uvuvi, naunga mkono kabisa hoja ya Serikali ya kupinga uvuvi haramu, sigombani nao katika hili. Wavuvi wa Lake Tanganyika wanakwenda kununua nyavu hizi madukani.

Mheshimiwa Spika, naomba nieleze kidogo kwamba kuna sheria imepitishwa kwamba nyavu ambazo zinatakiwa zivue ndani ya Lake Tanganyika ni milimita 8. Sasa hii milimita 8 inapitishwa na nani? Hii milimita 8 inapitishwa na watu wa TBS. Kwa hiyo, wale wenye maduka wanaagiza mzigo kutoka nje, unakuja TBS wanaukagua na TBS wanapitisha unakwenda madukani na madukani wananchi wale wanakwenda kununua kwa ajili ya kwenda kufanya shughuli mbalimbali za uvuvi.

Mheshimiwa Spika, inanisikitisha sana, kule Lake Tanganyika wale wavuvi wamekwenda madukani, wameuliza nyavu za milimita 8, wamenunua, wamekwenda kwa ajili ya uvuvi lakini kwa bahati mbaya sana Waziri wa Uvuvi pamoja na timu yake ikatuma na kipimo kingine kipya milimita 8 nyingine ambayo sijui wameitoa wapi. Wamekwenda tena kupima kule, wamekamata nyavu wakasema zile nyavu zipo chini ya kipimo chao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilimpigia simu Mheshimiwa Waziri Mkuu nikamueleza jambo hili, nilimpigia Waziri wa Uvuvi na Mifugo na Waziri wa Viwanda na Biashara, hapa kuna mchanganyiko, inasikitisha sana. Unakuta kuna raia au mtumishi amestaafu, amekwenda nyumbani kafika kule chini Lake Tanganyika amekuta kazi hakuna, wakamshauri kazi kubwa tuliyonayo huku ni uvuvi. Yule mtu anachukua kiinua mgongo chake anakwenda dukani kutaka nyavu halali, milimita 8 anaitaka, anapewa. Anafika kule anaunga nyavu zake anaanza uvuvi milioni 15 ameingiza katika uvuvi. Anakuja mtu mwingine wa uvuvi na kipimo chake kingine tofauti na cha TBS anapima anasema hii siyo milimita 8, anamkamata, anamtoza faini shilingi milioni tano lakini yule mzee anasema mimi nimenunua dukani; kwa nini hawa wanaouza nyavu wasikamatwe nikamatwe mimi ambaye sijui chochote? Mheshimiwa Waziri Mkuu watu hawa wanaumia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri sana Serikali ilifuatilia ikaunda Tume huru ikaenda kule; wamo watu wa TBS, Wizara ya Uvuvi na Usalama wa Taifa kupima zile nyavu zimeonekana ni halali. Sasa Waziri anatoa tamko kwamba anatoa miezi mitatu nyavu zile ambazo zipo chini ya kiwango cha kwao wao kuwa mwezi Juni wawe wameziondoa. Kwa hiyo, amewapa muda wa miezi mitatu waweze kuvua kwa muda ili waweze kufidia nyavu zile ambazo wamezinunua madukani.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kosa la Serikali, Serikali imekuja na vipimo viwili; TBS wana kipimo chao lakini Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wenyewe wana kipimo chao, mwananchi atajuaje kipimo halali ni kipi? Mwananchi huyu anayekwenda dukani kununua nyavu atajua vipi kuwa hii ndiyo TBS haitakiwi na hii ndiyo Wizara ya Uvuvi inatakiwa kwa sababu nyavu zipo madukani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya sana au kwa bahati nzuri sana, baada ya Serikali na Tume kugundua kwamba Serikali ndiyo yenye makosa, wakaruhusu kwamba nyavu hizo zitumike ndani ya miezi mitatu, lakini wameruhusu nyavu wakati sio wa uvuvi. Masika hii wavuvi wote wanasimamisha uvuvi kwa sababu wakivua dagaa wakizianika zinalowana. Wametoa miezi mitatu mwisho mwezi Juni lakini kosa sio lao. Kwa msingi huo ilitakiwa Serikali ilipe fidia kwa sababu makosa ni ya Serikali; makosa ni ya Wizara ya Uvuvi na Wizara ya Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilimpigia Waziri wa Viwanda na Biashara anajua na Mheshimiwa Waziri Mkuu, nikampigia Mheshimiwa Waziri wa Uvuvi, wamekwenda wamechunguza imeonekana TBS wana makosa au Wizara ya Uvuvi ina makosa, kwa sababu wamekuja na vipimo viwili. Ushauri wangu tungewapa watu muda wa mwaka mzima. Shilingi milioni 15 kuirudisha ndani ya miezi mitatu kwa kosa la Serikali haitowezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mvuvi huyu naye anaongeza mapato ndani ya Mfuko wetu wa Taifa, mvuvi huyu ni sawa na mkulima na mvugaji lakini anaonewa siku hadi siku. Mheshimiwa Waziri Mkuu nikuombe sana muda aliotoa Mheshimiwa Waziri wa miezi mitatu ni mdogo kwa kosa la kwetu sisi wenyewe. Kama Serikali ingeweza kutusaidia basi huu muda ambao tumewapa wa miezi mitatu ambapo wavuvi wamesimamisha uvuvi kwa sababu kuna mvua, hawawezi kuvua wakati huu, uvuvi rasmi unaanza mwezi Juni, basi waruhusiwe kuanzia mwezi Juni, wapewe muda wa mwaka mmoja waweze kurudisha gharama zao ama Serikali ifidie gharama hizo iwarudishie fedha zao walizonunua nyavu madukani ambapo maduka hayo yanauza nyavu halali na leseni wanazo. Namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu atusaidie wavuvi hawa wanahangaika sana na sisi ni wawakilishi wao tuna haki ya kuwatetea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya machache, naunga mkono hoja. Nikupongeze sana kwa kazi kubwa, nimpongeze na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya kuitumikia nchi yetu. Ahsante sana. (Makofi)