Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Nafikiri pia ninao wajibu wa kuzungumzia suala la ugonjwa wa corona lakini nitakuwa tofauti kidogo na wenzangu. Ugonjwa huu ni ugonjwa wa Kidunia na ni tatizo linalotuhusu Tanzania na wanaotuzunguka na dunia kwa ujumla. Nataka kumwomba Rais, afikirie tena aweze kufunga mipaka ya nchi kwa sababu; kuna watu wanafika pale Airport wakitokea nje wanarudi nyumbani. Anajua akifika Airport, anaita uber yake anakwenda kwake labda Tabata au Manzese lakini akifika pale anachukuliwa kwenda kwenye isolation, sawa tunakubali siku 14, lakini wanapelekwa kwenye hoteli za gharama na ndiyo maana watu wanatoroka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sijajua ni utaratibu gani unatumika, labda watusaidie na hasa watu wa TAKUKURU, hizi hoteli zimekuwa vetted vipi na kwa nini ziwe hoteli za gharama na Ofisi ya Waziri Mkuu ni ofisi ambayo ina fungu la majanga na maafa kama haya. Mimi nikiwa na corona na nimetoka safari, sijapanga mimi niwe na corona, kwa hiyo ina maana imekuja mimi nikiwa sina pesa. Kwa nini Serikali isifanye maeneo tofauti ya kuwaweka hawa ndugu zetu, wakakaa hizo siku 14 bila gharama hiyo kubwa, dola 150, dola 100, dola 50 hizo ni hela nyingi sana kwa hawa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafikiri tuna haja kwanza ya kufunga mipaka kwa sababu sisi sio kijiji na wala sisi hatuna TBS ya kuzuia magonjwa yasituingie. Naomba tulifikirie kwa upya na tukae chini kwa upya tujipange na hasa Wizara hii tunayoizungumzia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, naomba niongeze suala la Wizara hii ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu alilizungumza. Ofisi hii imetamka vipaumbele vine, moja ya kipaumbele wanazungumzia uchumi wa viwanda, uchumi wa viwanda bila kilimo huwezi kufanya maendeleo yoyote. Asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima. Usipounganisha viwanda na kilimo huwezi kupata faida yoyote. Tunafahamu kiwanda, mkulima wa korosho amelima korosho, tumeimba wimbo huu muda mrefu sana kwamba hawa watu wanahitaji viwanda vya kubangua korosho hapa nchini, lakini mpaka leo viwanda hivyo bado havijawa tayari. Tuna wakulima wa chai kule Rungwe, kwenye ripoti ya Waziri Mkuu anazungumzia yule mkulima wa parachichi, yule ni mfanyabiashara binafsi. Serikali inahitaji kuwa na kiwanda, inahitaji kuweka miundombinu ya wakulima wa parachichi waweze kuuza kwa bei ambayo yule mfanyabiashara binafsi anapata faida mara nne na sisi tunafikiri tunapata faida kumbe tunamnufaisha mtu mmoja.

Mheshimiwa Spika, kama Taifa tunapozungumzia viwanda ni lazima tukae chini tuoanishe kati ya viwanda na kilimo, kwamba kilimo kinapolimwa na chai inapolimwa tuwe na viwanda vidogo vidogo vya chai. Zao la chai linanyweka nchi nzima. Kama sio Tanzania lakini dunia nzima wananunua chai na wala hatujawahi kusikia soko la chai limeshuka bei. Leo hii Wakenya wananufaika kwa zao la chai, lakini sisi hatuna viwanda, tunapeleka kitu ambacho hakina thamani zaidi. Tungekithaminisha katika nchi yetu tungesaidia wakulima wetu kupata kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia uchumi ambao unaoanisha uchumi wa mtu binafsi na uchumi wa Kitaifa, mimi naweza nikaona kwamba sipati hela kwa sababu thamani ya mali ninazozizalisha hazifanyiki hapa nchini. Kwa hiyo tuna haja kubwa na ya makusudi tuweze kutengeneza uwezo wa watu wetu kuzalisha na kupata wateja na sisi tuna watu wengi, tukijipanga vizuri, soko la ndani bado linatuhitaji. Kwa hiyo, nilitaka nichangie katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nataka niingie kwenye habari ya siasa, nimesikia watu wengi wanazungumza humu ndani. Chama cha upinzani chochote kilichomo humu ndani kipo kihalali na kikatiba. Kubezana sidhani kama ni njia sahihi, tunapozungumzia haki, haki inabeba vitu vingi sana. Leo hii ni nani humu ndani, mimi najua na kama mama kuna akinamama wenzetu ambao ni wabaya waliolea watoto wa kambo, anamshika mtoto wake ili ampige mtoto wa kambo. Ni kweli yule mtoto anafurahi, ndivyo ambavyo wenzetu humu ndani wanafurahi, lakini wasijue wanajenga immune ya kiburi kwa sababu kila siku ukipigwa, kesho tena umepigwa, unajenga kiburi na unajijengea ujasiri, mmetujengea ujasiri unnecessary. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni nani asiyejua kwamba leo hii watu wanafanya mikutano, kundi fulani linafanya lingine halifanyi. Ukiuliza, intelijensia, intelijensia hiyo iko upande mmoja? Intelijensia hiyo iko kwa nani peke yake?

SPIKA: Umesema nani asiyejua? Spika hajui, tutajie kwamba fulani anafanya mkutano na fulani hafanyi.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, unafahamu kwamba kiongozi wako wa chama cha siasa Mwenezi Polepole anazunguka nchi nzima. Mnyika kazunguka Mwanza mmemkamata! Kama ulikuwa huna taarifa nakupa taarifa! Ni watu wangapi wanafanya mikutano? Mheshimiwa Sugu Mkoa wa Mbeya hafanyi mikutano, RPC anakwambia intelijensia inakataa, Tulia juzi tu hata siku nne hazijaisha na corona, yuko na wananchi! Ina maana huoni? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, undugu tuliozaliwa nao, urafiki tuliokuwa nao…

SPIKA: Mheshimiwa Mwakagenda, kawaida ya Maspika wote duniani wao huambiwa!

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, nakwambia.

SPIKA: Ahsante!

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, undugu tuliojengewa humu ndani kuna watu wana ma- boyfriend humu, kuna watu tuna kunywa chai pamoja humu lakini kwa tabia hii… [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

SPIKA: Mheshimiwa Sophia, una hakika? Maana meza yangu haijui hayo…

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: … mimi ninaye! (Kicheko)

SPIKA: Meza inakutaka basi utoke wazi maana umeamua kutoka wazi! (Kicheko)

MHE. SOPHIA H. MWAKAENDA: Mheshimiwa Spika, nimetuma barua kwa Mwakagenda, akishaniridhia nitatoa hadharani.

Mheshimiwa Spika, tunahitaji umoja, kujenga umoja ni kazi kuubomoa ni kitu kidogo. Sisi sote tunawakilisha wananchi…

SPIKA: Nafikiri Sophia hapo ulipokwenda ama uendelee ama ufute kwa sababu umelituhumu Bunge na nina hakika magazeti yote yatajaa kwamba watu wana mahawara humu ndani na watu wana wake zao na waume zao na heshima zao. Kwa hiyo ni bora ukajitokeza tu wazi ukaeleza nani na nani ni mahawara humu…

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, mimi nimefuta, naomba niendelee.

SPIKA: Basi kama umefuta tunaelewana.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosisitiza umoja ni muhimu, mwisho wa siku sisi ni ndugu tumetumwa na wananchi kuwawakilisha, tufanye kazi kwa pamoja bila kubaguliwa.

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee suala la Tume ya Taifa. Ameizungumza msemaji mmoja kwamba tunakimbilia kusema refa atutetee. Tume ni refa ndiyo wala sio utani! Lazima asimame katikati na sisi tumesema toka mwanzo tungebadilisha kanuni zetu na taratibu zetu,

Mwenyekiti wa Tume akachaguliwa na Bunge hili au na kitu kingine chochote tusingekuwa na malalamiko haya.

Mheshimiwa Spika, kazi ya Tume ni uchaguzi, mwanzo wa mwaka mpaka miaka mitano inapoisha, ndiyo kazi yake. Kazi yao kuhakikisha watu wanajiandikisha kwenye madaftari, watu wanapiga kura na kusimamia uchaguzi na kuhakikisha mtu anayestahili kutangazwa anatangazwa, lakini utakuta siku za kujiandikisha Tume inaweka siku chache. Watu wengi hawajaandikwa, tukienda kule Zanzibar, watu wengi hawana vipande, wameshindwa kujiandikisha kupiga kura ili waje wachague mtu wanayemtaka.

Mheshimiwa Spika…

SPIKA: Mheshimiwa Sophia pokea taarifa. Waziri wa Nchi.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,
naomba tu nimpe Taarifa Mheshimiwa Sophia, utaratibu wa Tume katika kufanya jambo lolote ambalo linahusu uchaguzi ni utaratibu shirikishi. Kabla Tume haijaanza kuandikisha wapiga kura, kabla haijaanza kuboresha daftari vyama vyote vya kisiasa vimekuwa vikishirikishwa na vinakuwa na maamuzi ya pamoja. Kwa hiyo naomba tu nimwambie Mheshimiwa Sophia kwamba hicho anachotaka kukisema si kitu cha kweli kwa sababu kila jambo limekuwa ni shirikishi na baada ya ushirikishwaji Tume ndiyo inaanza kufanya kazi na safari hii imefanya vizuri kweli, hata mikoani haikuanza kazi kabla ya kuwashirikisha wadau wote ikiwemo vyama vya siasa na nafikiri hata Sophia alikuwa anashiriki hiyo mikutano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba tu nimpe hiyo Taarifa Mheshimiwa Sophia Mwakagenda.

SPIKA: Mheshimiwa Sophia pokea taarifa.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, sijaipokea Taarifa kwa sababu kazi yangu mimi ni kuishauri Serikali na yeye ni Serikali. Namshauri kwamba Tume kazi yake ni kusimamia uchaguzi mwaka wa kwanza mpaka mwaka wa tano. Tunaomba Tume haina kazi yoyote, Tume haishughuliki na corona wala malaria, inashughulika na uchaguzi. Kwa hiyo tunaiomba Tume kuanzia mwaka wa kwanza tunapomaliza uchaguzi iendelee kuwaandikisha watu wapya wanaofikia umri wa miaka 18 ambao walikuwa na miaka 17 wameingia 18 iwaandikishe. Kama kuna watu wamekufa iwatoe kwenye daftari na ukifika wakati tunaenda kwenye uchaguzi sasa, tupate majina mapema. Kwa hiyo, ninachoomba, naishauri Serikali, sio kwamba lazima uchukue Mheshimiwa Jenista, mimi nashauri kama Mbunge ambaye nina wajibu wa kuishauri Serikali na ndiyo kazi iliyoniingiza humu ndani.

Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa bado sio huru na kama wako vizuri, wamejenga reli, wamefanya kazi zote, kwa nini wana wasiwasi na hiki kitu kidogo tu cha kuunda Tume Huru, kwa sababu wakiunda watashinda! Kwa sababu wana madaraja kama wanavyosema! Tunataka tusiwe na doubt yoyote, ndiyo maana tunashauri iundwe Tume Huru ya Uchaguzi na kama uko vizuri, Mbunge unapendwa…

SPIKA: Mheshimiwa Sophia, tangu jana tunauliza, Tume Huru inafananaje? Kila mtu akisimama Tume Huru, Tume Huru…

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika…

SPIKA: Hasemi kwa sababu wasiwasi…

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika…

SPIKA: Usiwe na haraka, dakika zako tunazitunza.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Ahsante!

SPIKA: Wasiwasi wetu ni kwamba leo huyu mtu atasema refa hatumwamini, mkibadilisha refa atasema linesman, mkibadilisha, Kamisaa, mkibadilisha TFF, sasa Tume Huru hiyo mnayoiongea, wote inafanana? Kila mtu ana picha ya Tume yake au ni nini ili Serikali iweze kukuelewa na kuwaelewa wote wanaoiongelea subject hiyo.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Tume Huru na hasa Mkurugenzi Mkuu na watendaji wengi wanateuliwa na Rais ambaye kikatiba na kikanuni ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi na nchi hii ni nchi ya Vyama Vingi. Kwa hiyo natoa wazo leo, ni vyema wakaomba kazi, tukawafanyia vetting, wakaletwa Bungeni, tukawachagua tukapata mmoja ambaye tunamuamini sisi kama wananchi wa Tanzania na wala sio kuteuliwa na mtu mmoja. Leo hii Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ndiyo Rais, kesho atakuja mwingine.

MBUNGE FULANI: Taarifa.

SPIKA: Je, ni nchi gani ambayo unadhani ina mfumo ambao Bunge ndiyo linateua Mwenyekiti wa Tume, Sophia.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, tuko kwenye mjadala mpana wa kusaidia Taifa letu, hata kama maongezi yangu unafikiri hayajaenda sambamba lakini wako watu waliopelekwa shule na wanasoma…

MWENYEKITI: Kwa sababu inaelekea unaongelea subject ambayo hujaifanyia utafiti wa kutosha!

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, tuna Kenya…

SPIKA: Kenya bado pamoja na Bunge kushiriki, Rais ndiye anayemteua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi. Mimi sikatai hoja yenu, mnielewe! Mimi nia yangu ni kwamba yaani mje na vitu ambavyo mmejiandaa, mmejipanga vizuri, mnapofanya presentation mimi siwazuii, unapofanya presentation yako yaani unashuka umejipanga, ndiyo maana tunaanza saa nane ili kuwapa nafasi Waheshimiwa Wabunge kuchambua, kuangalia references na kadhalika na sisi wengine tunajuajua kidogo kinachoendelea kwa hiyo huwezi kutudanganya. Hatusemi kwamba Tume iliyoko ni malaika, lakini ni vizuri kujipanga kidogo na kutoa mifano ambayo, yaani kulisaidia Taifa kweli kwa mtu ambaye umefanya homework yako, unashuka vizuri. Endelea tu Mheshimiwa Sophia.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, kama chama tumeandika barua kwa Msimamizi Mkuu wa Nchi japokuwa tunaona siku zinasogea nafikiri na maelezo unayozungumza wewe ambayo yameenda kisomi na yaliyoandikwa kihalali ili waweze kusaidia Serikali. Tumeshaandika barua.

Mheshimiwa Spika, viongozi wetu wameshiriki na kuongea na Rais wa nchi kutaka kuitwa na kuzungumza na kuwa na maridhiano ili waweze kueleza ni nini wanachokitaka. Naomba niendelee…

SPIKA: As long as hiyo barua hamjaandika kwa Spika wala nakala Spika hamjampa na Waheshimiwa Wabunge hawa hawajui kinachoendelea sidhani kama ni haki kutueleza, maana sisi tunashangaa yaani, hatuelewi ndiyo maana…

Nauliza hiyo kwa nia njema unielewe vizuri.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, Serikali kuna Bunge, kuna Mahakama, tumetuma kwa Serikali, mimi naongea hapa ndani kama Mbunge ndani ya Bunge.

SPIKA: Hebu kaa chini! Huyu ni Mbunge gani asiyejielewa? Kama umeandika vitu kwenye mihimili mingine kwa nini unaongea hapa sasa? Subiri, kama unaongea hapa, tueleze na sisi! Unaongea kuhusu kitu gani ufafanuzi wake ni nini? Barua yenu ina nini na wewe unaongelea nini? Kuna ubaya gani katika ushauri huo? Kuna ubaya gani katika ushauri huo? Sisi barua yako hiyo hatuna, hatuijui! Wewe ndiyo unaijua na huko ulikopeleka. Tunapokutaka sisi tueleze ni kitu gani unaeleza, tunakosea nini hapo?