Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kutoa pongezi. Kwa kweli ni furaha sana kuchangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu mambo mengi mazuri sana yamefanyika. Nampa pongezi Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mwenyezi Mungu azidi kumbariki.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpa pongezi pia Mheshimiwa Rais kwa kufanya mambo mengi mazuri. Tunampongeza sana na tunamwombea mbele ya Mwenyezi Mungu, tunaamini kuwa utapita bila kupingwa, hakuna Mpinzani mbele yako. Nikirudi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya mambo mazuri sana kumsaidia Mheshimiwa Rais na wewe Ruangwa watakupa kura za kutosha utapita bila kupingwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Jenista kwa kumsaidia mambo mengi Mheshimiwa Waziri Mkuu. Vilevile niwapongeze Mheshimiwa Kairuki kwa mambo yote anayosaidia; Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Stella Ikupa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe mwenyewe umefanya mambo mazuri sana. Tunajidai kwenye Bunge hili kwa kuwa na Bunge mtandao. Mwenyezi Mungu akubariki na umeacha alama, kila mmoja atakuwa anajua kuwa wewe ndiyo ulianzisha Bunge mtandao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunakushukuru sana na tunakupongeza sana pamoja na Naibu wako pamoja na Wenyeviti wote kwa kutuongoza kwa muda wa miaka mitano kwenye Bunge hili. Tunawashukuru na Mwenyezi Mungu awabariki nyote.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mafanikio ni mengi ambayo yote yameandikwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na kila mmoja anayaona kama anajidai haoni sijui yeye yuko wapi. Reli tumeiona, elimu tumeiona, hospitali tunaziona, maji tunaona, kila kitu tunaona. Kwa kweli Serikali yetu ya Awamu ya Tano tunaipongeza, Tanzania tunajivunia na tunafurahi kuishi kwenye nchi yetu, inapendeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kuongelea kuhusu miundombinu. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kweli wamejitahidi pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu, mmefanya mambo mazuri sana. Nianze na barabara. Barabara za lami zimejengwa, tumeunganishwa. Naweza nikatoka hapa nikaenda Ruvuma siku hiyo hiyo; nikaenda Mtwara siku hiyo hiyo nikafika; nikaenda Lindi siku hiyo hiyo nikafika; nikaenda Kagera nikafika siku hiyo hiyo; nikaenda Mara siku hiyo hiyo nikafika. Kwa hiyo, nashukuru sana kwa mambo hayo ambayo mmeyafanya kwa kuunganisha barabara za lami. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nashukuru kwa upande wa barabara za vijijini, zilikuwa zimejengwa kweli siyo uongo, lakini mambo ya tabianchi hatuwezi kuyabadilisha. Ni kweli tumepata mafuriko, yametokea na tumeyaona, Ila nawashukuru sana, tena sana kwa sababu ingawa yametokea kwa mfano kwenye Daraja letu la Kiegea ambalo linaunganisha barabara na usafiri wa kwenda mpaka nchi za nje, Mheshimiwa Rais alifika, Mheshimiwa Waziri Mkuu amefika, Mheshimiwa Waziri, Eng. Kamwelwe amefika na Waheshimiwa wamefika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru kuwa licha ya kuondolewa hayo madaraja, lakini Serikali inachukua tahadhari haraka sana na kurudisha usafiri na sasa hivi magari yanapita kwenye Daraja letu la Kiegeya ambalo liko kwenye Mkoa wa Morogoro, Wilaya ya Kilosa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande huo huo, naomba tena sana, kwa sababu barabara za vijijini kutokana na mabadiliko ya tabianchi na mafuriko yaliyotokea barabara nyingi za vijijini zimeharibika. Kwa sababu barabara nyingi za vijijini ziko chini ya TARURA, nami naungana na watu wanaosema kuwa TARURA waongezewe fedha za bajeti kwa sababu ya kutengeneza hizo barabara. Madaraja mengi ya vijijini yameharibika, siyo Morogoro tu, ni mikoa mingi imepata dharura hiyo. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu iwe dharura, iweze kuchukuliwa ili hayo madaraja yaweze kutengenezwa na tuweze kupata usafiri hasa kwa mazao pamoja na wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa afya, kwa kweli tunashukuru sana kwa ujenzi wa Vituo vya Afya, ujenzi wa Zahanati, ujenzi wa mahospitali na hata Mkoa wangu wa Morogoro yamejengwa, tunakushukuru sana. Naomba kutoa ushauri kuwa mpaka sasa hivi unakuta Vituo vya Afya vingine na zahanati nyingine kuwa wataalam hawatoshi. Kwa hiyo, naomba huo mgawanyo wa wataalam; manesi, madaktari bingwa, wataalam wa maabara, uweze kuangaliwa ili tuweze kupata mgawanyo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunajivunia hata hospitali zetu za kanda, sasa hivi kwa kweli zinafanya vizuri. Ukiona Benjamin Mkapa inafanya kazi vizuri, Muhimbili inafanya kazi vizuri hata za Kitaifa. Kwa hiyo, sasa hivi tumepunguza hata wagonjwa kwenda nchi za nje na hasa ukiangalia na ugonjwa huu wa Corona. Kwa hiyo, tunamshukuru Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Corona nami naomba kuongelea Corona; kwa kweli ni ugonjwa ambao unaumiza sana. Nilikuwa naangalia kwenye mtandao, unaona unawashika hata watoto wadogo, wanatenganishwa na wazazi wao. Kwa hiyo, ninachokiomba kwa Ugonjwa kwa ugonjwa wa Corona, tuuangalie kwa makini. Pia nawashauri wazazi waweze kuchukua ushauri ambao tunapewa pamoja na Mawaziri wetu, Rais wetu na Waziri Mkuu ili tuweze kuwalinda hata watoto wetu ambapo wewe mzazi unaweza ukapona lakini mtoto wako akachukuliwa akawekwa kwenye karantini. Kwa hiyo, inasikitisha sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kuongelea kuhusu elimu. Natoa pongezi kwa Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa mambo mengi inayoyafanya kuhusu elimu na hasa kwa mkopo huu ambao umeidhinishwa wa World Bank wa Dola za Kimarekani milioni 500 ambazo zitasaidia watoto wetu wa sekondari pamoja na kupunguza mimba za utotoni kwa sababu hata mahosteli yataweza kujengwa. Kwa hiyo, nashukuru sana kwa hilo.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali pia kwa kurudisha usafiri wa treni kwa upande wa Dar es Salaam kwenda Moshi na Tanga kwenda Moshi, pamoja na uendelezaji wa ujenzi na ukarabati wa Reli ya Kati pamoja na ujenzi wa Reli ya SGR.

Mheshimiwa Spika, ombi langu na ushauri wangu kwako na Mawaziri wote, naomba sana hizi reli zitakapokamilika, tupunguze malori yanayopita kwenye barabara zetu ili mizigo inayobebwa kwenye malori haya iweze kubebwa kwenye treni hizi, kwa sababu haya malori yanaharibu barabara zetu. Hebu angalia Wabunge wote tunasafiri kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam, lakini unakuta mahali pengine barabara zetu siyo rafiki kwa sababu ya haya malori ya mizigo. Pia yanaleta msongamano na yanasababisha ajali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ulinzi na usalama. Nchi yetu imebarikiwa kuwa salama chini ya Jemedari wetu, Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Tunashukuru sana vyombo vya ulinzi na usalama, vinafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, naomba sana wananchi wote wanisikilize kwamba tuzidi kutunza amani na usalama kwenye nchi yetu kusudi tuweze kuendelea vizuri kwani amani hainunuliwi, inatunzwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mambo ya Mfuko wa Taifa wa Vijana, natoa pongezi kwa sababu wamefikiwa vijana wengi, vikundi 586, vijana ambao wamefikiwa tayari ni 4,222, lakini ninaomba licha ya kutoa pongezi, elimu izidi kutolewa kwa vijana wote, waweze kupata elimu jinsi ya kupata huu mkopo na hasa kwenye Halmashauri nyingine ambazo bado hazijafikiwa kwa sababu ni Halmashauri 155 ambapo mpaka sasa hivi wametoa hivi vikundi na wameweza kuwapata hao vijana. Hii mikopo iweze kuwasaidia hata vijana ambao wako kwenye kada zozote zile kuanzia wahitimu wa Vyuo Vikuu mpaka wale wa Darasa la Saba, wote waweze kupata na waweze kujiajiri kwa sababu ajira kama tunavyojua haipo. Ajira ni ya kujiajiri na ajira ni wewe mwenyewe.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo naomba kuongelea ni kuhusu nishati. Namshukuru sana Waziri, Mheshimiwa Dkt. Kalemani pamoja na Mheshimiwa Subira kwa kazi nzuri sana wanayoifanya. Ni nzuri sana. Wamefanya kazi nzuri, tumeona umeme. Watu wengine tulikuwa tumezaliwa na kukulia kwenye vibatari, lakini sasa hivi tunaona umeme. Kwa hiyo, jambo ninaloomba ni moja tu; kama mpango ulivyopangwa kuwa vile vijiji pamoja na Vitongoji vilivyorukwa kwa mpango huu wa REA III viweze kufikika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano pale Morogoro kuna Kitongoji cha Chekereni, hakina umeme, lakini naona kuna kiwanda cha mikunde kinawasha umeme pamoja na pale Mtego wa Simba umeme upo, lakini chenyewe kiko katikati hakina umeme. Kwa hiyo, naomba na chenyewe pamoja na vijiji vingine ambavyo vimekosa umeme vipatiwe umeme.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa ni kuhusu pensheni. Kwa kweli kuna wale wafanyakazi wengine ambao hawakufanya kazi kwenye mfumo wa Serikali, wanalia huko, hawajapata pensheni. Walikuwa wanaomba kama inawezekana, watu wote waweze kupata pensheni waweze kupata hela kidogo kama TASAF inavyofanya angalau kuangalia wale ambao hawana uwezo.

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwa kweli Tanzania yetu inapendeza, tusonge mbele chini ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Rais na Waziri Mkuu tunawapa pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante.