Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru sana kwa ushauri huo ambao umeutoa wa kitaalam kweli kweli kwa ajili ya kuepuka carbondioxide, hongera sana kwa utaalam huo na nitakufuata nije nijifunze funze kidogo mambo ya miti shamba.

Mheshimiwa Spika, watu wa Sikonge wamenituma kupitia mikutano ambayo niliifanya kwa kila kijiji mwaka jana, nije nitoe shukrani za dhati kabisa na pongezi nyingi kwa Serikali inaongozwa na Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa miradi mingi ambayo tumeipata Sikonge na imesimamiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu bila kumsahau Makamu wa Rais, Mawaziri wote, Watendaji Wakuu wa Serikali, kwa ujumla wao tunawapa pongezi kubwa sana kwa weledi ambao wameutumia katika kuiongoza nchi hii kwa viwango vya kihistoria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nichukue nafasi hii kukupongeza wewe binafsi na uongozi mzima wa Bunge kwa kuendesha Bunge kwa weledi wa hali ya juu, lakini kwa kutuletea Bunge Mtandao imekuwa ni historia kubwa sana kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, binafsi kama Mbunge wa Sikonge, niliomba miradi mingi kwa niaba ya wananchi wa Sikonge, Serikali ilikubali na utekelezaji umekuwa mkubwa na nikwambie kwa mara ya kwanza tangu dunia iumbwe, wananchi wa Sikonge wameanza kuona lami ambayo inatoka Tabora, inapita Sikonge inakwenda mpaka Mpanda, hilo ni jambo la kihistoria kwao na kwa mara ya kwanza watu wa Sikonge watapata Mahakama ya Wilaya, ambayo ilikuwa ni shida kubwa, wengine walikuwa wanasafiri kilomita 500 kwenye Mahakama ya Wilaya, Tabora Mjini.

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa mara ya kwanza tangu dunia iumbwe, wananchi wa Sikonge watapata Hospitali ya Wilaya ya Serikali. Kwa mara ya kwanza pia kumekuwa na ukarabati mkubwa sana kwenye Chuo cha Maendeleo ya Wananchi kimekuwa kipya cha kisasa. Kwa mara ya kwanza nyingine tumepata vituo vya afya viwili vikubwa Kituo cha Kipili na Kituo cha Nyahua; wananchi hao kutoka sehemu mbali kabisa kilomita 380 Kipili na kilomita 200 Nyahua wataanza kupata huduma vipimo na dawa huko huko waliko bada ya kwenda kusafiri kwenda Sikonge, Makao Makuu ya Wilaya.

Mheshimiwa Spika, tangu dunia iumbwe, Jimbo langu la Sikonge na Wilaya ya Sikonge, tumepata shule mpya mbili za kidato cha tano na sita ambayo nayo ni historia. Niseme tu kwa mara ya kwanza shule zetu kongwe ambazo walisoma viongozi wetu wa juu kabisa wa nchi hii, akiwemo marehemu Mzee Sitta, zimekarabatiwa Shule ya Msingi Sikonge, Shule ya Msingi Chabutwa, imekarabatiwa sasa ni mpya kabisa. Kwa hiyo, kwa kweli mambo mengi yamefanyika Sikonge ambapo katika kipindi hiki cha miaka mitano imekuwa ni historia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa maji kwa mara ya kwanza tumepata bwawa kubwa maana yake tulikuwa na Bwawa la Utiyati ambalo lilijengwa mwaka 1959. Kwa mara ya kwanza tumepata Bwawa lingine la Igumila ambalo ni kwa ajili ya matumizi ya wananchi. Ingawa huku mjini tutakuwa na maji kutoka Ziwa Victoria, ambayo sasa yamefika Tabora Mjini.

Mheshimiwa Spika, lazima nizidi kuipongeza Serikali kwamba yote haya yamefanyika chini ya usimamizi wa Chama cha Mapinduzi. Kamati ya Siasa ya Mkoa ilipotembelea Sikonge hivi karibuni ilitoa shukrani zake za dhati kwa Serikali kwa utekelezaji mzuri sana wa Ilani ya Uchaguzi katika Jimbo la Sikonge na kwa kweli kama Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya nizipokee hizo pongezi na naomba nizifikishe Serikalini kupitia kikao hiki cha Bunge ambayo ilipitia hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, bado ziko changamoto chache ambazo ningependa kuziainisha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mafuriko, hii ni changamoto ni ya nchi nzima, lakini kwetu sisi katika jimbo imekuwa ni changamoto maalum kwa sababu mafuriko yametutenganisha na mawasiliano ya mikoa miwili. Hatuna mawasiliano na Mkoa wa Katavi na hatuna mawasiliano na Mkoa wa Mbeya kwa sababu ya mafuriko. Kwa hiyo, naomba hii changamoto Mheshimiwa Waziri Mkuu aipe kipaumbele cha juu kabisa kwa upande wetu katika Jimbo la Sikonge na Mkoa wa Tabora ili angalau tupate suluhisho la kipaumbele cha haraka sana ili tuweze kurudi katika mawasiliano na wenzetu wa Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Mbeya. Maeneo mengine yote ambayo yameharibiwa na mvua pia ni vizuri yakapatiwa mpango wa dharura wa utengenezaji ili wananchi warudi katika shughuli zao za kiuchumi za kawaida.

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine bado tunaendelea na ufinyu wa ardhi ya kilimo na ufugaji katika Jimbo la Sikonge. Mheshimiwa Waziri wa Maliasili alipotembelea Sikonge mwaka jana alituahidi kwamba Serikali itafanya utaratibu wa kuboresha na kuzipandisha hadhi hifadhi zetu na misitu iliyoko katika Wilaya ya Sikonge ili kupunguza maeneo yale ya misitu ambayo hasa ambayo hayatumiki sana ili kuwaongezea wananchi maeneo ya kulima na maeneo ya ufugaji. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri wa Maliasili kupitia kwako, walikumbuke suala hilo hili mbunga zetu, hifadhi zetu na misitu yetu iboreshwe ipandishwe hadhi ili lipatikane eneo kubwa zaidi kwa ajili ya kilimo na ufugaji.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ni tumbaku, kwetu sisi Sikonge au Mkoa wa Tabora Wilaya kama tatu au nne na baadhi ya wilaya nyingine nchini hapa tumbaku ni uchumi. Sisi ni wategemezi wakubwa sana wa tumbaku ili kupata fedha, wakulima wetu katika kipindi cha miaka mitatu minne iliyopita wamekuwa na changamoto kubwa sana ya soko, sehemu ya kuuzia tumbaku naamini hiyo ni kengele ya kwamba.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana TLTC waliondoka hapa Tanzania, kwa hiyo mnunuzi mmoja amepungua, hata kama hajaondoka TLTC bado tulikuwa na soko finyu la kuuzia tumbaku. Sasa ameondoka TLTC tangu mwaka jana British-American Tobacco wanaomba kuingia kwenye soko la Tanzania na tangu mwaka jana kumekuwa na majadiliano kati ya BAT, Wizara ya Kilimo, na Wizara ya Fedha kuhusiana na masuala ya kodi.

Naomba hiki kikosi kazi cha kodi kitilie maanani na wazingatie wakulima wa tumbaku ili kuhakikisha kwamba kama kuna vipengele vya kodi ambavyo vinahitaji marekebisho, basi vije kupitia Finance Bill ya mwaka huu mwezi sita ili mwezi wa Saba, BAT waingie kwenye soko la tumbaku ili kununua tumbaku.

Mheshimiwa Spika, hiyo itakuwa ni kazi kubwa sana na itakuwa ni mchango mkubwa sana kwa wakulima wetu kwa sababu BAT yeye kwanza kwa miaka miwili ya kwanza ataingia kununua tumbaku ambayo imekuwa inazalishwa kwa ziada na hii tumbaku ambayo imekuwa ikizalishwa kwa ziada, ndiyo tumbaku ambayo wakulima wamekuwa wananyonywa sana.

Mheshimiwa Spika, wiki iliyopita kwa taarifa ambazo tunazo sisi kutoka Tabora, ni kwamba, wapo wakulima ambao walikuwa hawajauza, wameuza tumbaku kilo moja Sh.280 ambao ni unyonyaji wa hali ya juu sana kama anaingia BAT kununua tumbaku imezidi ziada ya mikataba maana yake ni kwamba atanunua kwa bei ambayo alinunua Alliance One ambayo alinunua mnunuzi mwingine itakuwa ni faraja kubwa sana kwa wakulima.

Mheshimiwa Spika, naomba sana Serikali itilie maanani suala hili, vile vingezo ambao walikubaliana, najua Mheshimiwa Bashe ni mtu ambaye amelishughulikia sana suala hili na kwa kushirikikana na BAT na Wizara ya Fedha wamefanya vikao vingi sana tangu mwaka jana, lifikie hitimisho hili mapendekezo ambayo wamependekeza hapo awali yaweze kuingizwa kwenye sheria ili tuweze kupata mnunuzi mpya.

Mheshimiwa Spika, ya kwangu yalikuwa ni hayo kwa niaba ya watu wa Sikonge nashukuru sana. (Makofi)