Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja ya wachangiaji kwa siku hii ya leo.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa neema na rehema zake ambazo amekuwa akitujaalia kwa kila iitwapo leo lakini zaidi sana, napenda sana kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Rais wa Zanzibar pamoja na timu yote ya Mawaziri kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakitekeleza vizuri na kwa uzalendo mkubwa na kwa umahiri Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Wajumbe wote wa Kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi kwasababu wao wamekuwa wakisimamia kwa ukaribu sana utekelezaji huu wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na kwa namna ya pekee nimshukuru sana Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Dkt.Bashiru Ally kwa namna ambavyo amekuwa akituongoza vizuri katika chama chetu lakini pia kwa jinsi ambavyo amekuja Mkoani Mtwara mwezi uliopita na amesimamia vizuri, amekagua miradi ambayo imekuwa ikitekelezwa. Kwa hiyo, nampongeza na namuomba aendelee na moyo huo.

Mheshimiwa Spika, nichukue pia nafasi hii kukushukuru na kukupongeza sana kwa kazi nzuri ambayo unaifanya na niseme hili suala la E-parliament limekuja kwa wakati muafaka kwa sababu nilikuwa najiuliza hapa kwamba ingekuwa ni wakati ule wa kuhangaika na makabrasha sijui kama kuna mtu ambaye angeweza kusoma makabrasha yale kwa sababu kila mmoja angekuwa anogopa kupekuwapekua. Kwa hiyo, nimuombe Mwenyezi Mungu akubariki sana wewe na Naibu Spika, Katibu wa Bunge pamoja na timu yako kwa jinsi ambavyo mmekuwa mkitujali na kuwa na maono ya kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mtwara; Wananchi wa Mkoa wa Mtwara wamenituma nilete shukurani zao za dhati kwa jinsi ambavyo Serikali yetu ya Awamu ya Tano imekuwa ikiwasaidia na ikiweka jitihada katika kuwainua kimaendeleo na kwa kuanzia tu niseme; katika maendeleo ya miradi ya maji tunakwenda vizuri. Manispaa ya Mtwara sasa hivi imefikia hatua ya kupunguza kwa kiasi kikubwa sana mgao wa maji na sasa iko katika hatua za kutengeneza chujio la maji kule Mtawanya.

Mheshimiwa Spika, pia kuna mradi wa Mkwiti ambao una lots tatu; lots mbili ziko katika hatua za utekelezaji lakini kuna lot moja ambayo imebaki na naiomba Serikali sasa iongeze kasi ili kusudi wananchi wa Tandahimba na Newala waweze kupata maji kwa sababu mradi huu wa maji ya Mkwiti utatumika pale lot ya tatu itakapokuwa imekamilika.

Mheshimiwa Spika, nishukuru pia kwa upanuzi wa uwanja wa ndege ambao unaendelea kule Mtwara, lakini pia upanuzi wa bandari ujenzi wa hospitali ya rufaa ya kanda na ujenzi wa hospitali za wilaya pamoja na vituo vya afya ambavyo vinaendelea na vitatusaidia sana kuhakikisha kwamba afya ya wananchi wa Mtwara inaboreka.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa namna ya pekee, nishukuru sana sana kwa ujenzi wa barabara ya uchumi ambao unaendelea kwa sasa, lakini kwa upande huu niiombe Serikali pia iongeze kasi kwa sababu bado kidogo naona kilometa ambazo zimekuwa covered ni chache, lakini naamini kabisa katika bajeti hii tutakuwa tumepiga hatua kubwa.

Mheshimiwa Spika, kama walivyosema wenzangu kuhusiana na ugonjwa wa corona, nami niungane na wenzangu wote kutoa mchango wangu katika eneo hili. Sidhani kama kuna mtu ambaye atakataa kwamba ugonjwa huu hauna dawa ugonjwa, hauna dawa na kilichobaki, ni kumwomba Mwenyezi Mungu. Hili tukimwachia Mwenyezi Mungu naamini kabisa atatusaidia kama alivyotusaidia kutuokoa kwenye kimbunga kilichotokea mwaka jana ambapo hakuna ambaye alitarajia kimbunga kile kisingeweza kutupata, lakini ni kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu kimbunga kile kiliyeyuka bila kutarajia.

Kwa hiyo, naamini kabisa kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu atatuepusha na janga hili, kwa hiyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu kusali na kumwomba Mwenyezi Mungu atuepushe na hili janga laini pia atusamehe popote pale ambapo tumemkosea kwa namna moja au nyingine.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mchango wangu kidogo, Waziri Mkuu ametuambia kuwa, kuna kamati tayari imeshaundwa ambayo inakutana. Sijui wajumbe wa Kamati hii pamoja na kwamba ametuambia ni Mawaziri na wataalam kutoka sekta mbalimbali, lakini napendekeza kwamba tungekuwa na wataalam wa lishe waliobobea ambao wangeingia kwenye Kamati hii, lakini na wataalam wa micro biology, naamini kabisa tunao. Kwa hiyo, wataalam hawa kwa mfano kwa upande wa lishe, ukiangalia clips nyingi sana watu ambao wamekuwa wakishambuliwa na huu ugonjwa wanajitibu kutokana na vyakula.

Mheshimiwa Spika, lakini vyakula hivi vina kazi kubwa sana ya kuzuia nikiwa na maana kwamba kuna kuwa na zile contents ambazo zinakuwa na uwezo mkubwa wa kutoa kinga dhidi ya maradhi ya virus, kwa mfano wengi wamekuwa wakitaja kwamba wametumia machungwa, malimao, tangawizi na vyakula hivi kwa kifupi tuseme ni vile vyakula ambavyo vinakuwa na zinc na vitamin C. Sasa ukiangalia tabia ya zincm ina kazi kubwa sana ya kusaidia kinga ya mwili dhidi ya maradhi mbalimbali. Kwa hiyo niombe tu kwamba wale wataalam wa lishe watatusaidia sana sana kutushauri kwa mfano, katika matumizi ya tangawizi, vitunguu swaumu, mbegu za maboga maziwa korosho na watatuelekeza mazao mengi ambayo yanatoa hivi vitu ambavyo vinatusaidia katika kuongeza kinga ya mwili.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kidogo suala la mafuriko. Suala hili ni matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi na limekuwa likisumbua sana kwa muda mrefu, kwa hiyo, ni ushauri wangu sasa Wizara ya Ujenzi ikae na kuangalia ule mpango ambao nchi yetu uliweka katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na Wizara ambayo inahusika na ujenzi ikae iangalie ni mambo gani ambayo imeyaruka ili kusudi iweze kuyajumuisha katika mpango wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Nimekauka koo, ahsante sana.

SPIKA: Watakuletea maji, watakuletea maji muda si mrefu.

MHE.ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, haya ahsante nasikia kukauka koo sijui ni kwa nini. (Kicheko)

SPIKA: Ahsante sana, Mheshimiwa Anastazia Wambura.

MHE.ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)