Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia nitoe mchango wangu mdogo.

Mheshimiwa Spika, nataka nianze walipomalizia wenzangu kwenye jambo hili la Tume huru ya uchaguzi; katika uhalisia kijana anayedai, anayeomba kuoa katika familia ni kijana ambaYe ana base yaani ameshaonyesha ana mwanga, anajua maisha yake ataishi vipi aidha anafanya kazi au analima ana shamba. Sasa wapinzani kitendo cha kudai Tume huru ya uchaguzi wakati hakuna mlilowafanyia wananchi ni sawa sawa na kijana ambaye kula na kulala bure anayedai kuoa.

Mheshimiwa Spika, wapinzani walipewa Wabunge zaidi ya 100, Madiwani zaidi ya 1500, hamna walichokifanya. Sasa hivi umefika wakati wa uchaguzi wanadai waongezewe tena ili wafanye mabadiliko. Kama mlishindwa hivyo hata tukiwapa Nchi hamna kitu mtakachokifanya.

Mheshimiwa Spika, Chama Cha Mapinduzi tuko tayari kwa uchaguzi. Tumefanya mambo mengi sana. Nimpongeze Mheshimiwa Rais katika kila Nyanja. Niwape mfano, upande wa Vijijini; wananchi wetu wa Vijijini asilimia 90 ni wakulima na wengi wanalima kwa ajili ya chakula. Mwanzo Mwananchi akilima kidebe chake kimoja hawezi kukatisha mageti yalikuwa kibao lakini Rais wetu kwa kuliona hili akaondoa ushuru wote kwa hiyo wakulima sasa hvi ukilima ukiwa chini ya tani moja hulipii ushuru wa namna yoyote. Hizo ndiyo base zetu zinazotufanya twende kwenye uchaguzi kifua mbele.

Mheshimiwa Spika, kwenye mazao ya biashara kama Pamba, Tumbaku, Kahawa, Mkonge, Miwa kodi zilikuwa zaidi ya 140 lakini zimepunguzwa sasa hivi ziko chini ya 125. Hizi zote zinatufanya sisi twende kifua mbele kwenye uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, mtaani, bodaboda niwatolee mfano; wenzetu walikuwa wanawapa viroba bodaboda sisi tumewaondolea kero. Kwa mfano; trafiki walikuwa wanawasumbua sana. Bodaboda akikatiza anapigwa fine 60,000 au 100,000 au 120,000 lakini sasa hivi kipindi kile Waziri ni Kangi alipiga marufuku bodaboda fine ni moja tu na bodaboda zote ambazo zilikuwa kwenye vituo vya Polisi zimefagiliwa zote wamerudishiwa wenyewe sasa hawana watu wa kuwasaidia na hao ndiyo walikuwa watu wanaowasaidia katika kampeni.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Machinga; Machinga zamani walikuwa wanalipia ushuru kila kona wanayokatiza sasa hivi Machinga anapewa kitambulisho cha shilingi 20,000 marufuku kusumbuliwa anakwenda kufanya biashara popote, wao walikuwa wanawatumia katika maandamano.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa wasomi; elimu ya juu tunakumbuka tulikuwa tuna maandamano kila siku, kila Chuo utasikia leo mgomo, kesho mgomo. Zamani mikopo ilikuwa inatolewa kwa matabaka sasa hivi mikopo hakuna kutoa kwa matabaka. Kwa hiyo, Wanafunzi wanapata mikopo kwa hiyo wamekosa watu wa kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, madarasa yanajengwa; juzi World Bank wametuidhnia mkopo wa Dola milioni 500. Wapo wapinzani ambao walikuwa wanakwenda wengine walikwenda hadi nje ya Nchi. kwenye hili nataka kujua, Tume ya Maadili ya viongozi wajibu wapo ni upi? Kiongozi anapotoka kwa ajili ya kwenda kuichafua Nchi huko nje, Tume ya Maadili isiishie tu kuangalia mikopo, madeni na mali zetu, iangalie na viongozi kama hawa. Niwaambie tu viongozi, wazee wetu ambao mnatulea tuko humu, watu kama hawa sijui mmewaleaje mimi hata sielewi.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa ardhi; tumeshuhudia zamani hati ya nyumba, ya kiwanja walikuwa wanapata matajiri tu sasa hivi hadi masikini wa kawaida. Mimi kule Ulanga wamefanya pilot study yaani wamechukua eneo kama ndiyo case study, kila Mtu anayemiliki ardhi anapewa hati bure. Sasa hati ilitoka kutoka miaka 10 hadi wiki mbili. Wizara ya Ardhi pale Mtu anapimiwa kiwanja ndani ya wiki mbili ameshapata haki yake. Zote hizo tunakwenda kifua mbele kwenye uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara na nishati kwenye REA; Vijiji vyote sasa hivi vinapata umeme hizo zote ni nyenzo zetu kwenye uchaguzi ndiyo tunakwenda navyo.

Mheshimiwa Spika, unyenyekevu wa viongozi wetu wa juu; Chama Cha Mapinduzi viongozi wa juu wananyenyekea viongozi wa chini lakini wenzetu viongozi wa juu wanawalangua viongozi wa chini, wanawachangisha michango. Hizo zote ni nyenzo zetu za kwenda kwenye uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Rais wetu, kiongozi ,mwenye maono. Kwanini nasema hivyo? Rais wetu alipoingia madarakani alipiga marufuku safari za nje. Hebu imagine na corona hii maana yake kipindi kile Wabunge badaa ya vikao vya Bunge wote walikuwa wanakwenda nje. Vikao vinapotaka kuanza ndiyo wanarudi sasa Wabunge wangerudi na corona hii tungekuwa wageni wa nani? Kwa hiyo, Rais wetu alikuwa na maono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa vituo vya afya na hospitali za Wilaya; vituo vya afya zaidi ya 400, hospitali za Wilaya zaidi ya 67, hospitali za rufaa. Hivi na corona hii tungekuwa wageni wa nani tusingekuwa na vituo vya afya hivyo na hospitali za Wilaya?

Mheshimiwa Spika, nataka nijikite kidogo kwenye janga la corona; kwanza naomba Wabunge tuambiane ukweli, tofauti ya corona na HIV maana yake wengi wanailazimisha Serikali ianze kupima watu, hiyo siyo suluhu. Tungekuwa na mahali tukishawapima hawa watu tunawapeleka hiyo ingekuwa sawa lakini eti unampima mtu halafu unamuachia aende akarudi nyumbani. Janga la corona uamuzi uko mikonini mwa kila Mwananchi, kila Mwananchi usafi wako ndiyo utakaokupelekea wewe kutokuwa na corona au la!

Mheshimiwa Spika, cha msingi hapa naomba katika Majiji, Wilaya, Halmashauri zetu tutunge Sheria ndogo ndogo za dharura. Kwa mfano; kwenye vyombo vya usafiri kama bajaji na daladala na usafi katika mitaa yetu hiyo itatusaidia. Niipongeze Serikali, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kutokurupuka katika janga hili maana yake kuna Nchi kwa mfano; Nchi za wenzetu jirani wamekimbilia kuna Nchi moja hapo walifunga mipaka wiki tatu zilizopita walizuia Ndege lakini wagonjwa kila siku wanazidi. Sisi hatujafunga mipaka mpaka leo tuna wagonjwa 20. Kwa hiyo, naomba niendelee kuwaasa wananchi wote, kuwapongeza madereva bajaji, madareva bodaboda na wananchi wengine kwa kuendelea kuzingatia haya.

Mheshimiwa Spika, mwisho naomba niongelee suala pensheni; Mheshimiwa Jenista Wazee wa Ulanga watakulaani. Nimetoka Ulanga Wazee zaidi ya 57 wastaafu, walimu waliostaafu tangu mwaka juzi hawajapata kiinua mgongo, hawapati pensheni yao ya mwezi. Hebu imagine mtu amefanya kazi miaka 30 alizoea kila mwisho wa mwezi anapata mshahara leo hii ana mwaka wa pili hajapata pensheni yake, hapati pensheni ya mwezi. Nimeenda Ofisi ya Kanda Morogoro hawana majibu wanasema iko Dodoma. Jamani huo uhakiki gani mtakuja kuwaua wazee wa watu. Wametaka kuja Dodoma kwenye Bunge hili nimewaambia hapana wageni hawaruhusiwi wamesema bora wafe na corona kuliko kufa na njaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa naomba nikupongeze wewe na huu mfumo wa E-parliament kwa kuwa na maono. Hivi leo hii na mavitabu yale tungepona na hii corona? Leo nimeona kuna kigazeti kimoja kimeandika “mnyukano mpya wa Lissu na Ndugai”. Wewe uko imara ndani umewagonga na kanuni wametoka nje na nje wakikuchokoza najua watakutana na bakora.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)