Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia hoja hii muhimu sana ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza, napenda kushukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano na hasa Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya hususani kwenye mambo ya miradi mikubwa ambayo inaendelea. Napenda pia kumsifu Mheshimwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri na Naibu Mawaziri wote ambao wapo katika Ofisi yake, wanafanya kazi kubwa na tunashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kufanya ziara yake Muheza, katika Mkoa wa Tanga. Naamini alipokuja ziara imeweza kufufua mambo mengi na wananchi wa Muheza hawawezi kumsahau hususan kwenye suala la maji ambapo aliongozana na Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Waziri. Kwa kweli kuja kwake kulifanya tenki kubwa ambalo linajengwa pale Muheza la lita laki saba liweze kujaa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua Mheshimiwa Waziri Mkuu aliacha kiporo lakini yale maji kwenye lile tanki la lita laki saba bado yamejaa. Tunaamini kabisa kwamba atakaporudi basi ataweza kuyafungulia na wananchi wa Muheza waweze kupata maji. Nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia napenda kukupongeza hasa katika kuingia kwenye digital, sasa hivi tunatembea na tablet. Hata hivyo, tulikuwa na mawazo kwamba basi Bunge lijalo watakaorudi waweze kuwa na screen katika table zao ingekuwa ni vizuri sana. Tunakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo, napenda kuchangia mambo yafuatayo. Pale kwa Waziri Mkuu kuna Kitengo cha Maafa lakini kwa kweli hakipewi umuhimu unaostahili. Kitengo kile naamini kabisa kina upungufu mkubwa wa fedha na ni vizuri kikaimarishwa kwa sababu mafuriko ambayo yametokea wakati huu wataalam wanasema hatujawahi kuyapata katika kipindi miaka 15 au 20 iliyopita. Kitengo kile kikiimarishwa naamini kitaweza kusaidia sana.

Mheshimiwa Spika, sisi tuliathirika kwa kiwango kikubwa sana kule Amani ambapo kwenye ziara ya Waziri Mkuu pia tulikuwa tumpeleke Amani lakini tulishindwa kumpeleka kutokana na barabara. Mafuriko yaliharibu sana barabara za kule na mpaka sasa hivi barabara za kule vijijini kuna sehemu kata huwezi kupita. Kwa hiyo, tunaomba kabisa kwamba Kitengo kile kiimarishwe na TARURA ambao wanashughulika na barabara za vijijini waweze kuongezewa fedha kwa sababu kazi wanayofanya TARURA ni nzuri, lakini uzuri wake hauonekani kwa sababu ya ufinyu wa bajeti ambayo inapatika.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kushauri kwenye Kitengo cha Uwekezaji cha TIC. Utaona kwamba Kitengo kile kina Mkurugenzi Mkuu mzuri sana na kuna kitu kile wanakiita One Stop Center lakini Maafisa ambao wamewekwa pale hawana uwezo. Maafisa ambao wamewekwa pale kutokana na Wizara zao ili waweze kukifanya kile Kitengo kiwe the real One Stop Center hawa uwezo wa kutoa vibali, leseni, kuangalia ni vitu gani ambavyo mwekezaji anatakiwa kupewa bila kupata consultation tena kutoka Wizarani, sasa hiyo inakuwa siyo One Stop Center. Inatakiwa Maafisa ambao wanapelekwa pale wawe na uwezo wa kuamua, wawe na uwezo wa kutoa vibali na kufanya mambo yote yanayohusiana na mwekezaji. Anachotaka mwekezaji akifika TIC apate vibali vyote pale siyo aambiwe tena aende Labour au TRA, hapana, ule ni usumbufu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni vizuri tuangalie uwezekano wa kukiongezea nguvu. Waheshimiwa Mawaziri ambao wako kwenye Wizara zinazohusika wapeleke Senior Officers pale ambao wanaweza kutoa maamuzi, hapo ndiyo tunaweza kukifanya kiwe One Stop Center.

Mheshimiwa Spika, nilitoa mfano kwamba twende Mauritius, ni nchi ambayo One Stop Center yake wanaiita Mauritius Enterprise, ina lead. Pale mwekezaji akienda, at the time naondoka pale ilikuwa three days anakuwa amepata kila kitu sasa hivi naambiwa ni some hours.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Waziri mhusika kwanza namshauri sana aende Mauritius, aangalie One Stop Center yao iko vipi, Mauritius Enterprise, naamini atajifunza. Hapa tunasema kwamba mtu anapata vibali siku saba lakini mwekezaji anakuja hapa na siku saba hizo anakuwa hajakamilisha kupata vibali vyake. Sasa tutakapokamilisha mambo haya nafikiri yatasaidia sana.

Mheshimiwa Spika, kuna kitu kinaitwa roadmap ambacho amekiongelea Waziri kwenye Kamati na pia blueprint. Ni vizuri hiyo blueprint basi itoke maana imekuwa ni kama kizungumkuti, kila siku inasemwa iko tayari lakini haitoki. Kwa hiyo, ni vizuri mambo haya yaweze kurekebishwa.

Mheshimiwa Spika, kuna miradi mikubwa ambayo imekwama hasa ukiangalia Mradi wa Bomba la Mafuta, umeanza kwa nguvu sana sasa hivi naona mambo yamepoapoa sijui kwa nini. Vilevile LNG Project nayo ilianza kwa nguvu sana imepoapoa. Twende Mchuchuma na Liganga nayo ilianza kwa nguvu sana nayo imepoapoa. Hivi vitu unaambiwa kwamba bado majadiliano yanaendelea, ni vizuri hayo majadiliano yaendelee na yamalizike na kama pia kuna compensation ambazo watu wanatakiwa walipwe basi walipwe.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ni Corona ambalo kwa kweli ni janga kuu Waheshimiwa Wabunge wameliongelea kwa hisia tofauti na kubwa sana. Ni vizuri basi Serikali ikatenga fungu maalum, kwa sababu tumeangalia kwenye Mpango halikuwepo, lakini ni vizuri ikaja hapa na mpango, tusingoje hali ikawa worse tutashindwa kuizuia. Ni afadhali sasa hivi Serikali ije na mpango ambao utaeleza, najua kuna Kamati ambayo imeundwa, lakini Kamati haijaja na taarifa yoyote ambayo inaelezea ni kitu gani hasa ambacho kinatakiwa, kama ni suala la financial basi zitengwe.

Mheshimiwa Spika, hata wewe kwenye Kamati ya Uongozi uliongelea hata Bunge lenyewe lichangia na Wabunge tuchangie lakini tukasema aah, aah. Hata hivyo, ni vizuri pia ukafikiria tena ili tuone kwamba na sisi mchango wetu kama Wabunge, siyo kama ulivyosema siku ngapi zile hata siku moja, siku mbili.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)